Pages

Tuesday, June 21, 2016

Dondoo muhimu wakati unapotaka kununua zulia

Hakuna sakafu ambayo ni laini na yenye hisia za kifahari kama ya zulia. Ndio maana ni utamaduni wa dunia nzima kwa watu mashuhuri kutembea juu ya zulia wakati wa dhifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

Zulia ni sakafu yenye usalama zaidi kwa michezo ya watoto na hata
uwezekano wa wao kuanguka na kuumia ni mdogo. Ni ukweli kuwa zulia linahitaji utunzaji wa ziada ukilinganisha na sakafu nyingine kama za marumaru au tarazo. Kuwepo kwa rangi, malighafi na mitindo mingi ya mazulia, inaweza kukuwia vigumu kuchagua lililo sahihi kwa ajili ya nyumbani kwako. Rangi nyingine zinaweza kuhitaji usafi wa kila mara ambapo haitaendana na ratiba yako ya mchakamchaka wa kila siku. Vilevile mazulia yenye rangi moja na zilizokolea sana yana tabia ya kupauka. Endapo unaweka zulia la namna hiyo sehemu linayopitiwa zaidi ina maana sehemu hiyo itaacha alama za kupauka.  Mazulia ya hivi yanafaa zaidi kwenye chumba cha kulala kuliko sebuleni au kwenye corridor. Zulia lisilo sahihi linaweza kuchakaa haraka, kupauka au kung’ang’ania madoa hata kama utalisafisha vipi. Tumia fedha zako kwa akili wakati wa kununua zulia kwa kuzingatia dondoo hizi.

Bajeti
Bajeti ni dondoo muhimu sana ambayo ndio itasimamia nyingine zote zinazofuata. Utagundua kuwa kuna tofauti kubwa ya bei kati ya mazulia ya manyoya ya unene fulani ukilinganisha na ya unene wa tofauti yake. Ukiwa tayari una bajeti yako ni rahisi kuamua ni zulia lipi unaloweza kumudu.

Ubora
Ubora hapa tutauangalia katika nyanja mbili, kwa zulia jipya au la mtumba. Kwa mazulia mapya najua baadhi ya wanunuzi hapa nchini hasa kwenye miji mikubwa wamezoea kwenda kununua kwenye eneo moja tu kwa sababu labda ndilo wanaloamini kuwa wanaweza kupata mazulia. Ila kiukweli kuna showroom nyingi zenye mazulia tofauti tofauti ya kutoka nchi mbalimbali na ubora wake vilevile ni wa ngazi tofauti tofauti.  Zulia unalotaka kununua hakikisha lina manyonya yaliyojishindilia. Hutataka kununua lenye manyoya machache kiasi kwamba baada ya muda mfupi linachakaa. Unahitaji zulia lenye ubora wa hali ya juu ambalo linakuhakikishia kuwa nalo miaka mingi hadi ulichoke mwenyewe uamuae kulibadilisha.

Kwa upande wa zulia la mtumba cha muhimu ni kuhakikisha unachagua lile lililo kwenye hali nzuri zaidi ambayo unaweza kuiamini.  Uzuri wa mazulia mengi ya mitumba ni kwamba yanaonyesha mwaka yaliyotengenezwa kwahivyo ni rahisi kugundua ubora wake kwa kuangalia ni muda gani limetumika.
Na pale unapotaka kununua vizulia vidogo vya milangoni au bafuni, ni vyema kuhakikisha vina ule mpira eneo linaloshikana na salafu ili kuzuia utelezi na pia majimaji kupenya kwenye manyoya.

Ukubwa
Ukubwa wa zulia unalotaka kununua ni kigezo muhimu cha kufanya maamuzi. Hakikisha unapima eneo unalotaka kuliweka ili uweze kutambua ukubwa sahihi wa zulia unalohitaji. Sichoki kusisitiza kuwa fenicha zinatakiwa zikae juu ya zulia na miguu ya mkaaji inatakiwa nyayo zitue kwenye zulia. Kizulia kidogo sana kwenye chumba kikubwa huwa kinaleta ukakasi na kuonekana kama kitu kilisicho mahali pake.

Rangi na michoro
Mwanzoni nimegusia kidogo kuhusu rangi. Kabla hujatoka nyumbani kwenda kununua zulia piga picha ya vyumba unavyotaka kuweka mazulia hayo. Kuna rangi ambazo zinasaidia kupunguza ukali wa rangi nyingine. Kwa mfano, kama chumba kina rangi za mwanga, zulia la rangi nzito/giza litafaa ili kupunguza ule mwanga. Fikiria je unataka rangi na michoro ya zulia iwe ndio kitovu cha chumba?
Rangi na michoro ya giza inasaidia kuficha madoa. Mara zote angalia sampo ya rangi ya zulia unayotegemea kununua kabla hujafanya maamuzi.

Kwa ushauri tuwasiliane 0755 200023

1 comment: