Pages

Wednesday, January 27, 2016

KUTOKA KWANGU:....Dondoo 7 za kuongeza mwanga kwenye chumba chochote


Wengi wetu tuna vyumba ndani ya nyumba zetu ambavyo havipati mwanga wa kutosha kiasi ambacho tungependa iwe. Pazia nzito, zulia au sakafu ya rangi za giza na rangi ya ukutani isiyo sahihi vinaweza kuwa ndivyo vinachangia chumba kisiwe na
mwanga wa kutosha.

Kama unataka chumba kiwe na mwanga wa kutosha wakati wa mchana iwe kuna mawingu ama laa, chukua muda kufanya maboresho ambayo inabidi yafanyike. Dondoo hizi 7 zitakusaidia kuwa na mwanga wa kutosha katika chumba chochote.

1. Kuwa makini na pazia. Wakati wa kutundika pazia kwa ajili ya faragha au umaridadi wa chumba hakikisha unatumia fimbo sahihi. Hii ina maana kuwa fimbo za pazia ziwe laini za kuteleza kwa kuweza kuruhusu pazia kufunguka kwa urahisi hadi mwisho.

2. Paka ukuta rangi nyepesi. Maeneo kama sebuleni rangi nyepesi kwa maana ya rangi za mwanga huwa hazipitwi na wakati. Na hata kama unapendelea rangi nzito basi waweza kuzihusisha kwenye maeneo mengine kama vile sofa au zulia. Vitu vichache vyenye rangi nzito ni sahihi kwa kuchangamsha na kuchombeza  sebule huku ukuta ukiwa ni mweupe.

3. Sambaza mwanga unaoingia.
Tumia kioo kikubwa kurudisha chumbani mwanga kidogo unaopatikana. Kiweke mkabala na dirisha ili kisambaze mwanga wa jua unaoingia kupitia dirishani.

4. Achana na pazia nzito. Kama suala la faragha ni muhimu sana kwenye chumba unachotaka kuongeza mwanga, hilo lisikupe tabu. Weka pazia nyepsesi lakini zenye maua mengi madogodogo na yaliyo karibu karibu. Pazia za namna hii zitaruhusu mwanga wakati huohuo zikiwa zinasisitiza faragha.

5. Mfumo mzuri wa taa. Zifuatazo ni aina ya taa unazoweza kuweka chumbani. Taa za kuninginia, za kuchimbia kwenye dari, za ukutani na mezani na za kusimama toka sakafuni. Mfumo huu mzima ni muhimu sana kwa chumba kisichokuwa na mwanga wa jua wa kutosha.

6. Ondoa ukuta unaotenganisha sebule na chumba chakula. Kama nia ni kuongeza mwanga sebuleni au kwenye chumba cha chakula, ni kwamba  vyumba hivi viwili visipokuwa na ukuta unaovitenganisha inasaidia kuongeza mwanga. Kama bado itaonekana ni muhimu kutenganisha vyumba hivi viwili labda kwasababu ya kiyoyozi au sababu nyingine yoyote basi tenganisha kwa milango ya vioo na hasa ile ya kufungua kwa reli.
Pia kama kuna mlango wa ndani wa kuingia sebuleni badala ya wa mbao weka wa kioo. 

7. Ongeza vitu vya kung’aa. Sio tu vioo vya ukutani vinavyoweza kusambaza mwanga chumbani. Vitu vya kung’aa kama vile glasi na silva vinasaidia kuongeza mwanga kutokana na kule kumeremeta kwake.

Kipe chumba mwanga wa kutosha. Bila shaka dondoo moja wapo kati ya hizo zitakusaidia kukipa chumba mwanga wa kutosha unaohitaji. Niambie dondoo zako za namna unavyohakikisha unapata mwanga wa kutosha nyumbani kwako.


Kupata ushauri wa mapambo ya nyumba na bustani nijulishe. Let's meet 0755 200023

No comments:

Post a Comment