Pages

Wednesday, November 25, 2015

UPI NI WAKATI SAHIHI WA KUWEKA NA KUONDOA MAPAMBO YA KRISMASI?


Chini ya mwezi mmoja ujao tutakuwa na sikukuu ya Krismasi na baadhi ya sehemu hasa kwenye maduka makubwa tayari wameshaweka mapambo ya krismasi ambayo ni pamoja na mti, taa za kumeremeta na kadi.

Lakini je, ni wakati gani unaweka mapambo yako ya Krismasi nyumbani? Na pia je, ni wakati gani unayaondoa? Je, unayaweka wiki kadhaa kabla au unasubiri siku chache tu kabla ya sikukuu?  Au labda hupambi kabisa,  huenda yanawaletea watoto ugomvi na wanakimbilia kuyanyofoanyofoa!

Nimefanya mahojiano na baadhi ya wakazi wa jiji la Dar kuhusu swala hili la ni muda gani muafaka wa kuweka na kutoa mapambo ya krismasi na hapa ni majibu niliyopata. Yasome uyatathmini wewe maono yako je yanaendana na baadhi ya hawa?

“ Mti wangu wa krismasi na mapambo yake nauweka kuanzia tarehe 1 Desemba kila mwaka. Watu hawatakiwi kuamini eti mambo ya bahati mbaya kwamba unaweza kufa kabla ya kuiona sikukuu, ni upuuzi”, anasema Sara kutoka Bonyokwa.

“ Nadhani mapambo ya krismasi yanatakiwa kuanza Desemba 1, yaanze na sherehe za msimu wa sikukuu, na yaondolewe Januari 3 baada ya kuuona mwaka mpya”, anasema Monica wa Gongo la Mboto.

“ Yanatakiwa yawekwe siku 12 kabla Yesu hajazaliwa. Hata hivyo ndio sababu ya mapambo haya”, anasema Robert wa Kinyelezi.

“Nadhani mapambo ya Krismasi yanatakiwa yawekwe toka Novemba, ambapo ni vizuri kwani yananyanyua mioyo ya watu ndipo wanaanza kujitayarisha!”, anasema Shana wa Mbuyuni.

“Nyumbani kwangu, huwa tuna kawaida ya kuweka mapambo ya Krismasi toka mwezi wa tisa lakini pia  ni wazo zuri kuyaweka kuanzia Desemba 1 kwasababu ndio mwanzo wa sikukuu ya Krismasi”, anasema mama mchungaji Anna wa Mzambarauni.

“Mimi ni Muislam kwahivyo sisheherekei Krismasi. Lakini bado nawapa watu kadi na zawadi kwasababu ni msimu wa sikukuu” , anasema Asia wa Kitunda.

“Nadhani mapambo yenu ya Krismasi myaweke Desemba, lakini baadhi ya watu na maduka wanaweka toka Novemba. Inasikitishaje? Anasema Dominic wa Vingunguti.

“Nadhani mapambo ya Krismasi yaanze kuwekwa Desemba 1 na yaondolewe mara baada ya mwaka mpya, anasema Elli wa Tabata.

“Nadhani kuanza kuweka mapambo ya Krismasi Novemba ni mapema sana. Ya kwangu nayaweka Desemba 1, lakini baadhi ya marafiki zangu wanasubiri hadi siku ya mkesha wa Krismasi ndio wanaweka. Mimi siwezi kusubiri hivyo! Sijui ninachopendelea zaidi kwenye mapambo haya ila kikubwa ni furaha tu kuwa sikukuu iko njiani”, anasema Lizi wa Karakata.

“Yanatakiwa yawekwe tarehe 1 Desemba ili yaanze na kipindi cha majilio”, anasema Anna wa Banana.

“Familia yetu inajali sana kipindi cha Krismasi. Tumeshaweka mapambo yetu yote tayari, na kipindi hiki baba amenunua taa nyingi za vimulimuli kwa ajili ya kuzungushia nje. Nyumba yetu inaenda kupendeza sana!”, anasema Stela wa Segerea.

“Krismasi sio kuhusu mapambo wala santa klausi, ni kuhusu Kristo. Sisi hatujali kuweka miti wala mapambo”, anasema Tom wa Mbuyuni.

“ Sisi hatuweki mapambo yetu hadi  baada ya siku ya kuzaliwa ya babu ambayo ni Desemba 15. Wote wanakuja na tunasheherekea pamoja Krismasi”, anasema Jesca wa Kitunda.

“Nadhani watu wanatakiwa kuwa na mapambo yanayohusu utamaduni wao kwasababu Krismasi ni kuhusu kuzaliwa mkombozi na sio Santa. Watu wanayapaisha mapambo na kufikiria tu zawadi na sherehe; inatakiwa kusherekea kuzaliwa Kristo. Kwahivyo weka mti wiki moja kabla ya Krismasi”, anasema Bella wa Bonyokwa.

“ Sisi tumeweka yetu leo! Najua ni mapema kidogo lakini kwa maduka yaliyoko kwenye jengo hili sisi ndio wa mwisho! Wenzetu wote wameshaweka” , anasema Bertha wa Segerea

“Mimi sisheherekei Krismasi, lakini nadhani hao wanaosheherekea inawapasa kujiandaa mapema iwezekanavyo ili kuwa na muda na nguvu za kutosha” anasem Ndita wa Makoka.

“Huwa tunaweka mapambo yetu kwenye tarehe 12 Desemba. Sioni ni kwanini maduka mengi makubwa yanaaza kuweka toka Oktoba hadi mapema Novemba”, anasema Margareti wa Mbuyuni.

“Mti wetu wa mwaka jana ndio tumeutoa stoo jana tumeanza kuunganisha na tutaupamba leo!”, anasema Lucy wa Kipawa.

Msomaji wangu umeona mawazo mbalimbali kuhusu wakati muafaka wa kuweka na kuondoa mapambo ya Krismasi. Tukutane hapahapa wiki ijayo.

Makala hii imeandaliwa na Vivi.
Je, unauza bidhaa au huduma inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue? Nijulishe simu/whatsapp 0755200023

www.vivimachange.blogspot.com

2 comments:

  1. Mi hata sijui nashangaa nikirudi nyumbani kuna mapambo, baada ya krismas hivyo hivyo nashangaa hakuna mapambo.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Safi sana Matola, yaonekana una ubavu mzuri anayetunza nyumba vyema

      Delete