Pages

Wednesday, November 2, 2016

Namna ya kuepuka harufu kwenye jokofu

Kutokea sehemu moja au mbili ndani ya jiko, hakuna sehemu inayokusanya harufu kirahisi kama jokofu. Kuepusha harufu kwenye jokofu sio ngumu kivile ikiwa unajua unachofanya, kwa kutumia njia sahihi. Endapo jokofu lako litakuwa linatoa harufu mbaya tumia njia mojawapo kati ya hizi na
hakika tatizo litakwisha.

Tafuta chanzo cha harufu
Wakati mwingine ni rahisi kusahau ni nini kilichopo kwenye jokofu na kimekuwa huko kwa muda gani hadi pale unapofungua mlango siku moja na kukutana na harufu ambayo hujaipenda. Vyakula vinapokaa muda mrefu vina tabia ya kutoa harufu, na vinaweza kujaza jokofu lako harufu mbaya ajabu. Na hata inapotokea umeondoa vyakula hivyo, jokofu linaweza kuendelea kutoa harufu kwa wiki kadhaa.

Mara zote inasemwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba, na ni vivyo hivyo kwa harufu za kwenye jokofu. Hakikisha vyakula vyote vilivyohifadhiwa ndani yake havijapita muda wa kutumika. Hii ni kazi ambayo unatakiwa kuifanya angalau kila mara moja kwa wiki kupitia kwenye jokofu na kuondoa kila ambacho una wasiwasi nacho au kimepita muda wake.

Hata kama jokofu litafanyiwa usafi wa uhakika, harufu ndani itaendelea kuwepo hadi pale utakapoondoa chanzo chake. Chakula chenye hali yoyote isiyo ya kawaida au kuota kwa ukungu (hasa kwenye mikate) ni wakati wa kuvitupa.

Angalia shelfu la kuwekea mbogamboga kama kuna matunda yaliyooza au mboga zilizoharibika. Kama hakukuwa na umeme kwa zaidi ya masaa 24 huenda ukatakiwa kutupa vyakula kama nyama, samaki na maziwa  kwani vinaharibika ndani ya masaa machache.

Safisha kwa kina
Kama umeshaondoa vyakula vyote vilivyoharibika na kupita muda wake lakini bado kuna harufu; ni wakati wa usafi wa kina. Ondoa vyakula vyote kwenye jokofu ili kusafisha kila mahali kwakuwa huenda vyakula vilivyokuwa vinatoa harufu vilichuruzikia ndani hadi kwenye kingo za shelfu. Weka vyakula hivyo sehemu ya baridi hata kama ni kwenye jokofu lingine. Ondoa shelfu zote na zisafishe kwa maji moto na sabuni. Fanya hivyo pia kwenye kuta, dari na sakafu ya jokofu. Safisha mlango kwa ndani. Kausha na taulo halafu rudishia mashelfu na hatimaye vyakula.

Harufu iking’ang’ania
Kama bado kuna harufu, inaweza kukubidi uondoe vyakula vyote, lizime na kuliacha mlango wazi kwa siku kadhaa hadi harufu itoweke.

Njia nyingine zilizothibitika kuweza kuondoa (kuepuka) harufu kwenye jokofu ni kwa kutumia hamira au mkaa. Fungua pakiti ya hamira uiweke ndani ya jokofu na iache wazi. Inanyonya harufu zote na kuliacha likiwa na hewa safi. Inakupasa kubadilisha pakiti ya hamira kila mwezi kwa ajili inaishiwa nguvu ya uendelea kunyonya baada ya kipindi hicho.

Mkaa unaondoa harufu kwenye jokofu kwa kudumbukiza kipande ndani ya kikombe chenye maji halafu unakiweka ndani ya jokofu.
Pia kuwa kuna deodoranti zinauzwa madukani kwa ajili ya kuweka kwenye majokofu.

Usipochukua hatua mapema, inawezekana usiweze kuondoa harufu mbaya kwenye jokofu. Ina maana utakuwa na machaguo mawili ambayo ni ama kuishi na hiyo harufu kwa kuivumilia au kununua jokofu lingine.

Hata hivyo baada ya kutumia njia zote hizi kama hamna mafanikio ya harufu kutoweka na kama jokofu ni mpya na liko kwenye waranti, wasiliana na wauzaji pengine tatizo ni la kiwandani.


nifollow instagram @vivimachange

No comments:

Post a Comment