Pages

Monday, August 22, 2016

Namna ya kupendezesha kona tupu




Kila kona ya chumba iliyo tupu ni fursa yako kubuni namna ya kuipendezesha. Na wakati unaipendezesha unaweza kujikuta unaitumia pia. Mara nyingi kona zimekuwa zikisahaulika au kudharaulika, ukitaka uitumie kona ipasavyo ni pale unapokuwa na nyumba ndogo huku unahitaji kunufaika na kila eneo na pengine una  vitu vingi unavyohitaji kuviweka katika mpangilio ili nyumba yako iwe na
muonekano wa  kuvutia.  Endelea kusoma makala hii ufahamu njia za kuifanya kona iliyo tupu ipendeze na kutumika kwa manufaa zaidi.

·         Weka shelfu za vitabu ambazo zimetengenezwa kwa muundo wa kufuatisha kona ilivyo. Hii ni moja ya njia nzuri za kufanya kona isiyokuwa na kitu iweze kutumika na shelfu zinaweza kwenda hadi juu kabisa karibia na dari hata kama utapanda juu ya kitu wakati wa kuchukua kitabu kilicho shelfu la juu zaidi.
·         Mbali na shelfu za vitabu unaweza pia kuweka shelfu kwa ajili ya kuonyesha mapambo mengine madogodogo na hata mimea midogo ya urembo.

·         Tundika bembea la kumpembelezea mtoto. Unajua jinsi nyumba yenye mtoto wa kubebwa inavyokuwa na msongamano wa viti vya kubembea sakafuni. Unaweza kuondokana na msongamano huo kwa kununua bembea na kulitundika kwenye kona. Licha ya bembea husika kuwa la mtoto hata wewe mtu mzima unaweza kubembea  pale anapohitaji kujiburudisha kidogo.

·         Fanya kona iwe kituo cha kufanyia kazi zako za kiofisi kwa kupatengenezea dawati na kiti. Hakuna eneo zuri la kufanyia kazi kwa kutuliza akili kama ambalo macho hayakutani na usumbufu. Kwa mkao huu wa kwenye kona ni kwamba macho yako yanatazama moja kwa moja kwenye kazi yako au ukivuta pumzi unayaelekeza ukutani.  Vilevile ni njia ya kufanya kona iwe kituo cha kuwekea vitu vya kukuwezesha kuwa na mpangilio. Kwa mfano sehemu ya kuwekea nyaraka, kalamu au kuchajia vifaa vya elektoniki,  huku eneo la juu ukiweka mbao za kutobolea karatasi za ujumbe mbalimbali kama vile  ratiba za mapishi na usafi wa nyumba.

·         Ifanye kona iwe eneo la kutundika picha za familia. Huhitaji ukuta mkubwa kwa ajili ya kusambaza picha za familia yako badala yake tumia kona kuongeza mvuto.

·         Weka mmea mkubwa unaofaa kuoteshwa ndani hapo kwenye kona kama hutataka kuweka shelfu au sanaa zozote. Hii itasaidia kuingiza uoto asili ndani ya nyumba huku matawi yake yakitumika kuijaza kona yenyewe.

·         Tumia kona kutengeneza eneo la kutundikia nguo, hasa kwenye chumba cha kunyooshea au cha wageni kwani mara nyingi vyumba hivi ni vidogo kwahivyo pachika fimbo itakayokutanisha pande mbili za kuta za kona kwa ajili ya kutundikia nguo, kutumia kona kwa shughuli hii ni matumizi mazuri ya chumba husika.

·         Tumia kona kutengeneza eneo la kuhifadhia michezo ya watoto


·         Weka sofa la duara au lenye vipande viwili ambavyo vitaunganikia kwenye kona.

·         Weka meza ya duara. Meza ya duara inakaa watu wengi kuliko ile ya pembenne. Inapokuwa karibu na kona eneo linafiti vizuri kuweka kiti cha kukalia, na kikiwa ni cha mgongo mrefu kona inapendeza zaidi.

·         Pendezesha kona kwa kuweka vinyago vikubwa.


·         Patengenezee kabati au kimeza cha kona chenye miguu mitatu. Bila shaka utakapomtafuta fundi mzuri ana uwezo wa kuchukua vipimo vya kona yako na kukutengezea fenicha ya kufiti hapo vizuri kabisa. Na pia sia ajabu kwenye maduka ya fenicha kukutana na kimeza au kabati la aina hii  ambalo litatosha kwenye kona. Kuna sababu ya kwanini hizi fenicha za hivyo zinatengenezwa.

Kwa dondoo za kupendezesha nyumba nifuate instagram @vivimachange

No comments:

Post a Comment