Pages

Tuesday, February 9, 2016

KUTOKA KWANGU:..Tumia saa za ukutani kufahamu muda kimtindo!

Hakuna ubishi kwamba siku maalum kwenye maisha yako zinaweka kumbukumbu za wakati huo. Na kinachoanza kusema wakati ni saa.
Saa za ukutani zinaweza kuonekana si chochote kama kifaa cha mapambo ya ndani lakini kama ukichagua kwa umakini zinaongeza maana ya kuwa matumizi  na hapo hapo pambo. Kuna watu ambao wanalijua hili na wanaweza kuchukua muda mwingi kuhangaika kupata saa zenye muonekano sahihi wa kuendana na mapambo yao ya
ndani. Saa zikatumika kuwaambia muda na wakati huohuo zikiongeza mvuto ukutani.

Zifuatazo ni dondoo za jinsi taa za ukutani zinavyoweza kutumika kama pambo la ukutani:

Unaweza kuweka saa tofauti  na pia zaidi ya moja kwenye kila chumba.
Saa za ukutani zenye muonekano wa pambo ziko za mitindo mingi na zinapatikana kirahisi na hata bei zake sio kubwa, Zipo ambazo fremu zake ni za mbao na zimenakshiwa kwa mikono, zipo za chuma na zipo za plastiki ngumu. Na hata za madini ya thamani kama silva huwa zipo.  Cha muhimu zaidi kukumbuka wakati unachagua saa za ukutani zenye muonekano wa pambo, chagua ambayounajisikia kwamba inakuwakilisha wewe na kwa kiasi fulani inaboresha muonekano wa chumba chako.

Kutundika saa za ukutani hakuna tofauti na kutundika fremu za picha au michoro chumbani au kwenye ujia. Ni sehemu ya mapambo kwa ujumla wake.  Kwa ajili saa za ukutani sio gharama kubwa unaweza kuwa nazo kadhaa. Moja ya mtindo wa kupamba kwa saa za ukutani ni kuzitundika kadhaa mahali pamoja kwenye mstari. Unaweza kuziwekea muda wa saa halisi katika miji maarufu ya maeneo tofauti ya dunia. “Watoto wangu wanaishi ng’ambo na nimeweka saa tatu kuonyesha muda wa Chicago, London na Dar es Salaam katika mstari mmoja,” anasema Merina Ruge, ambaye ni mkazi wa Kunduchi, Dar es Salaam.

Kutundika saa nyeusi kwenye ukuta wenye rangi nyepesi kunatengeneza mwelekeo wa jicho la mtazamaji.
Muundo wa saa ya ukutani unachangia muonekano wa pambo, kwa mfano saa ikiwa ya muundo wa kinyumba cha ndege bila shaka ni ya kipekee. Muundo mwingine wa saa unaoweza kufikiria ni zile zenye mlango wa mbele wa kioo. Miundo ni mingi mizuri na ya kipekee kwa mfano zipo saa zinazoonekana kama ni fremu za picha.
Unaweza kutundika saa kutokana na matumizi ya chumba. Kwa mfano saa ya jikoni unaweza kutundika yenye muundo wa matunda. Kwa  ukuta wa chumba cha watoto vilevile weka saa zinazoendana na umri na jinsia yao.

Kama umetundika saa ya ukutani kumbuka unastahili kujua muda kimtindo, na hakuna kizuri zaidi ya saa sahihi kwako. Kwa muda wa furaha na wa huzuni, saa ya ukutani haikuachi!


Vivi ni mashauri wa mapambo ya nyumba. Kama kuna lolote linakutatiza kuhusu mapambo ya nyumba na bustani yako wasiliana na mimi. Nimekuwa kwenye huu wigo kwa muda mrefu sasa kwahivyo nina uzoefu wa vingi. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment