Pages

Wednesday, August 3, 2016

Jinsi ya kutunza ubao cha mbao cha kukatia

Kwenye majiko yetu wakati wa kuandaa vyakula kwa ajili ya kupika wengi tunatumia ubao wa kukatia. Zipo mbao za kukatia zilizotengenezwa kwa malighafi tofauti tofauti kama vile mbao, plastiki na glasi. Kiafya ubao wa mbao umeonekana ndio unafaa zaidi kuliko hizi nyingine zote kwa sababu hauwezi kupeleka chembechembe yoyote ya plastiki kwenye chakuwa kama ambavyo inaweza kutokea kwa ubao wa plastiki.

Hapa tunaangalia namna ya kusafisha na kutunza ubao huo wa
mbao wa kukatia wakati unapoandaa chakula jikoni.

Osha kwa kusuuza
Tofauti na ule wa plastiki, ubao wa mbao unatakiwa kuoshwa kwa mithili ya kuusuuza tu kwani mbao ni malighafi asili ambayo haihimili kusuguliwa kwa nguvu na maosheo makali.
Maosheo magumu kama misugulio itumie kwenye sinki, sufuria za kushikana na chakula na kwenye vyombo vya plastiki ila kwa ubao wako wa mbao uoshe kwa kutumia sponji laini, sabuni na maji ya uvuguvugu.

Usiloweke ubao wa mbao kwenye maji kwani unaweza kuusababishia kulainika na kuanza kumomonyokamomonyoka.

Matunzo
Kutokana na kwamba mbao ina vimashimo vidogo ambavyo vinapitisha maji na vitu vingine, ni rahisi vijidudu kuweka makao. Ili kuua vijidudu vyovyote kirahisi, changanya kijiko kimoja cha vinega kwenye nusu kikombe cha maji pamoja na limao na sambaza kwenye ubao wako mara baada ya kuusafisha. Ruhusu ukae kwa nusu saa na ndipo unaweza kuuchukua na kuusuuza. Uache ukauke kabisa kabla ya kuutumia tena.
Fanya zoezi hili kila baada ya muda fulani kutokana na matumizi yako hasa kama ubao unakatia kwa wingi vyakula aina ya nyama.

Kama kuna matunda na mbogamboga zimesababisha ubao wako ukatengeneza madoa tumia chumvi na limao kuusafisha. Nyunyuza chumvi juu ya ubao halafu isugue kwa limao ambalo limekatwa nusu. Sugulia upande uliokatwa halafu ukimaliza usuuze na kuuanika.

Kuhakikisha kuwa ubao wako wa kukatia haubaki na harufu za vyakula tumia magadi soda kidogo na yaache juu ya ubao usiku mzima. Kesho yake usuuze na kila kitu kitakuwa sawa.

Upake mafuta
Mbao ina vijishimo, ukiwa unaupaka ubao wako mafuta kabla ya kuutumia kutasaidia kuziba vijishimo hivyo visinyonye juice/majimaji wakati unapoutumia kukatia vyakula.

Tumia visu vikali
Visu vinahusika moja kwa moja kwenye ubao wa kukatia. Kisu kikiwa butu kitakufanya ugandamize kwa nguvu wakati wa kukata, ambapo inaweza kupelekea kuharibu ubao kwa kuutengenezea nyufa.Unaweza kuepuka hii kwa kunoa visu vyako mara kwa mara na kutumia kisu sahihi kwa kazi sahihi.
Ubao wa kukatia wa mbao unawezesha visu vyako vibaki kwenye makali muda mrefu zaidi kuliko mbao za glasi, seramiki au plastiki
Uzuri wa ubao wa mbao wa kukatia haupingiki. Ni rafiki kwa visu vyako, ni salama kwa familia yako na pia ni vyema kuunga mkono vya kwetu kwa kutumia bidhaa hii inayotengenezwa na wajasiriamali wadogo!

No comments:

Post a Comment