Pages

Sunday, September 25, 2016

Jinsi ya kuchagua rangi ya kupaka dari

Dari naweza kuliita ni ukuta wa tano wa chumba lakini, mara nyingi haipati rangi nyingine zaidi ya nyeupe. Kwa muda mrefu toka nyumba za kisasa ziwepo, nyeupe imechukuliwa sio tu kama rangi salama bali pia sahihi kwa ajili ya dari. Kuna wakati kweli nyeupe inaweza kuwa ndio chaguo muhimu na pekee, lakini kama hujawahi kufikiria rangi nyingine mbali na
nyeupe huenda ukawa unapoteza wigo mpana wa kupendezesha na kuongeza manjonjo ya chumba.

Ifuatayo ni mikakati na njia zitakazokuwezesha jinsi ya kuchagua rangi ya dari.

Tukianza na mkakati wa rangi nyeupe ambao ni kawaida kwenye dari nyingi kwani wengi wanaamini kuwa ina faida kwamba hutakuwa na haja ya kuibadili mara kwa mara.  Kwamba wanaweza kubadili rangi ukutani lakini dari ikabakia na nyeupe yake ile ile. Rangi nyeupe darini inakifanye chumba king’ae na pia hisia ya kuwa kuta ni ndefu.

Mara nyingi rangi nyeupe ndio chaguo sahihi la dari kwani inafanya hamu ya kutazama juu isiwepo na kuelekeza mvuto kwenye kuta, fenicha na samani.
Kwenye vyumba ambavyo vinapokea mwanga wa jua kidogo, dari nyeupe inasaidia kuupokea na kuusambaza maeneo mengine ya chumba.

Namna nyingine ya kuchagua rangi ya dari ni kuipaka rangi sawa na ya kuta. Njia hii inakifanya chumba kiwe na hisia ya kuwa na utajiri wa rangi na pia ukamilifu.

Vilevile unaweza kupaka dari rangi ambayo inapishana kidogo na ya kuta. Ni namna ambayo rangi za kuta na dari zinakuwa za jamii moja lakini rangi ya kimojawapo ikawa inaelekea kwenye upande wa nzito zaidi au nyepesi zaidi. Nyepesi ya bluu na njano ya siagi ni rangi zinazopendeza darini. Bluu inakupa hisia ya anga.                                    
Namna hii ya kuchagua rangi ya kupaka dari inakupa pia ile hisia kwamba bado uko chumba kilekile.


Namna nyingine ya kuchagua rangi ya dari ni kwa kupaka rangi nzito kwenye dari kuliko ya kwenye kuta na rangi hizi mbili ziwe ni kutoka jamii tofauti kabisa. Mpishano wa rangi hizi mbili una kawaida ya kutengeneza muonekano wa kuvutia. Ni vyema kufahamu kuwa rangi nzito darini inatengeneza hisia ya kwamba kuta ni fupi na pia hisia ya mahaba zaidi. Kwahivyo ni sahihi kwa chumba chenye kuta ndefu hasa kikiwa ni kile cha kulala au cha bafuni. Na kumbuka kuwa endapo kuta zote za bafu zimefunikwa kwa marumaru, darini ndio mahala pekee pa kujidai kwa kupaka rangi. Kuwa makini usijepata rangi nzito darini kama kuta za chumba ni fupi kwani na itatengeneza hisia kwamba chumba hicho kinataka kukufukia!

No comments:

Post a Comment