Pages

Friday, June 5, 2015

Ni mara ngapi unatakiwa ufue matandiko yako?

Wote tunathamini usingizi mwororo, lakini ni vigumu kuupata kama matandiko ni machafu. Ndipo inaleta maana kuwa matandiko yanapaswa kusafishwa mara kwa mara kadri ya matumizi.
Katika makala ya leo nimefanikiwa kuongea na mtunzaji wa nyumba Bi Joyce Shao na hapa anatuelimisha mengi kuhusiana na usafi wa matandiko. Anaanza kwa kusema kuwa matandiko ni pamoja na mito, shuka, foronya, blanketi, duveti au komfota na godoro. Kwa kanuni ya msingi,  ni vyema kufua shuka na foronya mara moja kwa wiki au kila baada ya wiki mbili.

Kutokufua matandiko yako mara kwa mara kutachangia kuongezeka kwa matatizo ya kiafya kama mzio na pumu. Kama wewe, mwenzi wako au mtoto anaumwa, hakikisha unafua shuka kila siku na kuabadilisha foronya kila siku ambazo mgonjwa analalia.

Wengi wanatumia foronya kuvalisha mito yao, kama unatumia foronya sanasana unatakiwa kufua mito yako mara moja ndani ya miezi miwili, wakati foronya inabidi zifuliwe kila wiki. Mafuta na uchafu kutoka kwenye nywele zetu unaweza kuzama ndani hadi kwenye sponji zilizotengenezea mto. Kufua foronya kutazifanya ziwe safi na kuondokana na harufu mbaya.

Kuhusu muda shuka zinapotakiwa kufuliwa baada ya kutumika kunategemea zaidi na chaguo la mtu. Wapo wanaopenda kufua angalau kila wiki na wapo wanaofua japo kila baada ya wiki mbili. Na hii inategemea pia na mazingira yalipo nyumba, kuna nyumba ambazo vumbi kufika chumbani ni rahisi sana na zipo ambazo vumbi halifiki chumbani. Ni vizuri kuwa na hisia kuwa shuka unazolalia ni safi na kuwa na kitanda kilichotandikwa shuka safi.

Shuka zinapata uchafu na mafuta kutoka kwenye miili yetu  na pia udongo ambao unaweza kusababisha madoa. Hakikisha unacheki na kuondoa madoa kila mara unapozifua. Pia epuka kufua shuka na maji ya moto kwani maji ya moto yatazifanya zisinyae. Unaweza usigundue kusinyaa huko hadi pale unapozirudisha tena kitandani kwa ajili ya kutandika. Maji ya uvuguvugu ni mazuri zaidi kufanya shuka ziwe safi bila kusinyaa.

Kuamua ni kwa kila muda gani kufua blanketi zako inategemea na matumizi. Kama una blanketi mwishoni mwa kitanda ambalo halifunguliwi likatumika, kulifua kila baada ya miezi michache italeta maana. Ila kama blanketi linatumika kila siku au kila usiku unaweza kuhitajika kuliweka kwenye ratiba ya kulifua kila baada ya wiki mbili. Kuwa makini kufuata maelezo ya utunzaji wake kwenye lebo na fua kuendana na muongozo. Kama blanketi halitumiki sana kuwa makini na uchujaji rangi, kama una wasiwasi ni vyema kufua blanketi peke yake bila kuchanganya na nguo nyingine.

Endapo una komfota au duveti ambalo linatumika tu kama pambo la kitanda ukiwa umeshakitandika kukifanya kionekane kunyooka vizuri, kama hamna chochote kilichomwagikia, huna haja ya kuyafua zaidi ya mara mbili kwa mwaka. Kwa ajili kwa kawaida haya ni makubwa ni vyema yafuliwe kwenye mashine za kufulia. Endapo huna mashine hiyo basi peleka kwa dry cleaner.


Kwa upande wa godoro, kutumia foronya la godoro ni njia nzuri ya kuongeza maisha ya godoro lako. Foronya hizi zinazilinda godoro lililoko ndani yake na zinatakiwa kuondolewa na kufuliwa japo mara mbili kwa mwezi. Na pia endapo kuna chochote kimemwagikia ni vyema kuvua foronya na kusafisha doa hadi kwenye godoro kwa kusponji eneo la doa.

Yale matandiko ya ziada kwa ajili ya kupambia kitanda kwa ujumla huwa hayatumiki na kwa maana hiyo hayachafuki mara kwa mara. Kama wewe ni mtu mwenye mzio na vumbi unaweza kuyafua mara moja ndani ya miezi miwili au mitatu. Kwa watu wengine wote yafue mara mbili tu kwa mwaka inatosha.

Kumbuka kuwa matandiko ni yako unayalalia wewe mwenyewe kwahivyo kuyaweka katika hali ya usafi kila wakati ni kwa faida yako.


Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment