Pages

Thursday, December 31, 2015

KUTOKA KWANGU:....Jinsi ya Kupamba Jiko kwa Kuongeza Rangi


Huenda uko kwenye mchakato wa kumalizia chumba cha jiko au labda unakifanyia marekebisho. Jiko la rangi moja linapooza, ukiongeza rangi ndipo unajisikia kweli unapika.

Hizi hapa ni njia unazoweza kutumia ili kuongeza rangi jikoni:

Kuweka marumaru za rangi tofauti kwenye eneo dogo la ukutani.
Marumaru hizo zinaweza kuwa ni zile za michoro inayohusiana na mambo ya jikoni kama vile zilizochorwa vyakula, laa zinaweza kuwa ni ukanda mwebamba wa rangi tofauti na ya zilizoko kwenye sehemu kubwa ya ukuta. Eneo hilo liwe ni la juu ya kaunta ili paonekane vizuri. Cha muhimu ni ziwe na uwiano wa rangi na maeneo mengine ya jiko.

Kuboresha makabati. Huna haja ya kuyaondoa ila unaweza kuyapaka rangi mabayo unadhani itafanya jiko lichangamke na liwe na mvuto. Vilevile kumbuka kupaka rangi ambayo itashirikiana na ya kuta. Kwa kupaka makabari rangi ya kuchangamka utaliongezea jiko lako uhai kwani sehemu kubwa ya jiko inayoonekana ni makabati kuliko hata ukuta.

Weka vitendea kazi ambavyo vinaongeza rangi. Vifaa vya jikoni kama vile jokofu, kipasha chakula na visaga vyakula unaweza kuvipata kwa rangi tofauti tofauti. Kama nia yako ni kuongeza rangi jikoni basi chagua vitendea kazi vya rangi mbalimbali.

Weka sanaa za rangi mbalimbali. Rangi kama nyekundu, zambarau na jamii za bluu zinavuta jicho kuzitazama zaidi. Sanaa za kuning’niza zinatengeneza maeneo ya mvuto jikoni na pia zinatoa utambulisho wa mwenye nyumba. Sehemu yenye nafasi nzuri ya kuzitundika ni juu ya dirisha, na hii ni kwakuwa pia wengi hawaweki pazia jikoni kwahivyo mahali hapo ni sahihi kutundika sanaa zako za ukutani za jikoni.

Ongeza rangi kwenye shelfu. Kuna wale wenye majiko makubwa yenye eneo la shelfu za wazi. Kama umebarikiwa kuwa na jiko la aina hii basi unaweza kutumia eneo hilo aidha kulipaka rangi au kuweka vyombo vya rangi. Kama utaamua kupaka shelfu rangi basi weka sahani nyeupe, ila kama utaacha shelfu na rangi yake ya asili au na rangi nyeupe basi weka sahani na vyombo kama vile majagi na mabakuli makubwa ya rangi. Kwa namna hii ni kama mashelfu yanaongea na mtazamaji.

Zama kwa undani zaidi. Maadam mkakati wako ni iwe iwavyo unataka kuongeza rangi jikoni basi zama hadi kwenye vitu vidogodogo. Hapa ni pale ambapo umeshafikiria yale maeneno makubwa kama makabati, kaunta, ukuta, sakafu na vifaa. Sasa zama kuongeza rangi kwa kupitia vitu kama vile vikombe, glasi na vikontena vya kuhifadhia vyakula.

Bila shaka msomaji wangu kama ulikuwa unawaza ni kwa namna gani upambe jiko lako, makala hii itakuwa imekupa mwanga wa nini cha kufanya.

Ukishapamba nishirikishe kwa simu/whatsapp 0755 200023 ili tuzidi kuelimisha na wengine.



No comments:

Post a Comment