Pages

Monday, August 29, 2016

Staili za ubao wa kichwani mwa kitanda




Ubao wa kichwani ni kile kipande cha fenicha ambacho kiko kichwani mwa kitanda. Unapotaka kuwa na kitanda cha kuvutia, ubao wa kichwani ndio sehemu pekee kwenye fremu ya kitanda panapokupa nafasi ya kufanya hivyo. Ingawa sio kila kitanda kina ubao huu ila kilicho nao sio siri kwamba kinavutia kuliko kisicho nao. Makala hii itakujuza aina mbalimbali za mbao za kichwani na jinsi ya kuchagua ambao utaongeza mvuto wa chumba cha kulala.

Zaidi ya kufanya kitanda kivutie, ubao wa kichwani unakiongezea thamani. Pia ubao huo unaweza  kutumika kuendana na mtindo na
muundo wake ulivyo. Kwa mfano, watu wanaotaka kukaa wakiwa kitandani, ubao wa kichwani unasapoti mgongo nyuma ya mito. Na pia zipo mbao za kichwani ambazo zimetengenezwa kwa mitindo mbalimbali kama vile kuwekewa shelfu za vitabu na vitu vya mapambo au hata eneo juu ambalo unaweza kuwekea kikombe na miwani ya kusomea. Mbao ndefu za kichwani zinaweza kupigiliwa kulabu za kutundikia nguo za kulalia au taulo. Nyingine zimewekewa taa kwa ajili ya kusomea unapokuwa kitandani.

Mbao za kichwani zinatofautiana kuendana na malighafi na umbo. Ni vyema ukafahamu za mitindo na miundo mbalimbali ili wakati unapotaka kutengenezewa au kununua kitanda uchague chenye ubao ulio sahihi kwako. Pia ni vyema ujue kuwa ubao unaweza kuwa umejishika moja kwa moja kwenye kitanda au umejitenga ambapo unakuwa umesimama toka sakafuni au umepachikwa ukutani eneo kilipo kitanda.

Mbao za kichwani zilizotengenezwa kwa malighafi ya mbao ndio za kisasa zaidi, zina namna nyingi ya kupendezeshwa na zinaweza kupakwa rangi tofauti tofauti.  Ubao wa namna hii unaweza kuongezewa sponji na kitambaa na hata kuwekewa vishimo vidogo vingi ambavyo tunasema ni vifungo yote hiyo ikiwa ni kuufanya uvutie. Vivyohivyo ubao wenye michoro unafanya kitanda kivutie zaidi pale kinapotandikwa kwa kuoanisha matandiko yenye rangi na michoro hiyo.

Kuna maumbo mengi ya mbao za kichwani kwahivyo haijalishi kuwa kwa vile kitanda ni cha pembe nne basi na ubao utatakiwa uwe ni wa pembe nne. Kitanda kinaweza kuwekewa ubao wa umbo lolote liwe ni pembe tatu, duara au pembe sita. Na hata upana wake unaweza kuzidi ule wa kitanda. Ila inashauriwa ni vyema ukubwa wa ubao wa kichwani uendane na ukubwa wa chumba, vinginevyo unaweza kuonekana kukizidi nguvu pale utakapokuwa mkubwa sana huku chumba kikiwa kidogo.

Bila shaka unaweza kupata ubao wa kichwani wa mtindo na muundo unaotaka kutoka kwa mafundi vitanda waliobobea. Uzuri mmoja wa kutengenezesha kitanda ni kwamba una wigo mpana wa kubuni, kuchagua na kuonyesha ubao wa kichwani unaotaka utengenezewe kwenye kitanda chako.

Nifuate instagram @vivimachange

No comments:

Post a Comment