Pages

Saturday, June 6, 2015

Mama asoma shule ya msingi na wanae watatu..

Aisha, katikati nyuma akiwa na wanae watatu shuleni
“TANGU nilipozaliwa mkoani Morogoro mwaka 1990, sikupata nafasi ya kujiunga na masomo maana familia yetu ilikuwa ya kuhama hama na baba hakuonesha nia ya kunisomesha kabisa.”

Ndivyo anavyoanza kusema Aisha Ally (25), mama mwenye mume na watoto watatu ambao anasoma nao katika Shule ya Msingi ya Meru, jijini Arusha.

Mama huyo anasoma darasa la tano huku mwanawe Philomena (9) akisoma darasa la nne, Giftgod (5) akiwa darasa la kwanza pamoja na Thecla (3) ambaye yuko shule ya awali hapo hapo katika Shule ya Msingi Meru.

Kisa, huruma Aisha aliyezungumza na gazeti hili wiki hii, amesema matatizo yaliyoikumba familia yao huko nyuma, yalichangia ashindwe kabisa kuhudhuria masomo na badala yake akajikuta akiolewa na kupata watoto.

Kwa mujibu wa Aisha, alipanga kuanza darasa la kwanza kabisa, lakini walimu wa Shule ya Msingi Meru walimshauri aanzie darasa la nne kwani umri wake ulikuwa mkubwa.

Sababu nyingine iliyosukuma walimu watoe ushauri huo kwa mujibu wa Aisha, ni binti yake mkubwa, Philomena ambaye wakati huo alikuwa darasa la tatu na hivyo kama angeanza darasa la kwanza, angekuwa amemzidi mama yake kwa darasa moja.

Viboko
Akizungumza kwa kujiamini, Aisha alisema umbo lake dogo na ufupi wa kimo, vimemsaidia kuonekana kama mwanafunzi wa kawaida kiasi kwamba baadhi ya walimu wasiojua historia yake na wageni, humchukulia kama wanafunzi wengine tu na kumchapa viboko pale anapokosea.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Meru, Mussa Luambo amesema kuna utaratibu maalumu wa kusaidia wanafunzi waishio kwenye mazingira magumu, wakiwemo wale waliokosa elimu utotoni.

Kwa mujibu wa Mwalimu Luambo, Aisha ni miongoni mwa wanafunzi 20 walio kwenye kitengo hicho na baadhi ya walimu wameamua kuchangia fedha kutoka mifukoni mwao ili kuwasaidia.

“Kwa kweli wanafunzi wenye umri mkubwa huwa hatuwachapi kabisa ila tu kwa upande wa Aisha mwili wake mdogo huwa unamponza. Kuna walimu wasiomfahamu hivyo hudhani ni mwanafunzi wa kawaida,” alisema Mwalimu Luambo.

Mtoto ashuhudia
Akizungumza na gazeti hili, binti mkubwa wa Aisha, Philomena alisema; “Wakati mwingine huwa tunachapwa viboko pamoja na maumivu yakizidi mimi na wanafunzi wengine hulia machozi, lakini mama huwa halii kama sisi, tena haogopi wala haoneshi kujali kupewa adhabu.”

Hata hivyo, Aisha anakiri kuwa viboko ndio suala linalomkera zaidi shuleni hapo, kwani akishachapwa fimbo kadhaa za mkononi, baadae inakuwa vigumu kwake kufanya kazi za nyumbani za kufua, kuosha vyombo na kupika.

Biashara
Hivi karibuni alilazimika kuhamisha makazi yake na watoto kutoka eneo la Moshono, alikokuwa akiishi na mumewe Shani Malepu na kuanza kuishi katika chumba cha uani kwenye jengo ambalo amefungua biashara yake ya duka mjini Arusha.

“Kule Moshono ni mbali sana na shule na ilikuwa inatugharimu nauli za kila siku ili kuwahi masomo na mara nyingi tulikuwa tunachelewa kufika shuleni,” alielezea Aisha. Mama huyo ana matarajio ya kuendelea na elimu ya sekondari na anasema kuwa Mungu akimsaidia basi angependa kufika hadi chuo kikuu kabisa.

“Mimi binafsi nina juhudi katika elimu, maana nilianza shule nikiwa tayari najua kusoma maana nilikuwa najifunza mwenyewe nyumbani huku nikiendelea na biashara zangu kama kawaida,” anasema.

Mume
Akizungumza na gazeti hili, mume wa Aisha, Malepu alisema haoni tatizo kwa mama wa watoto wake kusoma shule ya msingi na wanawe. “Ni uamuzi wake mwenyewe na anaonesha kupenda shule.

Tuliwahi kupanga kuwa ajiunge na vyuo vya ufundi stadi, lakini baadaye akaona ni vyema zaidi ajiunge na elimu ya msingi na ninadhani ana mpango wa kuwa mwalimu baadaye,” alisema.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment