Pages

Tuesday, March 22, 2016

Faida za kumhusisha mtaalam kufremu picha unazotaka kutundika ukutani

Huenda ndio umetoka fungate na umepokea picha zako za harusi, kwahivyo wewe na mume wako mnaanza kufikiria na kuchambua ambazo mngependa kukuza na kutundika ukutani. Au labda umepata mtoto na ni wakati wa kumuongeza kwenye hazina ya picha za familia ulizotundika ukutani. Vyovyote vile, kufremu picha ni sanaa inayohitaji msanii anayeijua vizuri kazi hiyo.

Fremu za picha iwe ni za mbao, plastiki au chuma huwa zinahusisha miundo ambayo picha inapowekwa ndani yake inaruhusu kuwa kivutio kwa wale wanaoitazama. Fremu yenyewe tu ni sanaa ambapo utakapochagua ya rangi na muundo sahihi bila shaka inajisimamia yenyewe kabla hata haijawa na picha ya ndani!

Ingawa ni ukweli kwamba wapo watu wanaonunua fremu na kuweka picha peke yao, ni vyema kufahamu kuwa msanii wa picha na fremu ana uzoefu na utaalam wa kujua ni fremu ipi inafaa kwa picha ipi. Na pia anajua hatua sahihi za kupitia ili kufremu picha katika ubora unaokubalika. Fikiria thamani ya picha zako kwa
maana ya muda, maandalizi na gharama uliyotumia kuzipiga. Bila shaka usingependa kuwa na matokeo ya mwisho ambayo hutayafurahia.

Zifuatazo ni faida za kumhusisha msanii kufremu picha zako badala ya wewe kufanya mwenyewe:

Kuokoa muda
Unapoamua kukaa chini na kufremu picha zako, hakuna shaka kuwa utachukua muda mrefu sana kwani huna uzoefu wa kazi hiyo. Msanii atafanya kwa muda mchache zaidi kwa kufuata hatua sahihi na mwisho kupata matokeo mazuri kimuonekano na imara kwa kutokuwa na wasiwasi kwamba labda fremu yako itasambaratika baada ya muda au pengine ianguke na kuvunjika.

Usahihi wa kufremu
Hata kama utanunua fremu zenye mvuto kiasi gani kufremu picha zako mwenyewe ni ngumu kupatia hasa kwenye kona. Na mtazamaji ataona tofauti tu kati ya picha uliyofremu wewe na aliyofremu msanii. Hii ni kwasababu msanii ni kazi yake na anafuata hatua sahihi. Pia ukubwa na muundo wa fremu unahusika kwenye sanaa ya utundikaji wa picha hizo mara baada ya kuzifremu. Kwa mfano fremu zinazofanana na kulingana zinapendeza zikiwa eneo moja na katika mstari mmoja. Msanii wa fremu anajua haya yote ambapo wakati wa kufremu anazingatia matokeo ya mbeleni pia.

Vilevile msanii anajua namna ya kufanya picha ya ndani isichezecheze kwenye fremu yake. Na ni jinsi gani aifunge fremu eneo la nyuma endapo mbeleni utataka kufungua na kubadili picha. Msanii anajua kioo kipi kitafaa kwa fremu ipi.

Aina za kufremu
Msanii wa picha na fremu anajua aina mbalimbali za kufremu kutokana na jinsi picha ilivyo. Zipo picha zenye kingo na zipo ambazo zimejaa kwenye karatasi nzima yaani hazina kingo, na vilevile msanii mtaalam anajua picha ya ukubwa upi inaendana na fremu ipi.  Bila kusahau kufremu pia kunatokana na wingi wa sura kwenye picha husika. Kwa mfano endapo picha ina watu wengi basi fremu inatakiwa kutokuwa na madoido. Vile vile rangi ya picha inahusika kwamfano kama picha ni ya nyeusi na nyeupe inapendeza kwenye fremu ya rangi nyeusi na isiyo na madoido. Fremu na aina za kufremu vilevile zinazingatiwa kwenye kufremu picha za watoto.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment