Pages

Saturday, September 3, 2016

Faida za kuwa na vimeza vidogo vya pembeni




Vimeza vya pembeni ni vimeza vidogo vya kando ambavyo vina msaada mkubwa  na tofauti tofauti katika chumba chochote. Kama hukuwa navyo, utakavyokuwa navyo utashangaa ni kwa namna gani uliweza kuishi bila kuwa navyo.

Vipo vilivyotengenezwa kwa malighafi mbalimbali lakini kama unahitaji vimeza vya kando imara ambavyo vinaweza kudumu miaka mingi basi chaguo namba moja ni
vilivyotengenezwa kwa mbao ngumu. Mbali na kuwa imara vimeza vya pembeni vya mbao vina mvuto na ni rahisi kuvitunza miaka nenda rudi. Pia zaidi ya kutumika, vimeza hivi ni kwa ajili ya kupendezesha pale vilipo.

Kama sehemu ya fenicha za kwenye sebule yako, vimeza vya pembeni vina faida zaidi pale vinapokuwa mwishoni mwa sofa au baada ya kiti, pale ambapo unaweza kukaa na kuwekea juu yake kinywaji, kitabu au jarida kuwa karibu na wewe na kukuondolea usumbufu wa kunyanyuka mara kwa mara. Vilevile kwa upande wa sebuleni unaweza kutumia kimeza cha kando kwa ajili ya kuwekea taa za vivuli kuipa sebule mvuto au vilevile kutumia kimeza cha kando kuwekea mapambo na albam za picha za kumbukumbu za familia.

Kwenye chumba cha kulala wengi wanapendelea kuweka vimeza vya pembeni mwa kitanda ambavyo vina muonekano sawa na wa kitanda. Vimeza hivi ni murua kwa kuwekea taa za mezani za pembeni mwa kitanda ambazo zinatumika wakati umejinyoosha huku ukijisomea kitabu chako ukipendacho kabla hujashikwa na usingizi. Au pia unaweza kukitumia kuwekea glasi ya maji, kitabu, simu au kifaa kingine chochote. Baada ya kuperuzi mitandaoni ukiwa kitandani, utahitaji sehemu ya kuweka laptop yako. Kimeza cha pembeni ndio suluhisho namba moja. Unaweza kuwekea laptop bila kukuhitaji kunyanyuka toka kitandani.

Watu wengi wanatumia saa zenye kengele ziwaamshe muda wa kujiandaa kwenda kazini. Sehemu sahihi ya kuweka saa yako au simu yenye kengele ya kukuamsha ni juu ya kimeza cha kando kilicho karibu yako. Picha ya kwenye fremu na maua ni vitu ambavyo pia vinaweza kuwekwa juu ya kimeza cha pembeni mwa kitanda.

Zaidi ya kuwa inawezekana una seti  ya fenicha iliyokamilika katika chumba cha chakula, kuongeza kimeza cha kando inaweza kukupa msaada mkubwa. Ni sehemu sahihi ya kuweka chupa zilizo wazi zinazoendelea kutumika wakati wa chakula, au pia kuweka bakuli la matunda na hata maua au pambo uliloondoa mezani lipishe wakati wa kula.
Kwenye chumba cha chakula, kimeza cha kando chenye droo kinaweza kuwa msaada mkubwa wa kuhifadhia vitambaa vya meza, visu, vijiko na uma.


Licha ya kuwekwa vyumbani, kimeza cha kando chenye droo kwenye korido ni suluhisho kwa kuhifadhia bila kusahau kupendezesha. Hakika vimeza vya kando vina faida nyingi kwenye kila chumba

No comments:

Post a Comment