Pages

Thursday, November 1, 2012

My article for newspaper: Muonekano wa jiko



Muonekano wa Jiko

Jikoni huenda ni mahali ambapo panadharaulika sana kwenye nyumba za watu wengi; wanafikiria jiko kama ni mahali au chumba cha kupikia chakula tu kwa hiyo mapambo mahali hapo hayahusu. Hawawezi wakawa wanakosea zaidi ya kufikiria hivi; jiko linaweza kuwa mahali pazuri kuliko pote katika nyumba unayoishi kama una staili na unajua jinsi ya kupamba.

Jikoni ni moja ya sehemu muhimu sana kwenye nyumba yako. Ni sehemu ambayo pia inatembelewa mara nyingi zaidi kwa siku kuliko sehemu nyingine yoyote hapo nyumbani. Unatakikana kwenda jikoni mara kadhaa kwa siku, kuandaa chakula au hata kuchukua glasi ya maji baridi. Hutataka kuona jiko lako likiwa limejaa uchafu mavumbi na mafuta. Zaidi ya yote jiko linatakiwa kupambwa na kuonekana maridhawa na linalohuisha nafsi.

Chumba cha jiko la kawaida la kisasa kinakuwa na vitu kama jiko, sinki la maji moto na baridi, jokufu, makabati, kipasha chakula na vifaa vingine vya umeme. Yapo majiko makubwa kwa wenzetu wa magharibi ambapo kwao zaidi ya chumba cha jiko kuwa ni mahali pa kuandaa chakula pia ni mahali pa kufulia, kulia chakula na stoo ya kuhifadhia vyakula. Kubuni jiko la kukidhi mahitaji yako iwe ni kwa nyumba mpya au kubadilisha muonekano wa jiko la zamani inabidi kutembea na kutafiti kwa kuangalia aina mbalimbali za majiko ambayo tayari walau yanakidhi mahitaji ya jiko la kawaida ndipo nawe ukaweza kujiamulia la kwako. Kuna wataalamu ambao wanaweza kubadili jiko lako na kuwa la kisasa kuendana na mahitaji yako.

Chumba cha jiko kinahitaji vyombo ambavyo ni vya kawaida kwa walau kila mtu au familia. Sasa unamsaidiaje mtu ambaye anaanza maisha na anahitaji jiko. Lengo la makala hii ni kuongelea muonekano wa jiko la kisasa la kawaida kabisa sio hayo yenye sehemu ya kulia hapo hapo na sehemu ya kufulia.
Ingawa kuna aina mbalimbali za majiko kwa kila kaya, bado unaweza kujaribu kitu kipya na cha kisasa kwa ajili ya sehemu hiyo ambayo inatembelewa kuliko zote katika nyumba yako. Jiko lako ni mahali panapotakiwa kuwa na mvuto na pia kufanyia kazi kwa uhuru kwa kuwa na vifaa vinavyohitajika.
Vyombo kama sahani, vijiko, glasi na vikombe vinategemea zaidi ladha ya mtu binafsi hivyo sitaviongelea hapa. Vitu vifuatavyo vitafanya jiko lako liwe nadhifu:
  • Makabati
Aina ya makabati utakayochagua na mpangilio wake unatoa picha kubwa ya jiko kwani makabati yanachukua nafasi kubwa zaidi katika chumba cha jiko. Unaweza kuchagua makabati ya mbao hadi ya chuma ila ya mbao yanapendeza na yanadumu kuliko yote. Ya chuma yamekaa kiviwandani zaidi sio kwa ajili ya nyumba za kuishi. Kama una vyombo ambavyo ungependa vionekane basi weka makabati ya mbao ila yenye milango weka vioo. Vitasa na  mikono ya makabati na madroo na hata bomba la sinki visiwe vya urembo mwingi ila tu hakikisha ni imara na vina usalama kwa mfano visiwe na ncha za kumkwaruza mtumiaji. Vitu vyenye urembo mwingi vinaharibu muonekano wa jiko.

  • Sakafu
Jikoni kunatumika na kila mwanafamilia hivyo inatakiwa kuwa na sakafu ambayo ni imara na isiyoharibika kirahisi. Kama una watoto wadogo basi ni vyema kuwa na sakafu isiyoteleza, ambayo pia ni rahisi kusafisha kwa ajili watoto wana tabia ya kuokota vitu chini na kuweka mdomoni. Haishauriwi kuweka zulia jikoni kwa kuwa kuna mafuta na majimaji yanawagika chini wakati wa kupika na kusafisha vyombo na jiko lenyewe.
  • Hifadhi
Kama unahitaji sehemu ya ziada ya kuhifadhia zaidi ya makabati basi unaweza kuweka vitundikio vya masufuria au viraki kwenye kona ambayo unaweza kuweka vitu vidogovidogo.
  • Mwanga
Jiko linahitajika mwanga mwingi kwa kuwa shughuli nyingi na vifaa vingi vinatumika hapo kwa ajili ya kuandaa vyakula. Pia dirisha la kupitishia mwanga na hewa liwe kubwa kwa kuwa joto jingi linazalishwa jikoni na kwa mfano hapa kwetu watu hawana mazoea pia ni wachache sana waa uwezo kifedha wa kuweka kiyoyozi jikoni. Feni ya jiko kwa ajili ya kunyonya mvuke ikiwepo itakua vyema.
Mapambo ya jikoni sio kama ya chumba kingine kwa mfano chumba cha kulala au sebule, jiko linaweza kupambwa kipekee bila kuhusisha muonekano wa vyumba vingine. Nyumba yako bado itakuwa inavutia hata kama jiko limepambwa tofauti kabisa na vyumba vyote. Yote kwa yote, muonekano wa jiko lako unaweza ukavutia zaidi ya unavyofikiri kama una ladha ya staili na mitindo  basi unaweza kufanya jiko lako likawa ni sehemu kila mwanafamila anapenda kutembelea na pia kurahisisha kazi ya mpishi. Muhimu zaidi ya yote jikoni napo papambwe kama ilivyo vyumba vingine ndani ya nyumba yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23

No comments:

Post a Comment