Pages

Monday, January 23, 2017

Dondoo za upakaji wa makabati ya jikoni rangi mbili tofauti

Hivi ulishawahi kufikiria kuwa na makabati ya jikoni yenye rangi mbili tofauti? Yani ya juu yawe na rangi yake na ya chini yawe na rangi yake tofauti.

Kutokana na uwepo wa rangi nyingi za finishing za makabati ya jikoni, baadhi ya wenye nyumba na wenye nyumba watarajiwa wanafikiria kuchanganya rangi mbili kwa ajili ya makabati ya jikoni. Mtindo huu unakuja kwa kasi kadri nilivyoongea na mseremala Andrew Komba wa kampuni ya kutengeneza fenicha ya Furniture Mart iliyopo Tabata Dar es Salaam. Anasema makabati haya yanaonekana ya kisasa na kufanya jiko lipendeze.

Iwe ni kwa muonekano au kuficha makosa yaliyojitokeza kwenye kupendezesha jiko, kuna sababu nyingi za
kuwa na makabati ya jikoni yenye rangi mbili tofauti. Kama unatafuta njia ya kuongeza  rangi, unaweza kufikiria kuwa na makabati yenye rangi mbili tofauti. Mtindo huu ni mzuri kutengeneza kitovu cha jiko hasa endapo halina kisiwa (mfano wa kauta ndogo ya katikati ya majiko ya kisasa). Kwa majiko yenye kisiwa kwa vile kiko kati kinaweza kuwa ndio kitovu cha jiko.

Muonekano wa jiko ni muhimu kwenye kuleta mvuto. Makabati ya jikoni ya rangi mbili yanakupa wigo mpana wa kubuni jiko lako huku ukihusisha rangi za kuta, kaunta, sakafu na mlango. Pia ni njia nzuri ya kufikia muafaka kama hamuwezi kukubaliana rangi za makabati ya jiko na mwenza wako!

Makabati ya jikoni yenye rangi mbili tofauti (zilizo sahihi) yanasaidia jiko lionekane kubwa. Kwa mfano, jiko dogo lenye dirisha lililoelekea eneo ambalo mwanga wa jua ni kidogo,  makabati yenye rangi nyepesi yatafaa zaidi kuliko ya rangi nzito kwa ajili rangi hizi zinafanya jiko lionekane kuwa na mwanga na kubwa.

Vivyo hivyo, rangi nzito zinapendeza kwa makabati ya chini huku yale ya juu yakiwa na rangi nyepesi.  Mtindo huu una faida kadhaa ambazo ni pamoja na kulifanya jiko lisionekane kujaa na vilevile kutengeneza hisia  za eneo kuwa kubwa kuliko lilivyo. Vile vile haya ya chini yenye rangi nzito yanalipa jiko hisia za kinyumbani zaidi.

Mtindo wa kupaka makabati ya juu rangi nzito na ya chini nyepesi haujapendelewa na wengi wenye kutaka kabati za rangi mbili. Ila faida yake ni kwamba makabati ya juu ya rangi nzito yanaleta hisia ya dari kuwa chini hivyo kuweza kuonyesha zaidi ubunifu wa usanifu wake.

Endao unataka kupaka makabati ya jikoni rangi mbili tofauti unapaswa kuhakikisha kuwa rangi hizo zinaendana na za maeneo mengine ya jiko.


Mwishoni kabisa kumbuka kuwa endao unapaka makabati rangi mbili tofauti itapendeza kaunta zikiwa nyeupe au krimu laa sivyo zikiwa nazo ni ya rangirangi jiko linaweza kuonekana halijatulia kwani makabati na kauta viko jirani mno.

No comments:

Post a Comment