Pages

Monday, August 1, 2016

Namna ya kuchagua rangi ya bafuni

 
Bafu ni chumba kidogo ambacho kinaweza kusababisha shida kubwa kama hutachagua rangi kwa umakini. Rangi hiyo inaweza kuwa ni ya marumaru za ukuta na sakafu, ya dari, rangi ya pazia au hata ya sinki la kuogea au ya bafu la kupachika. Ni rahisi kuchagua rangi isiyo sahihi kutokana na mawazo ya kizamani ya kwamba bafuni ni mahali pasipokuwa na sababu ya kupendezeshwa.

Endapo rangi isiyo sahihi itatumiwa bafuni inaweza kusababisha kusiwe na
mvuto na wewe ukaenda mle kwa kujilazimisha tu.

Ili uweze kuchagua rangi sahihi kwa ajili ya bafu lako kwanza inakubidi ufahamu changamoto za chumba chenyewe hata kabla ya kuwa na hiyo rangi unayofikiria. Kama bafu lina dirisha dogo sana au pia hapo dirisha lilipo linapakana na kivuli chochote kiwe ni cha mti au nyumba nyingine, uhafifu wa mwanga wa jua utagusa rangi yoyote unayotaka iwepo bafuni.

Upungufu wa mwanga wa asili inamaanisha kuwa utatakiwa kuchagua rangi ambayo itasaidia kuongeza mwanga bafuni. Wengi tukisikia rangi za kuongeza mwanga tunaenda moja kwa moja kwenye nyeupe. Sio lazima kuwa na bafu jeupe ili kuongeza mwanga endapo ni hafifu, rangi yoyote ambayo sio ya giza au nzito inafaa kuongeza mwanga pale taa zinapokuwa zimewashwa.

Ni kawaida kukutana na marumaru nyingi za bafuni zikiwa na rangi ya bluu, mantiki tu ni kwamba rangi ya bluu ni eneo la maji, na kwenye picha na mionekano mingi maji yanawakilishwa na rangi ya bluu. Sio lazima uamue kuchagua bluu kulingana na imani hii.

Bafu linaweza kuhisiwa baridi au lisilochangamka kutokana na kuzidiwa na rangi zilizopoa, kuanzia rangi za bomba ambazo nyingi ni silva ya kungaa, vioo vya kujitizama na hata vya bafu la kupachika na mng’ao wa marumaru zote hizi zinatakiwa kuwa na uwiano.

Bafu linatakiwa kujenga hisia za joto na burudani kwahivyo rangi kama za krimu, kijani laini, kijivu chepesi ni kati ya ambazo zinaweza kukupa hisia hizo.

Kuwa makini usije ukazidisha rangi. Kama bafu zima litaonekana kung’aa sana unaweza kutamani kutoka mbio pale macho yanapokutana nalo.


Unaweza kutumia rangi nzito kama vile rangi ya chungwa, damu ya mzee au udongo kwa vitu vingine vya bafuni kama mataulo, ndoo ya uchafu, kitenga cha kuhifadhia tishu au pia vesi ya maua.

No comments:

Post a Comment