Pages

Monday, March 13, 2017

Michoro ya ukutani ya Kitanzania unayoweza kutumia kupendezesha nyumba

Huenda unataka kupendezesha kuta za nyumba yako kwa sanaa za Kitanzania lakini inakupa changamoto kuwa sanaa hizo ni zipi. Labda umeshajenga au kurekebisha nyumba vizuri ila hatua iliyobaki umalizie ni kupendezesha kuta zake kwa sanaa. 

Makala hii inakufungua fikra uone ni aina zipi unazoweza kutumia. Kiukweli zipo mbalimbali na kwa wigo mpana. Nimeongea na dada Suma wa Tanzania Cultural Heritage waliopo jengo la Quality Center na hapa amenyambua aina mbalimbali za michoro ya ukutani ya Kitanzania kama ifuatavyo.

1.       Michoro  ya tingatinga
Tingatinga ni aina ya michoro ambayo ilianzia maeneo ya Oysterbay Dar es salaam kwenye karne ya 20 na baadaye ikasambaaa Afrika Mashariki nzima. Jina Tingatinga limetokana na mwanzilishi wa michoro hii aliyekuwa anaitwa Edward Saidi Tingatinga.

Michoro ya tingatinga haina uhalisia, kwa mfano mchoro wa
twiga utaonekana ni twiga lakini sio kama alivyo twiga halisi. Michoro hii ina rangi kali za kuvutia na kwa kawaida ni midogo ambapo pia imekuwa rahisi kwa watu mbalimbali hasa watalii kuinunua na kusafirisha makwao. Badala ya kuwaachia wageni pekee kufurahia uzuri wa michoro ya tingatinga inawezekana uzuri huu ukawa sehemu ya ndani ya mahali unapoishi.

2.       Michoro y kisu
Michoro hii ni ya kupendezesha nyumba ukutani kama ilivyo kwa ile ya tingatinga. Tofauti yake ni kwamba michoro ya kisu inaonyesha picha halisi, kwa mfano kama ni mchoro wa mtumbwi ni  kwamba unaonekana kabisa kama mtumbwi ulivyo.

3.       Michoro ya Zanzibar
Kama jina lake lilivyo ni kwamba michro hii inaakisi muonekano wa mandhari ya Zanzibar kama vile ni milango,  ufukwe na majengo mbalimbali ya Zanzibar.

4.       Michoro ya kanvasi
Michoro ya kanvasi ipo ya aina mbili ambapo aina ya kwanza ni ile iliyoko kwenye kanvasi moja na ikakamilika. Aina ya pili ni ile iliyopo kwenye kanvasi zaidi ya moja ili kuufanya mchoro mzima ukamilike. Kanvasi hizo zinaweza kuwa tatu au nne na ukiondoa moja mchoro wote unapoteza maana.

5.       Michoro ya magamba ya ndizi, henna na ngozi
Kundi la mwisho la michoro ya ukutani yenye muonekano wa Kitanzania ni ile iliyotengenezwa kwa magamba ya ndizi, ngozi au henna. Michoro ya henna inatengenezwa zaidi Tanzania visiwani.

Kwahivyo kwa wewe msomaji wangu unayehitaji kupendezesha kuta za nyumba kwa michoro yenye asili ya Tanzania, hayo ndio makundi ya michoro unayopaswa kuzingatia.

Kama una bidhaa au huduma zihusianazo na nyumba nijulishe tufanye mahojiano 0755 200023

No comments:

Post a Comment