Pages

Wednesday, August 17, 2016

Namna ya kupendezesha ndani kwa vyungu vya maua

Kuna namna nyingi za kuongeza mvuto ndani ya nyumba zetu na tunapotaka kufanya hivyo kwa kuweka  maua ya ndani, mara nyingi tunaenda moja kwa moja kwenye vesi za maua za meza ya kahawa au ya chakula. Ila vyungu vikubwa vya maua vya kuweka sakafuni ni njia ya ajabu ya kuchangamsha kona iliyozubaa au kusahaulika na kuigeuza mara moja kuwa kivutio namba moja cha jicho ndani ya chumba. Kutokana na
kuwa na vyungu vya aina, mitindo na ukubwa tofauti tofauti kuna uwezekano wa kupamba tofauti katika sehemu tofauti za ndani.

Vyungu vikubwa vya sakafuni vya maua vinawezekana kuwekwa kwenye chumba chochote na vikaendana na mandhari nyingine iliyopo ndani vilevile.
Unaweza kukifanya chungu kukaa kama kazi ya sanaa tu, kwa maana ya kwamba sio lazima uweke maua ndani ili kupendezesha, badala yake chenyewe unakigeuza ndio pambo na kinapendeza kabisa. Kwahivyo yote kwa yote inategemea lengo lako la kuweka hicho chungu kwenye chumba husika.

Vyungu vikubwa vya maua vya sakafuni vinapendezesha maeneo mbalimbali ya sebule, chumba cha kulia chakula, eneo la ngazi na hata eneo la kuingilia. Vipo vyungu ambavyo ni vya kutunza kwa uangalifu kama vile kioo na vipo vigumu, vipo vya rangi, maumbo na ukubwa mbalimbali kadri ya uwezo wako wa unachotaka. Hakuna kikomo na hii inavifanya kufiti kwenye nyumba yoyote, kama sehemu unayotaka kukiweka kuna uwazi mkubwa basi unaweka kile kikubwa kabisa. Haijalishi sehemu ikoje lazima kuna chungu ambacho kitapafaa.

Unaweza kutumia vyungu viwili vikubwa vya sakafuni kama njia ya kuonyesha mgawanyo wa chumba ikiwa ni pamoja na kuviweka jirani na taa za vivuli za kusimamisha sakafuni.

Unaweza ukachangamsha rangi ya chumba kwa kuongeza chungu cha maua cha sakafuni chenye rangi ya tofauti. Hivi ndio vile vitu ambavyo vinatengeneza mvuto. Kwa wale ambao hawapendi rangi kali wanaweza kuweka vyungu vyenye rangi zilizopoa zinazooana na za kuta. Ukiweka maua marefu kwenye chungu yanakifanya nacho kionekane ni kirefu.

Kuweka vyungu vya maua vya sakafuni eneo ambalo ni karibu na mchoro wa ukutani unaoendana nacho inaleta muonekano wa kuvutia. Ni uwezo wako tu wa kufikiri ili kutengeneza uwiano. Vyungu vinafaa kwa aina yoyote ya upambaji ambapo wale wanaopamba kwa mtindo wa kisasa wanatumia vyungu vyenye kuta laini na rangi kali kama vile chungwa, kijani na nyekundu wakati wale wanaopamba kiutamaduni wanaweza kuchagua vile ambavyo vina kuta na muonekano wa rafu huku rangi zake zikiwa ni zile zilizopoa.

Vyungu vikubwa vya maua vinakupa pia uwezo wa kuwa na muonekano wa rangi za asili ndani ya nyumba yako. Rangi hizo ni pamoja na rangi ya mimea ambapo mingi ni ya kijani na pia rangi ya udongo. Kama tujuavyo si kawaida kupaka kuta zote za ndani ya nyumba rangi ya kijani au ya udongo. Badala yake unaweza kutumia vyungu vya rangi hizo ili kuleta muonekano wa rangi za asili ndani ya nyumba pale unapohitajika kufanya hivyo. Pia weka miti ya bamboo ndani ya vyungu vyako katika nia ileile ya kuongeza uasili.


Vyungu vikubwa vya maua vinapowekwa sakafuni katika hali ya ubunifu, vinasaida kujaza sehemu zilizo na uwazi mkubwa. Uzuri wa vyungu hivi ni kwamba una uwezo wa kuvihamisha toka sehemu moja hadi nyingine ili kubadili muonekano wa chumba kirahisi kabisa.

No comments:

Post a Comment