Pages

Tuesday, November 6, 2012

My article for newspaper: Mapambo ya bafuni



Mapambo ya Bafuni
Ongeza mvuto bafuni kwako kwa gharama kidogo tu. Kuanza kujenda bafu tokea mwanzo ni gharama ila kuongeza mvuto kwenye lililoko tayari sio kazi kubwa. Kwa baadhi ya watu bafuni ni sehemu ambayo inaachwa kando (au ya mwisho kabisa kufikiriwa)kwenye maswala haya ya mapambo ya ndani. Fahamu kuwa bafuni panaweza kubeba ujumbe mzito hasa kwa wageni wanaokutembelea nyumbani.

Unapopanga kupamba bafu lako (au chumba kingine chochote) pa kuanzia ni kwenye ukuta. Ukuta unachukua sehemu kubwa ya chumba kwa hivyo fikiria ungetaka ukuta wa bafu lako uweje. Je unapenda kuweka taili ukuta wote hadi juu au nusu tu halafu umalizie na rangi. Taili hadi juu ni gharama ila inasaidia kunyonya mvuke hasa kama bafu linatumika na maji yote ya moto na baridi. Pia kama huwezi kuweka taili kuta zote unaweza kuweka hadi juu kwenye kuta za eneo la kuogea na kuta zingine ukaweka nusu ili kujipambia kwa kupiga rangi mbalimbali kwenye kuta zilizobaki bila taili. Taili za kufika hadi mwisho wa ukuta zimeonekana kuleta muonekano wa usafi zaidi na hata kama kuna mapambo au vitundikio vingine unapenda kuweka ukutani basi kuna mashine za kutoboa ukuta wenye taili na hivyo kuweza kutundika mapambo yako kirahisi.

Eneo la kuogea
Taulo na vizulia vidogo vyenye plastiki kwa chini za kuzuia maji ni vitupio muhimu bafuni; utakapoweka vya rangi mbalimbali na kuvibadili mara kwa mara basi vitabadili muonekano wa bafu zima. Weka pazia la eneo la kuogea lenye mvuto linalooana na rangi za taili.
                                                                                                                                                    Eneo Eneo la sinki
Kwa kuboresha muonekano wa eneo hili njia kuu ni kubadili staili ya bomba la sinki. Mabomba ya sinki yanakuja na mitindo mipya kila leo kwa hivyo kwa kuweka bomba jipya itabadili muonekano mzima wa eneo hili. Kama kioo juu ya sinki ni kidogo badili uweke kikubwa ambacho pia kitasaidia kuongeza mwanga bafuni. Badilisha taa ya juu ya kioo iendane na rangi nyingine za hapo bafuni kama vile rangi za mataulo au hata za pazia la eneo la kuogea.

Labda hili ni bafu lako la kuanza maisha baada ya kuachana na wazazi iwe ni kwa kuanza maisha ya ndoa au maisha ya peke yako ya kujitegemea basi kuna vitu kadhaa ambavyo ni muhimu kuwa navyo bafuni. Nimeorodhesha vitu ambavyo nadhani ni muhimu kuwapo bafuni kwako nyumbani, na kwa kweli nimechagua vile ambavyo vinavutia! Unaweza kuishi bila baadhi ya hivi vitu lakini kwa nini ufanye hivyo?
Kumbuka unastahili sehemu nzuri ya kujiandaa kabla ya kwenda kuchakarika siku nzima. Kwa nini usiwe na kila unachohitaji mahali hapo?

Bafuni pawe na mwanga wa kutosha. Linapokuja swala la taa za ndani, bafuni mara nyingi hapapewi kipaumbele na ni pa mwisho kufikiriwa kati ya vyumba vingine vyote. Wenye nyumba wengi wanaweka zaidi hela yao kwenye taa za sebuleni na jikoni. Bafuni kunahitajika taa hasa eneo la kioo, wengi wanaweka ile taa moja tu ya juu ya kichwa. Bafuni ni sehemu ya kuhuisha mwili kwa kuumwagia maji na ni sehemu ya kuanzia na kumalizia siku yako hivyo tusipasahau wakati wa kuamua swala la mwanga wa nyumba.
Bafuni kuwe na vioo vya kukidhi hitaji lako. Weka kioo popote bafuni unapodhani ya kuwa unahitaji kuweka kioo. Usinganganie tu utamaduni wa kioo cha bafuni kinakuwa juu ya sinki. Pia kuwe na seti ya mataulo yale hasaa ya kukausha maji na sio hayo ya barabarani yenye nailoni yasiyokausha vizuri.                                                                                                      
 

Vizulia, pazia la eneo la kuogea na kindoo cha uchafu maalum kwa mazingira ya bafuni ni muhimu viwepo bafuni.                                        
Bafuni kuwe na vifaa sahihi vya usafi na eneo la kuhifadhia . Pia mlango na kioo cha dirisha viwe vimetengenezwa kwa jinsi ya kuwepo faragha.

Kiwekeo cha miswaki ni kitu kidogo na  hutakiona cha maana kuwepo bafuni hadi pale mswaki wako utakapoanguka chini au chooni. Usisahau kuweka sabuni na taulo la mikono kwa ajili ya wageni.
 
Je kuna chochote hapa ambacho kimesahaulika kuwepo bafuni? Kuna katika orodha hii ambacho unadhani hukihitaji bafuni kwako? Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.k au simu namba 0755 200023

No comments:

Post a Comment