Pages

Thursday, December 1, 2016

Namna ya kudumisha usafi unapokuwa na wageni wa kulala

Msimu wa sikukuu unakaribia na wapo wanaopenda kuwa na wageni wa kulala nyumbani kipindi hicho. Ila hawapendi kupoteza mpangilio na usafi wa nyumba kutokana na ugeni.

Tuangalie unachotakiwa kufanya ili kudumisha usafi na mpangilio kwenye maeneo ambayo wageni wa kulala wanaingia wawapo nyumbani kwako. Maeneo hayo ni
nje ya nyumba, varanda, sebuleni, chumba chao cha kulala, bafuni na jikoni.

Nje ya nyumba na varanda
Ili kuepuka uchafu kuingizwa ndani kupitia viatu, hakikisha maeneo ya nje ya nyumba ni safi.
Weka tandiko la mlangoni eneo la varanda kwa nje na ndani ili wageni waweze kufuta viatu kupitia tandiko la nje na nyayo kupitia la ndani.

Weka kitundikio cha makoti, skafu na kanga varandani ili wageni wanapoingia ndani waweze kutundika nguo hizi endapo zitakuwa zimebeba uchafu wowote toka nje walikokua. Baadaye aidha zitavaliwa tena au kufuliwa.

Kwenye chumba cha kulala wageni
Fanya utandikaji uwe rahisi kwa kuweka duveti (linasaidia kupendezesha, kutandika haraka na kwa urahisi) na mito michache angalau miwili tu. Kuweka mito nane ni kujiongezea kazi kwako au kwa wageni.

Ondoa mrundikano kwenye maeneo yote ya chumba hiki ili wageni waweze kutumia meza iwe ni ile ya kuvalia au nyingine kwa ajili ya kuwekea vitu vyao. Chumba kisichokuwa na mrundikano  ni rahisi kusafisha. Kama inawezekana chumba kiwe na kabati la nguo au stendi pamoja na vitundikio vya nguo.

Chumba kiwe na kindoo cha taka na tenga la kuwekea nguo chafu.

Kwenye bafu la wageni
Mara moja kila siku nguo chafu ziondolewe zikafunliwe.
Matumizi ya sabuni ya maji badala ya ya kipande ni mazuri zaidi kwa bafu la wageni kiafya na pia haichafui kama ya kipande.

Wote tunajua ambavyo hatupendi tunapofua kukutana na taulo lililofutiwa vipodozi. Suluhisho la tatizo hili kwenye bafu la wageni ni kuweka kitambaa au tishu ambazo zitafanya kazi hiyo na ukatoa maelezo kwa wageni wako kuhusu kitambaa hiki. Unaweza kukitupa mara wageni wakiondoka.
Lazima kuwa na vihifadhio vya taulo ili kuepuka kuzikuta chini hapo baadaye.

Sebuleni
Toa maelekezo ya namna ya kuwasha vyombo vya burudani na matumizi ya rimoti. Hii itakuepusha kuja kuviseti upya endapo vitavurugwa.

 Jikoni
Waonyeshe wageni vinywaji vinakohifadhiwa ili waweze kujiandalia wenyewe. Waonyeshe kila kitu endapo watahitaji kunywa chai, kahawa, kakao, vinywaji laini na vyoyote vile vingine.

Weka matunda na vitafunwa kama biskuti, korosho na karanga mahali pa wazi ili wageni waburudike wakati usio wa chakula. Hutakuwa na wasiwasi kwamba chakula kimechelewa na wageni wana njaa

Mwishoni kama wageni wanataka kuingia jikoni wasaidie, waruhusu! Hakikisha tu kwamba kazi wanazosaidia ni nyepesi.

No comments:

Post a Comment