Pages

Thursday, August 6, 2015

Jinsi ya kupamba kwa vitu vyenye michoro kama iliyopo kwenye ngozi za wanyama


Michoro kama  iliyopo kwenye ngozi za wanyama haipitwi na wakati iwe ni kwenye nguo, vitupio na hata mapambo ya nyumbani.

Kupamba kwa vitu vyenye michoro hii si jambo jipya. Umaarufu wake unaongezeka kila siku na
kama rangi zimepangiliwa vizuri zinaweza kuleta muonekano maridadi sana. Watu wengi wanapenda michoro iliyopo kwenye ngozi za wanyama kama vile pundamilia, chui, chita na wengine wengi. Miaka ya karibuni mapambo na vitu vya ndani vyenye michoro hii vimekuwa vikiongezeka kwa kasi, kupatikana kwa wingi na kupendwa na wengi.

Ni ukweli kuwa baadhi ya hoteli za kitalii zinapendelea kupamba kwa kutumia vitu vyenye michoro inayofanana na iliyopo kwenye ngozi za wanyama. Nimejaribu kutafiti na jibu nililopata ni kuwa mgeni anayekaa eneo ambalo kiti au zulia lina rangi za michoro ya pundamilia kwa mfano, anakuwa na hisia kuwa yuko karibia na mnyama huyo, kwa kuangalia tu rangi hizo za michoro ya ngozi za mnyama kwenye mapambo yaliyoko pembeni mwake.

Kwa wale wanaopenda asili kupamba kwa rangi za michoro ya kwenye ngozi za wanyama inaburudisha nafsi zao. Inaleta muonekano ambao wenye nyumba wengi wanaupenda na pasipo shaka ni wa kipekee ndani ya nyumba.

Haijalishi msingi wa usanifu wa nyumba yako ukoje, kupamba kwa vitu vyenye michoro kama iliyoko kwenye ngozi za wanyama hakupitwi na wakati, ni kwa jana leo na kesho, ni ustaarabu usioisha. Zamani mapambo ya rangi za wanyama yalionekana kutundikwa zaidi ukutani, lakini kwa sasa utashangaa ni vitu vingapi vya ndani vyenye michoro hii vilivyopo sokoni, kamwe huwezi kukosea kwa kupamba navyo.

Sanaa, samani, malazi, vitupio, mazulia na masanamu ni baadhi ya vitu vyenye rangi za michoro kama ya ngozi za wanyama ambavyo vinakuwezesha kupendezesha nyumba yako zaidi ya mapambo mengine yoyote ambayo ulishawahi kutumia. Hakuna njia mbaya ya kupambia michoro hii, labda tu uwe umechanganya michoro mingi tofauti kwenye chumba kimoja.

Vitupio vya mapambo ndio vingi zaidi tunapotungumzia mapambo yenye rangi za michoro ya kwenye ngozi za wanyama. Michoro ya kwenye fremu yenye picha za pundamilia, twiga na wanyama wengine wa porini nazo ni nyingi na maarufu. Michoro hiyo inaweza kuwa ya nyeusi na nyeupe na hivyo kugeuka kuwa kitovu cha jicho.

Taa za mezani nazo zimekuwa na vivuli vyenye michoro kama iliyopo kwenye ngozi za wanyama na kuzifanya ziwe za mitindo ya kipekee. Vitupio vingine ni kama pazia na mito ya pundamilia na chuichui. Ni ukweli kuwa vyote hivi vinavutia machoni.

Mazulia makubwa ama yale madogo ya kutupia ni njia nyingine pia nzuri na maarufu ya kupamba kwa michoro ya ngozi za wanyama. Zulia zenye michoro ya ngozi za chui, pundamilia na twiga zinapatikana kwa ubora na kwa wingi.

Viti vya mkono navyo ni vifaa vingine vya ndani vinavyoweza kuwa na rangi za michoro kama iliyopo kwenye ngozi za wanyama. Viti hivi huwa vinapendeza vikiwa na michoro mikubwa na iliyokolezwa. Inashauriwa viwe ni vile viti viwili vya sebuleni na sio vya meza ya chakula.

Changamoto kubwa inayoletwa na mapambo yenye michoro ya ngozi za wanyama ni matumizi yaliyozidi. Hapa Bi Zoe ambaye anauza mapambo ya aina hii kwenye duka lililopo katika moja ya hoteli za ufukwe wa Dar es Salaam anashauri kuwa njia nzuri ya kutumia mapambo yenye michoro ya ngozi za wanyama ni kutumia mnyama mmoja au wawili na si zaidi ya hapo kwenye chumba kimoja. Anataolea mfano kwa kuuliza je, unaweza ukawakuta chui, pundamilia, chita na twiga wote wakiwa kwenye eneo moja huko porini? Kama jibu ni hapana basi na ndani ya chumba kimoja usiwaweke wote wanne pamoja.

Baada ya kuona juu ya upambaji wa vitu vyenye michoro kama ya kwenye ngozi za wanyama ni vyema tukumbuke kuwa pamba chumba husika kama vile wewe mwenyewe unavyoupamba mwili wako kuanzia kichwani hadi miguuni. Kama huwezi ukajipamba au ukavaa nguo na vitupio vyenye michoro ya wanyama kuanzia kichwani hadi kwenye unyayo vivyo hivyo na chumba chako usikipambe kwa michoro ya wanyama kila mahali.

Mapambo yenye michoro ya ngozi za wanyama haijawahi kukatisha tamaa. Utakapopamba kwa jinsi ulivyoelimika kwenye makala hii ni ukweli kwamba ndani ya nyumba yako hakutaonekana kama duka la zawadi za vitu vilivyotengenezwa kwa rangi za michoro ya ngozi za wanyama, vilevile haitoonekana kama zoo.


Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment