Pages

Wednesday, December 14, 2016

Namna ya kupamba mti wa krismasi

Umeshaanza kupata hamasa ya sikukuu? Tunaona mitaani na kwenye maduka makubwa ambavyo wauzaji wanauza mapambo mbalimbali ya sikukuu huku kwenye majengo makubwa na ofisi mbalimbali wakiwa wameshaweka tayari mapambo ya mti wa krismasi. Kila mwaka msimu huu wa sikukuuu duniani kote ni shamarashamra za aina yake.

Nyumbani kwako huenda tayari unao mti wako wa krismasi au
kama bado, ndio uko kwenye mchakato wa kuupata.

Kupamba mti wa krismasi kama mtaalam sio kazi kubwa kivile, na nakuhakikishia baada ya maelezo haya endapo hukuwa unafahamu namna ya kuupamba utafahamu kila kitu. Unachohitaji ni mziki wa sikukuu, mti (ambapo watu wengi siku hizi wanapendelea miti ya bandia), zawadi, mapambo ya kuzungusha, mapambo ya duara, taa za vimulimuli, nyota moja na kitambaa.

Hatua ya kwanza ni kuunganisha mti wako na kuusimamisha wima halafu funika kitako cha mti kwa kitambaa cha rangi ya kijani, nyeupe au nyekundu.

Zungushia taa za kamba za vimulimuli ukianzia juu ya mti kushuka chini. Kama mti ni wa kijani (kumbuka siku hizi ipo hata myeupe) chagua taa ambazo waya wake nao ni wa kijani – hii itasaidia waya ufanane na mti ili kuzifanya  taa ndio zichomoze zaidi. Kama baadaye utakuja kuweka nyota ya mwanga kule kwenye kilele cha mti hakikisha kwenye ncha ya waya wa taa kuna mahali pa kuichomeka. Endelea kuzungusha taa hadi chini kabisa mwisho wa majani.

Baada ya hapo chukua pambo lile refu la rangi za kuendana na mandhari ya mti wako halafu lizungushie tena kwenye mti mzima. Unaweza kutumia pambo hili likiwa kwenye rangi tofauti kama vile silva na nyekundu. Mzunguko upishane umbali wa inchi 4 hadi 6 kuendana na ukubwa wa mti. Kama kawaida anza kulizungushia kuanzia juu kushuka chini.

Halafu chukua vile vipambo vya duara vya kuning’iniza. Navyo unaweza kuchagua vya rangi kadhaa kama vile bluu, nyekundu na nyeupe na pia vya ukubwa tofautitofauti. Haya ndiyo mapambo ya mwisho kwenye mti wako. Yatundike kwa jinsi ambayo unayasambaza kila mahali kwa umbali unaoendana. Haya yanaruhusu mti kung’aa.

Panda kwenye stuli ndefu au ngazi ya ndani, pachika nyota moja pale kileleni. Hili ndio pambo la kujivunia na linaloongeza ladha ya kipekee. Kama ni nyota ya kutumia umeme unganisa na ule waya wa vimulimuli ili nayo itoe mwanga tofauti tofauti.


Mwishoni kabisa panga zawadi chini ya mti, ukianza na kubwa zikifuatiwa na ndogo. Zawadi hizo ziwe zimefungwa kwa riboni na karatasi za kufungia zawadi ambazo zinaendana na rangi za mti ili kuleta pamoja muonekano uliokamilika.

Mara umekamilisha kuupamba mti wako, ufurahie! Ila usisahau kuzima vimulimuli wakati wa usiku au ndani kukiwa hamna mtu.

No comments:

Post a Comment