Pages

Monday, November 7, 2016

Tofauti ya kutumia stika badala ya wallpaper ukutani

Nimekuwa nikiulizwa hili swali mara kwa mara na wasomaji wangu kuwa ni kwanini mwenye kupendezesha nyumba yake aamue kutumia stika ukutani badala ya wallpaper. Na leo nitalijibu kama ifuatavyo. Stika na wallpaper zote zinapendezesha kuta na zinakidhi malengo fulani kwenye kuta za nyumbani kwako.

Hapa ni
dongoo muhimu za kuzingatia kati ya tofauti ya kupamba kwa stika badala ya wallpaper wakati unapoamua kupendezesha kuta.

Lengo: Wallpaper kama jina lake lilivyo kwamba ni karatasi za ukutani zinabandikwa kufunika ukuta wote wa eneo unalobandika, wakati ambapo stika inafunika pale ilipobandikwa tu na sehemu nyingine yote ya ukuta iliyobaki inakuwa wazi. Tofauti na wallpaper, stika zina tabia ya kuupa ukuta hisia ya sanaa  na ni nyembamba sana kiasi kwamba zinashikana na ukuta kabisa. Bila kuchunguza kwa umakini na kugusa unaweza kudhani ni mchoro uliochorwa moja kwa moja ukutani. Kwahivyo kama unataka kugusa maeneo fulani tu ya ukuta na sio ukuta mzima basi stika ndio chaguo sahihi. Ila wakati huohuo kama unataka kufunika ukuta wote basi chaguo sahihi litakalokidhi lengo lako hilo ni wallpaper.

Ukubwa: Stika ni ndogo ndogo na ziko kwenye mfumo wa ua moja moja ambalo limekamilika. Zinapendeza zikibandikwa pembeni mwa luninga ambapo sehemu kubwa ya ukuta imefunikwa na kabati au shelfu kiasi kwamba sehemu hiyo haionekani wazi kwa hivyo hakuna haja ya kubandika chochote kwani hakitaonekana hata hivyo. Kwa upande wa wallpaper kama nilivyosema ni kwamba inakupasa kuibandika ukuta mzima hata zile sehemua ambazo zitafunikwa kwa fenicha nyingine.

Gharama: Kwa kuwa stika ni kwa ajili ya sehemu fulani ndogo tu ya ukuta ni wazi kwamba gharama yake ni nafuu kuliko ya wallpaper. Pia stika zina wigo mpana wa rangi na maua ya kuchagua na hazikupi changamoto kubwa ya kuoanisha na mapamba mengine ya chumba. Ni rahisi kwa stika kujenga timu na saa ya ukutani, fremu ya picha na sanaa nyingine. Kwahivyo kuleta muonekano wa mandhari nzuri ya ukuta na urahisi kwa kukontroli unachoongeza au kuondoa ukutani basi bandika stika badala ya wallpaper.


Ubandikaji: Hata kama hujui ukielekezwa mara moja tu ni rahisi kubandika mwenyewe stika uliyonunua. Iwe unaibandika sebuleni au kwenye chumba cha watoto. Kwa upande wa wallpaper sio rahisi uweze kubandika mwenyewe kama hujawahi kujaribu mara kadhaa. Kwani kuna matumizi ya vipimo, gundi na ulinganishaji maungio ambao unahitaji utaalam na uzoefu. Pia endapo unataka kubadili muonekano baadaye ni rahisi kufanya hivyo kwa ukuta uliobandikwa stika zaidi ya ule uliobandikwa wallpaper. Uondoaji na maandalizi ya ukuta kwa upande wa wallpaper unahitaji muda.

Nifuate instagram @vivimachange

No comments:

Post a Comment