Pages

Tuesday, August 9, 2016

Utunzaji wa sakafu ya mbao

Zamani kabla ya gharama ya mbao kuwa kubwa zaidi na pia kabla ya ujio wa marumaru watu wachache waliokuwa na uwezo wa kujenga nyumba bora waliweka sakafu ya mbao. Lakini pia kwa siku za karibuni nimeshuhudia wasomaji wangu baadhi wakitaka kufahamu kuhusu sakafu ya mbao. Ni kama vile imeanza kupata mvuto tena hasa kwenye sebule za nyumba za kisasa.

Nimeongea na
Patrick Joseph ambaye ni fundi wa sakafu za mbao na anatujuza namna ya kutunza sakafu hii ambapo ni swali namba moja linalowasumbua wengi wanaotamani kuwa na nyumba yenye sakafu ya aina hii. Fundi anaanza kwa kusema kuwa sakafu ya mbao ni ngumu, imara na ya kiwango ambayo inaweza kudumu miongo mingi kama itatunzwa ipasavyo. Hata hivyo ukosefu wa matunzo na usafi  unaweza kusababisha sakafu hii kuharibika mapema hasa kwa kutengeneza madoa, mikwaruzo na kupoteza mvuto. Zifuatazo  ni dondoo za kuzingatia ili kutunza sakafu ya mbao iwe unayo tayari au ndio unafikiria kuwa nayo.

Mazingira: Mbao ni malighafi ya asili ambayo inaonyesha tofauti pale inapokutana na joto kali sana na unyevunyevu mwingi kwa pamoja. Hali hizo mbili zinapopita kiwango inaweza kusababisha mbao kupasukapasuka na kuoza.
Vilevile mwanga wa moja kwa moja wa jua kutokea dirishani au kwenye mlango wa kioo unaweza kusababisha sakafu ya mbao kupauka na kuchuja rangi. Epuka hali hii kwa kuhakikisha kuwa wakati jua linalopiga moja kwa moja kwenye sakafu ya mbao pazia ziwe zimefungwa.

Uchafu: Mara kwa mara ni muhimu kufagia sakafu ya mbao kwa kutumia ufagio laini, ili kuondoa chembechembe zote za uchafu ambazo zinaweza kuikwaruza. Matumizi ya matandiko ya milangoni kwenye mlango wa nje na ya kuingia kila chumba yatasaidia kupunguza kiasi cha chembechembe za uchafu ambazo zinaweza kutua kwenye sakafu ya mbao. Vizulia vya kutupia navyo vinaweza kutumika kwenye yale maeneo yanayopitiwa sana kama vile kwenye korido. Epuka kutumia maji mengi au mara kwa mara kusafisha sakafu ya mbao. Safisha kwa kutumia bidhaa zilizoidhiniswa kwa ajili ya mbao.
Vitamu tamu kama bazoka navyo ni vya kuepuka kutafunwa ndani endapo una sakafu ya mbao.

Wanyama wa ndani: Baadhi ya watu wanapenda kufuga wanyama kama vile mbwa, paka, sungura na kadhalika ndani ya nyumba zao. Paka au mbwa wa ndani anapokuwa na kucha zenye ncha kali ni rahisi kusababisha mikwaruzo kwenye sakafu ya mbao. Kama kweli ni furaha yako kufuga wanyama hawa ndani, basi uwe unawakata kucha zao ili kuepuka hali hiyo.

Viatu: Viatu vya mchuchumio vyenye visigino visivyofunikwa na plastiki vina uwezekano wa kukwaruza na kuharibu sakafu za mbao. Vivyohivyo kwa viatu vilivyobeba mchanga. Unaweza kuhitajika kuweka kanuni ya kuvua viatu mlangoni kabla ya kuingia ndani.


Fenicha: Fenicha nzito zenye miguu iliyochongoka zinaweza kusababisha uharibifu mkubwa pale zinapoburuzwa kwenye sakafu ya mbao. Fenicha zinatakiwa kubebwa wakati wa kuzihamisha na pia miguu yake kuwekewa kizuizi laini chini ili isigusane moja kwa moja na sakafu.

No comments:

Post a Comment