Pages

Wednesday, September 30, 2015

Jinsi ya kutunza vyombo vya kupikia visivyong’ang’aniana na chakula (nonstick)


Vyombo vya kupikia visivyong’ang’aniana na chakula ni pamoja na masufuria na vikaangio. Vyombo hivi vina tabaka nyembamba ndani mwake linalofanya chombo husika kising’ang’aniane na chakula. Kwa kawaida kusafisha vyombo visivyong’ang’ania na chakula ni rahisi zaidi. Kiasi kidogo tu cha sabuni, sponji na maji ndivyo  unahitaji. Na baada ya hapo ni kuvifuta vizuri kabisa hasa kama maji unayotumia yana chembechembe za chumvi.
Zifuatazo ni dondoo za utunzaji wa vyombo vya aina hii.
Muhimu zaidi ni kufahamu ni nini utumie kwenye kuosha masufuria na vikaangio visivyong’ang’aniana na vyakula. Kamwe usitumie osheo la kukwaruza, badala yake tumia lile ambalo ungetumia kwenye vyombo vya aina nyingine kama vile vya plastiki, udongo ama mti. Hii ni muhimu ili usikwaruze na hatimaye kuharibu lile tabaka jembamba ndani ya vyombo hivi.

Endapo wakati wa kuosha kutakuwa na kaugumu ka chakula kutoka basi loweka chombo chako kwa muda na pia unaweza kutumia maji ya uvuguvugu.

Mara nyingi kile kinachoonekana kama ni madoa kwenye vyombo hivi  huwa ni utando wa mafuta uliojijenga. Tumia sabuni ya kutosha sponji na maji ya moto utamaliza kila kitu. Hii itasaidia kuondoa uchafu wote hadi ule ulio kwenye miisho na mikunjo ya vyombo hivi na hata harufu mbaya.

Usikate chakula ulichopika kikiwa bado  kwenye vyombo hivi kwa kutumia kisu au kitu cha chuma .  Na vilevile wakati wa kupika usitumie kijiko chochote kinachoweza kukwaruza. Yote haya ni kwa ajili ya kuendelea kutunza lile tabaka jembamba la ndani ya chombo husika.

La mwisho ni kuzingatia namna unavyohifadhi vyombo hivi. Watengenezaji wengi wanashauri kuhifadhi vyombo vya kupikia visivyong’ang’aniana na chakula kwa kuvitundika ili kuvizuia visikwazurane. Ila kama huna vitundikio basi inashauriwa kuhifadhi kabatini kwa kufunika bila kutumbukiza kimoja ndani ya kingine lengo likiwa ni lilelile la kuzuia kitabaka cha kuzuia vyakula kungangania kisikwaruzwe au kisiharibiwe na vyombo vingine vya chuma.

Vyombo vya kupikia visivyong’ang’aniana  na chakula vinatakiwa kubadilishwa pale tabaka la ndani litakapoharibika. Wakati huu ni pale unapogundua chakula kuanza kung’ang’ania kwenye maeneo fulani ya chombo na ukiangalia kwa makini utaona alama hizo. Chombo kitaendelea kumomonyoka kwahivyo kukibadilisha ndio uamuzi muhimu. Iwe umewekeza kwenye vyomba vya kupikia visivyong’ang’ania chakula vya bei kubwa au ndogo unaweza kuongeza uhai wa chombo chako kwa utunzaji wakati wa kuosha kupikia na kuhifadhi.


Kwa maswali au maoni tembelea www.vivimachange.blogpot.com

No comments:

Post a Comment