Pages

Monday, February 1, 2016

Kanuni 5 za kusimamia kwa mafanikio mradi wa ujenzi wa nyumba ya kuishi


 Leo nimeona niandae makala kuhusu namna mwenye nyumba anavyoweza kusimamia kwa mafanikio mradi wa ujenzi wa nyumba yake.  Baadhi ya wazazi wa familia changa wanaanza ujenzi bila kuwa na
uzoefu wowote na wakati mwingine baba yuko na pilika za kutafuta riziki ya familia wakati mama akiwa ndio msimamizi wa ujenzi huo. Hivyo basi kwa kuliongelea hili litawasaidia wale wanaojenga kwa mara ya kwanza na pia wale wenye mpango wa ujenga siku za mbeleni.

Nimeongea na mhandisi wa majengo bwana Kassim Ally na hapa anatujuza kama ifuatavyo. Wakati wa kufanya kazi kubwa ya ujenzi wa nyumba ya kuishi, mambo kama wauzaji wa vifaa bora, gharama na muda ni mambo yanayotakiwa kutiliwa maanani. Ingawa kuwa na uwezo wa kufikiria mbele katika kila hatua ya ujenzi ni lazima, kazi yenye mafanikio inahusisha pia ushauri wa malighafi zinazotakiwa kwa hatua hiyo.

Kila mmoja ambaye ameshawahi kujenga au kusimamia kazi ya ujenzi anajua ni kwa namna gani ilivyo na changamoto nyingi. Hivyo basi kusaidia kuwezesha mradi ufanikiwe, hapa ni kanuni 5 za namna ya kusimamia ujenzi wa nyumba ya kuishi ili kuhakikisha unapata matokeo uliyoyataka.

1.     Andaa mipango mapema
Ujenzi usiokuwa na mipango iliyoandaliwa ni moja ya changamoto kubwa kwenye ujezi wa nyumba za makazi. Ingawa dharura bado inaweza kuwepo lakini mambo mengi yanaweza kukamilika kirahisi pale kunapokuwa katika mipango ya mapema. Mambo kama hali ya hewa ya wakati wa ujenzi ni lazima yafikiririwe vinginevyo yanaweza kusababisha gharama za ziada kwa kusababisha mradi kuchelewa. Kimsingi kila kitu ambacho kinaweza kukwamishwa ujenzi lazima kifikiriwe kwanza.

2.     Pitia bajeti yako kila wakati
Katika ujenzi wowote uwe mdogo au mkubwa, ni vyema kuwa na pesa ya kutosha hadi kumaliza hatua fulani. Kabla hujaanza kuongea na mafundi, unapaswa kujua hali yako kipesa na uhakika wa wapi unapata hela ya nyongeza endapo utakwama. Mara nyingi miradi ya ujenzi inaishia kuongezeka bajeti ya kati ya asilimia 10 hadi 15, ni lazima kila siku uweke jicho kwenye hela uliyonayo na matumizi yanayotakiwa.

3.     Chagua watu sahihi
Hakikisha unampata fundi mkuu aliye sahihi. Anatakiwa aijue bajeti yako kwani ana uwezo wa kukupa mbadala na ushauri uli ufanye matumizi ya busara.

4.     Mfanye kila fundi ajue kifuatacho
Kama tunavyojua ujenzi unapitia hatua mbalimbali, na ili kuondoa lawama au hasara inayoweza kusababishwa kati ya fundi wa nyuma na anayemtangulia ni  vyema kuhakikisha kuna mawasiliano na kila fundi aliyeko eneo la ujenzi. Kunapokuwa na mawasiliano kati ya mafundi kunasaidia kushughulikia mapema na mara moja tatizo ambalo limejitokeza.

5.     Amini dhamira yako na furahia nyumba yako mpya
Ujenzi wa nyumba ya kuishi bila shaka ni ujenzi wako wa kwanza kusimamia hadi kukamilisha. Unaweza kuwa umechoshwa na maelezo mengi na michakato uliyopitia. Cha muhimu ni kwamba wakati unafanya maamuzi yoyote juu ya nyumba yako hiyo, amua kile ambacho unaamini kuwa ni sahihi kwako.
Safari ni ndefu na bila shaka unataka kuhakikisha unafurahia matunda yake.


Nishirikishe ulivyosimamia mradi wa ujenzi kwa mafanikio. Mawasiliano 0755200023. 

No comments:

Post a Comment