Pages

Thursday, October 27, 2016

Zingatia mambo haya matatu unaponunua kioo cha kupendezesha


Huenda  uko kwenye mchakato wa kupendezesha nyumba mpya au unaboresha ya zamani, kioo ni pambo muhimu unalohitaji angalau kwenye kila chumba. Ukisema kioo tu inaonekana kama ni kitu rahisi, madukani vipo vingi vidogo, vikubwa na vya maumbo mbalimbali. Hata hivyo ikifika wakati unapotaka kununua, kupata kilicho sahihi kwa chumba fulani pasipo changamoto, zingatia mambo haya matatu.

1. Urefu wa ukuta – Kabla ya
kununua kioo, unatakiwa upime urefu na upana wa ukuta unapotaka kukiweka. Hii inakusaidia kufahamu kabla ukubwa wa kioo unachohitaji ungali bado hujafika kwa muuzaji. Kuta ndogo zinapendeza zikiwekwa kioo kidogo (au kutowekwa kabisa kuendana na udogo wa ukuta) ili pasionekane kuwa na mrundikano. Kioo kikubwa kwenye ukuta mrefu na mpana kinatengeneza muonekano wa kuvutia.

Kwa nyongeza, fikiria ni picha gani unayotaka kuutengenezea huo ukuta unaotaka kuweka kioo. Je ni ukuta wa bafuni ambao kwa asili ni lazima uwe na kioo kwa ajili ya kutumika na sio nia hasa ya kupendezesha, au unataka kioo unachotaka kuweka kiwe ni alama ya pambo na kupendezesha ukuta husika? Kama ni kioo cha kutumika, je kinahitajika kutumiwa kwa shughuli ipi? Ndio tunajua kuwa kazi namba moja ya kioo ni kujitizama, ila je unajitizama uso tuu wakati wa kunawa kwenye sinki au ni kwa ajili ya kujitazama utosini hadi unyayoni ili uweze kujiona muonekano mzima?

2. Eneo – Ni ukuta upi ambao unataka kuweka kioo? Kama ni kwa ajili ya chumba cha wageni, kioo kinakua kama pambo kuliko matumizi. Kwa maana hiyo weka chenye mvuto na hasa kikiwa cha umbo la duara au yai kinapendeza zaidi.
Tofauti na chumba cha kulala cha wageni, kioo bafuni ni kwa matumizi zaidi. Kwa eneo hili unapaswa kuweka chenye umbo la pembenne na ukubwa wa kutosha kwa ajili ya mtu kujiona vizuri wakati wa kufanya shughuli zake za kila asubuhi kujiandaa kuvaa, kuchana na kubana nywele vizuri. Chanzo cha kutosha cha mwanga kwa kioo kilichowekwa kwa ajili ya matumizi haya ni muhimu.

 3. Staili ya chumba – Dondoo ya mwisho ya kuzingatia kwa wote mnaotaka kuweka vioo vya kupendezesha ni staili ya chumba unachotaka kukiweka (au ya nyumba nzima kama mandhari ni ya kufanana kila mahali). Je, mapambo ya ndani ya nyumba yako ni ya aina gani, kwa mfano pengine fenicha nyingi ni za chuma, itakua vyema ukiweka kioo chenye fremu ya chuma, vivyo hivyo kwa mbao. Kioo kioane na muonekano wa finishing za fenicha zilizopo.
Nyumba iliyopambwa kwa staili ya kiutamaduni ikiwa na sanaa ndogo nyingi, kioo nacho kinapendeza kikiwa na fremu iliyotengenezwa kwa nuundo wa kiutamaduni.


Ukizingatia mambo haya matatu, unakuwa na uhakika wa kuwa na kioo sahihi kwenye kila chumba kwenye nyumba yako!

No comments:

Post a Comment