Pages

Tuesday, June 28, 2016

Mifumo ya kuweka mpangilio ili kurahisisha maisha ndani ya nyumba

Mpangilio ndani ya nyumba unagusa vitu na maeneo mengi. Unapokuwa na mifumo ambayo umejiwekea bila shaka itakusaidia kuwa na nyumba nadhifu, safi yenye mpangilio na hivyo kurahisisha maisha. Katika makala hii tunaangalia vitu na maeneo mbalimbali nyumbani yanayohitaji kuwa na mpangilio na jinsi ya kuwa na mfumo wa kukuwezesha kufanikisha azma hiyo.

Karatasi
Mbali na karatasi za bili zinazoingia nyumbani ambazo kwa kawaida ni chache, sijui kama kuna nyumba inayoingia karatasi nyingi kama nyumba yenye watoto wa
shule. Mara unapogundua ni kiasi gani cha karatasi kinaingia nyumbani kila siku ni vyema kuwa na mfumo wa kuziweka kwenye mpangilio badala ya kusambaa kila kona. Kinachotakiwa ni kuweka mfumo wa kutunza karatasi hizo kwa kutumia mafaili. Kila mwanafamilia anayeingiza karatasi nyingi nymbani ni vyema awe na faili lake la boksi na liwe na jina. Kila karatasi inayomhusu inapoingia ihifadhiwe kwenye faili hilo. Zile karatasi za ujumla kama bili na barua nyingine za kawaida kama za toka kwa wajumbe na za namna hiyo hifadhi kwenye faili la peke yake.

Jikoni
Sasa, kama wanavyosema jiko ni moyo wa nyumba, na pia ni mahali pa mwanzo ambapo kweli panaweza kuvurugika mno kama hapana mfumo mzuri wa kuweka mpangilio! Kwenye nyumba nyingi pia jikoni ni njia ya kuingilia vyumba vya ndani na hata kuna wakati wageni wanapita kwenda sebuleni.Uwepo wa vifaa vingi, vyombo na hata dawa na sabuni mbalimbali za kusafishia, makabati na madroo yanaweza kujaa mara moja.

Njia ya kwanza kabisa ya kukuwezesha kuweka mfumo wa mpangilio ni kuondoa kwanza vitu usivyohitaji na tumia kitu chenye manufaa zaidi ya moja. Kwa mfano kama una kipasha chakula (microwave) kinachoweza kuchoma pia, basi huhitaji jiko lenye tanuri (oven). Baada ya hapo jaza kabati na droo kwa vitu unavyohitaji huku ukipanga vile unavyotimia mara kwa mara maeneo ya karibu na vile unayotumia mara chache maeneo ya juu.

Tumia kabati la chini ya sinki kwa kuhifadhia sabuni na dawa za kusafishia na karatasi za chooni za akiba endapo kule hakuna eneo la kuhifadhia.

Chakula
Wakati tukiongelea jiko, chakula pia inapaswa kiwe kwenye mpangilio. Hifadhi vyakula vikavu kwenye stoo ya jikoni ambayo kama ina mashelfu ni vizuri zaidi. Huko unaweza kutumia mchanganyiko wa mifumo ya vikasha, vikapu na vikontena vyenye majina.
Kwenye jokofu ni eneo la pili la kuweka mpangilio wa vyakula baada ya lile la stoo. Pangilia kwa kutumia nafasi vizuri huku ukihusisha vikontena ulivyochagua kwa makini na kuweka vyakula sahihi kwenye maeneo sahihi yaliyoainiswa tayari ndani ya jokofu.

Nguo
Nguo ni kitu kingine kinachoweza kuchukua kila eneo chumbani iwe ni kwenye kiti, kitandani, kabatini au kwenye droo. Baada ya kubakiwa na nguo unazohitaji ainisha zile za kukunja (kunja kwa njia ya wima) na za kutundika. Mpangilio wote huo uendane na aina ya nguo. Kwa mfano eneo la mashati, la magauni, suruali na kadhalika.

Vifaa na nguo za kazi za tope
Tunaishi maeneo mbalimbali ya nchi mijini na vijijini na vilevile majira ya baridi na ya joto. Ni vyema kuwa na eneo la kuhifadhia nguo, kofia na viatu vinavyotumika kwenye shughuli na nyakati hizo.

Midoli na michezo
Kama una watoto wadogo, midoli inaweza kuwa ni moja ya vitu vinavyokupa changamoto kubwa ya kuweka kwenye mpangilio. Michezo na midoli inaweza kusambaa kila mahali hata ikafikia hatua ya kuvunja watu miguu (fikiria unaingiza mguu kwa bahati mbali kwenye gari la toi lenye chuma). Cha kufanya ni kuweka mfumo wa kuhifadhia kama vile vitenga vikubwa kwa vidogo kwenye vyumba vyote vya watoto pamoja na maeneo yao ya kuchezea. Kama unaamua kwenda mbele zaidi unaweza kuwajengea shelfu za wazi ukutani kuwa wakimaliza kucheza wahifadhi michezo yao hapo.

Sasa basi, baada ya kutaja maeneo, vitu na mifumo yake ya kuweka mpangilio ni vyema tufahamu kuwa hakuna mfumo ambao ni sahihi zaidi kwa kila familia au nyumba ila kama lengo lako ni kuwa na mpangilio ndani ya nyumba, natumai orodha hii inaweza kukusaidia pa kuanzia kwa kujua kuwa ni maeneo yapi ya kipaumbele ili kurahisisha maisha hapo nyumbani.

Je kuna maeneo mengine ambayo ungependa kuongezea kwenye orodha hii? Ningependa kuyafahamu.


Simu 0755200023

No comments:

Post a Comment