Jinsi
ya kuvaa ukiwa unatokea ofsini kwenda kwenye kimnuso
|
Ni
saa kumi na moja jioni lakini sio muda wa kwenda nyumbani. Badala yake, kuna
kimnuso na wanawake wengi walivyo ni tukio ambalo linaweza kukuacha ukihangaika
juu ya nini huku duniani cha kuvaa kazini siku hiyo ili uunganishe na mtoko
wako huo wa usiku.
Mbaya zaidi ni kuwa huna muda wa kwenda nyumbani kubadili ni lazima utokee kazini ulikokuwa umekaa mbele ya komptyuta moja kwa moja kwenye usiku wa tafrija na shampeni. Lakini kabla hujaumia kichwa zaidi, vitupio vinaweza kubadili kabisa muonekano wa vazi fulani kutoka muonekano wa kiofisi kwenda kwenye usiku wa sherehe.
Sasa
ni wapi pa kuanzia? Anza siku yako kwa kuvaa sketi fupi ya rangi yoyote na koti la rangi
isiyofanana na sketi na kiblauzi ndani mwake. Usisahau mchuchumio wako
kuonyesha umbile na urembo wako. Baada ya saa za kazi wakati wa kuelekea
kwenye tafrija kama hutaweza kwenda nyumbani kubadili nguo unaweza kubaki na
kiblauzi cha ndani ya koti na kuacha koti lako kwenye gari na beba pochi na
sio ule mkoba mkubwa wa kazini.
Siri
ya kuvaa nguo zile zile ila mionekano tofauti kutoka mchana kuingia usiku ni
mpangilio wa nguo na vitupio vyako.
Changanya mavazi yako na vitupio kuendana na shughuli ya wakati husika ili
mavazi yale yale yawe na mionekano tofauti. Jenga taswira mbalimbali kwa
mfano kiatu hichi hicho ila na pochi tofauti tofauti inaonekanaje. Taswira ni
msingi wa mafanikio yako.
Hereni
zina nguvu kubwa ya kubadili muonekano wa mavazi ya kiofisi kwenda kwenye mg’ao
wa muonekano wa usiku. Kama huwa huvai hereni kazini au unavaa vile vidogo
sana basi usiku ni wakati wa kuvaa hereni kubwa zinazong’aa ambazo huwa
zinabadilisha hata mavazi rahisi kabisa. Jaza shingo yako na mkufu au hata
mtandio wenye rangi za kuwaka utabadili muonekano wa ofsini kuwa wa sherehe.
Hii itasaidia kuleta mwanga na rangi usoni mwako na hivyo kubadili muonekano
wako mzima. Kuendana na mtindo uliopo kuna wakati vidani, mikufu au shanga
zinavaliwa zaidi ya mmoja na unaweza basi ukaongeza na bangili.
Pete
kubwa yenye jiwe kubwa kati
iliyovaliwa kwenye kidole chochote inabadilisha muonekano wa kiofisi
kuwa wa kisherehe zaidi. Pete hii moja tu inatosha usivae zaidi. Hakuna kitu
kinachoonyesha unaelekea kazini kama mkoba wako. Mkoba unaweza kuharibu
kabisa muonekano wako wa vazi la sherehe. Kwanye sherehe beba pochi (ile
ndogo ambayo mara nyingi si ya kutundika) na weka vile vitu muhimu sana ambavyo
ni lazma unavihitaji popote uwapo kama vile leseni ya udreva, pesa taslimu
kidogo, kadi ya ATM, simu na funguo. Wakati wa kutoka kuelekea kwenye mnuso
unaweza kufungia mkoba wako kwenye droo la ofsini na kuuchukua kesho yake.
Kumbuka mkoba usiache kwenye gari kwani ni kishawishi kwa wezi wa kwenye
magari.
Linapokuja swala la vipodozi, ukiwa unatokea ofsini kwenda moja kwa moja kwenye sherehe usijaribu kujipaka tena uso mzima. Badala yate tumia vichache tu kama lipstiki, ongezea mascara kidogo na kimguso cha poda kuondoa mngao kwemye uso wako na ongeza vipodozi kwenye mashavu. Weka shedo za macho zenye rangi za silva na dhahabu. Vipodozi vya kwenye mashavu vizidi kidogo usiku kulinganisha na wakati wa kuwa ofsini.
Kwa nywele za chap chap chana
ulizonazo kama ni fupi ama funga kifagio kama ni ndefu na kuongezea kibanio.
Hizo hereni zako kubwa tayari zitakuwa zinashirikiana na nywele kuleta mvuto.
Mtandio
ama skafu inasaidia sana kubadili muonekano wa mavazi toka siku ya kazi
kwenda usiku wa kimnuso. Kwa ofsini funga kitambaa chako hicho shingoni
wakati usiku unaweza kufunga mtandio
au skafu yako kiunoni kama mkanda.
Rangi
zinaweza kuvalika kutokana na uamuzi wako ila nyeusi na nyeupe bado ni
maarufu kwa wanawake. Vaa rangi kazini lakini zigeuze kuonyesha urembo wako
nyakati za usiku.
Harufu
yako ni muhimu kukamilisha muonekano wako mzima; inakupa utambulisho, wakati
wa mchana tumia pafyum zenye ladha za maua ila usiku tumia pafyum yenye harufu
kali zaidi kusisitiza utu wako.
Kama
una mtoko utakaokugharimu kutokea ofisini moja kwa moja fuata dondoo hizi na
zitakuongoza kupata muonekano wako wa kazini na usiku siku hiyo.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni
niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23.
|
Pages
▼
No comments:
Post a Comment