Pages

Sunday, October 4, 2015

AY anataka mwanamke ambaye yuko smart kichwani

 ‘AY’ au Mzee wa Commercial ni mmoja kati ya wasanii ambao kwa muda mrefu sasa wako katika muziki wa kizazi kipya na amefanikiwa kujitunzia jina na ubora wa kazi zake unazidi kukua siku hadi siku.

Moja ya sababu zilizomfanya kufikia hapo alipo ni kutokana na kutambua kipaji alichonacho lakini pia amekuwa akionyesha juhudi binafsi.

Akizungumza na Starehe AY anasema ndoto yake nikuwa mfanya biashara mkubwa ndani na nje ya nchi na juhudi za kufanikisha hilo ameonyesha kupitia baadhi ya biashara alizo zianzisha nchini ikiwemo kumiliki vipindi viwili vinavyotambulika kama ‘Siasa za siasa’ na Mkasi vinavyorushwa katika kituo cha runinga cha Eatv.

Kipindi hicho kinachorushwa kila siku ya Jumatatu na luninga ya EATV ni maalum kwa mahojiano ya watu maarufu wa kada mbalimbali wakiwemo wafanyabishara, wanasiasa na wasanii.
Tofauti na vipindi vingine vya mahojiano, hiki hufanyika eneo la saloni ambapo muhojiwa hupata fursa ya kuchagua huduma yoyote inayotolewa na saluni hiyo huku akiendela na mahojiano ambayo hufanywa na mtangazaji maarufu wa kike Salama Jabiri.
Hata hivyo, katika kipindi hicho Salama anashirikiana na vijana wawili ambao hufanya kazi katika saloni hiyo ambao pia wakati wa mahojiano hufanya kazi ya kutoa huduma kwa mteja wao.
“Kufanya biashara na kuwa mfanyabiashara mkubwa ni ndoto yangu na muziki na umiliki wa vipindi haunipi changamoto sana kutokana na kuwa nafanya kazi na wasomi, wanaojielewa na kazi zao haziingiliani na kazi yangu ya muziki,” anasema.
Kwa mujibu wa AY, muziki kwake una faida na hafikirii kutoka katika tasnia ya muziki kutokana na kuwa ameufanya kwa muda mrefu na azidi kufanikiwa japo miaka mitano nyuma ulikuwa haulipi ukiliganishwa na sasa.

Anataka mwanamke gani?
AY anasema kuwa hajaoa, hana mchumba wala mtoto wa kusingiziwa ingawa anatamani kuwa na mwanamke mwenye hekima,akili zakuleta maendeleo katika familia na nchi kwa ujumla na si urembo pekee.
“Wanawake wazuri wapo wengi, nimekutana na wengi bali kuchagua mke sahihi ni kitu kinachohitaji busara na endapo nikisema niangalie uzuri wa mwanamke nitapoteza malengo yangu,naitaji mwanamke ambaye yuko ‘Smart’ kichwani” ,alisema.
Akizungumzia jina la Mzee wa Commercial’ AY anasema jina hilo alipewa na mtayarishaji wa muziki nchini, Pfunk Majani kutokana na kumuona akiweza kuitendea haki kila aina ya midundo aliyokuwa akipewa wakati wa utayarishaji muziki.
“Wasanii Watanzania ni waoga kuuliza yale wasioyajua au wanayoyajua ila hawana uhakika nayo, wengine hudhani kuwa wanajua mengi kuliko walio watangulia, tusiwe waoga kuuliza na kufatilia yanayohusu tasnia ya muziki ili tuweze kufikia malengo kwasababu muziki ni biashara,”anasema.
Akizungumzia kuhusu siasa, AY anasema kuwa hajawahi kuwaza kuingia katika siasa na wala hapendi japo hana budi kuwaunga mkono wasanii waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
“Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, kila mtu anahaki yakuonyesha mapenzi yake juu ya chama flani, wasanii wanao wasapoti wanasiasa wako sahihi ila nawasihi kuwa makini na kuepukana na rushwa za muda mfupi wakumbuke kwamba kuna maisha. baada ya uchaguzi,”anasema Ambwene.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment