Pages

Wednesday, February 17, 2016

KUTOK KWANGU:...Dondoo za maandalizi ya kupamba nyumba yako


Kupamba nyumba inaweza kuwa kazi ngumu na ya muda mrefu kwa baadhi, ingawa pia wapo wanaoona ni kazi ya kuvutia na wanaifurahia. Haijalishi wewe uko kwenye kundi gani lakini ni kwamba inaweza kukuchukua miezi kupata pambo dogo tu kama vile picha unazotaka kutundika ukutani ambazo unaamini utazipenda kuziangalia kila siku. Ukweli ni kwamba vitu vya nyumbani vimetawanyika kwenye masoko mbalimbali na vingine ni vidogodogo kiasi kwamba vinachukua muda mrefu kuvikusanya pamoja. Na vilevile inategemea na kipaumbele cha mwenye nyumba kwamba ni nini anataka kwa uwezo na umuhimu wa kuwa nacho kwanza kabla ya kingine.
Kwahivyo kazi ya kupamba inaweza kuwa ni ya kudumu au laa ikachukua muda mrefu tu.

Mambo matatu muhimu sana katika
mapambo ya nyumbani ni kupata vile vitu ambavyo unavipenda haswa, viwe katika ubora unaokubalika na viuzwe bei ya kawaida unayoweza kuimudu. Kuna maeneo mengi wanauza au kutengeneza vitu vya kuwa navyo ndani ya nyumba.  Unapoanza  kupamba nyumba yako hizi ni dondoo chache za kukuwezesha kufanya maandalizi:

Usijaribu kupamba vyumba vyote kwa wakati mmoja. Fikiria kwanza picha halisi ya chumba kimoja jinsi unavyotaka kionekane. Huenda ni chumba chako, au cha mtoto wa kiume, au wa kike, sebule, jiko, bafu, ofisi ya nyumbani au hata chumba cha wageni. Kuna mawazo lukuki kama vile rangi, taa, maua, karatasi za ukutani, mazulia na aina ya upambaji iwe ni wa kisasa au wa saresare. Kwahivyo kuwa mbunifu, hapa ndipo mahali unapoweza kuleta uwakilishi wako kwenye nyumba yako. Onyesha vitu unavyopenda.

Ukishakuwa na wazo tayari, chagua chumba kimoja na uanze nacho na andaa orodha ya vitu unavyotakiwa kununua kwa ajili ya chumba hicho. Je unataka kukipaka rangi upya? Kuongeza rangi ukutani kunaleta uhai wa chumba. Anza na eneo kubwa la chumba halafu malizia na vitu vidogo vidogo kama vile saa ya ukutani au taa za mezani.

Angalia bajeti yako. Je ni kiasi gani cha pesa uko tayari kukitumia. Chukua muda kidogo kuwekea bei kila kifaa ambacho umeorodhesha ili upate picha ni kiasi gani cha pesa unahitaji. Ukishajua hili itakupa moyo wa kuanza zoezi la kupamba.

Kuwa na orodha yako kila wakati ukijua ni nini unachotaka kununua na kipo kwenye hali gani. Tumeona vitu vya nyumbani vilivyokwishatumika tayari iwe ni hapa nchini au nje ya nchi, japo vipo kwenye hali nzuri vikiuzwa. Fungua macho yako wakati unaponunua. 

Chukua muda kuangalia huku na kule kuona ni nini kipo, kipo wapi na kwenye hali gani. Baada ya muda utakuwa umeshajua kabisa ni nini unanunua wapi na kwa bei nzuri. Unaweza kununua vitu vyako kwa kasi yako mwenyewe. Wakati mwingine hutakiwi kuwa na haraka kwa ajili kwenye harakati zako unaweza kukutana na kitu ambacho kweli umekipenda sana na kinaweza kukupa wazo jipya la kupamba.

Kusema kweli kupamba hakuna muda maalum ni kama vile ni tendo endelevu. Jipe muda wa kutosha ili upate muonekano unaotaka.
Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023


No comments:

Post a Comment