Pages

Monday, July 11, 2016

Tabia 5 za kukuwezesha kuwa na bafu safi la kisasa

Wengi hatupendi kufanya usafi bafuni, ni kawaida. Awali ya yote napenda tukubaliane kwamba katika makala haya bafu safi la kisasa linamaanisha chumba chenye eneo la kuogea, kupigia mswaki na kujisaidia.

Ni wachache wanaopenda kujipinda kusugua kuta zilizojenga utando wa sabuni au hata kusafisha bakuli la choo. Uzuri ni kwamba kuna tabia unaweza kujizoesha na
zikakuwezesha kulifanya bafu lako kuwa safi kwa muda mrefu na pia kupunguza kazi ya kusafisha inapofikia ule wakati maalum wa kufanya hivyo. Tabia hizo ni kama ifuatavyo:

Piga mswaki ukiwa umeinamisha shingo
Wapo wanaofanya hivyo ila pia wapo wengi tu wanaopiga mswaki wakiwa wamenyoosha shingo zao wakijiangalia kwenye kioo cha juu ya sinki. Unajua ubaya wake? Unasambaza mapovu ya dawa ya meno kwenye kioo na kila mahali kuzunguka sinki. Ukiinamisha kichwa kidogo na kuwa karibu na sinki, mengi ya mapovu haya yanaishia kwenye sinki na kusafirishwa na maji. Hili sio la kupuuzia kwani litakuokolea muda wa kusafisha kioo.

Suuza kuta za eneo la kuogea kila baada ya kuoga
Unaweza ukadhani kuwa inakuchukulia muda kakini si kweli. Kujenga tabia ya kusuuza mapovu ya sabuni na maji machafu kwenye ukuta baada ya kuoga kutafanya bafu lionekane safi kila wakati na zaidi ni kwamba wakati wa siku maalum ya kusafisha kutapunguza kazi na muda wa kusugua. Fikiria utando wa sabuni na uchafu wa mafuta toka mwilini ambavyo havitajiwekea tabaka kwenye kuta za bafu kwa sababu tu umesafisha wakati uleule wa kuoga.

Acha bakuli la choo safi kila ulitumiapo
Kusafisha choo kila baada ya kukitumia kunaondoa uchafu na harufu mbaya bafuni. Kusafisha haimaniishi tu kuflashi lakini pia kusugua endapo kuna uchafu umeng’ang’ania. Mara zote hakikisha brashi na dawa za kusafishia bakuli la choo ziko umbali wa mkono.

Futa mabaki ya vipodozi
Wengi wenye bafu za kisasa wana maeneo ya kuwekea vipodozi na kuweza kuvipaka wawapo bafuni. Badala ya kuacha unga wa poda na vipodozi vingine vikiwa vimewagika kila mahali unaweka ukaloanisha kipande cha karatasi ya chooni na ukafuta hapo mahali.

Kuwa na sakafu kavu
Ukiweza kuweka sakafu ya bafu lako kuwa kavu kila wakati itakuepusha na mengi. Ukavu sio wa maji tu bali hata mikojo ya watoto ama kimiminika kingine chochote sakafuni. Njia nzuri pia ya kuwezesha hili ni kutumia mabafu za kupachika au pazia za bafuni na pia kuwekeza kwenye vizulia vya bafuni ili nyayo zisisambaze maji unapotoka kuoga.

Msomaji wangu bila shaka utaona kuwa mantiki nzima ni kuacha safi kila eneo la bafu pindi unapolitumia.


No comments:

Post a Comment