Pages

Thursday, April 18, 2013

My Article for Newspaper: Jiko lenye mpangilio


Siri ya jiko lenye mpangilio mzuri

Muulize mwenye nyumba yeyote, atakuambia kuwa kati ya vyumba vyote kwenye nyumba yake, jikoni ni sehemu ambayo inatumika zaidi. Iwe ni kwa kupika, kula au hata burudani chumba cha jiko kinatumika kuliko vyumba vingine vyote. Kama mama uliye na shughuli nyingi unatakiwa kuwa na jiko lenye mpangilio wa kurahisisha shughuli ya kuandaa chakula bora kwa ajili ya familia yako. Hii inawezekana kwa kuwa na kila unachohitaji mkononi kwa maana ya kwamba kutoanza kutafuta chombo kimoja kimoja wakati wa kuandaa chakula kuanzia kisu, sufuria, kitaulo na hata sabuni ya kusafishia. Wakati unapokuwa una kila kitu unachohitaji kwenye ncha ya vidole vyako ni wazi kuwa utaandaa chakula bila msongo wa mawazo!

Kutokana na shughuli na matumizi mengi ya jiko ni muhimu jiko lako liwe na mpangilio mzuri kadri iwezekanavyo ili kuweza kurahisisha mambo. Hata hivyo kutokana na vitu vingi ambavyo jiko linabeba – vyakula, sufuria, vijiko, visu sahani vikombe,vifaa vya umeme na kadhalika ni kawaida kukuta kuwa chumba hiki ambacho kinatumika zaidi ndio chenye mpangilio dhaifu kuliko vyote.
Lakini jipe moyo kwa kusoma makala hii unaweza kuwa na mpangilio mzuri jikoni kwako.
Ondoa mrundikano kwenye kaunta za jiko. Hifadhi uma, visu na vijiko kwenye droo na sio kwenye kaunta ndani ya kibebeo. Kuondoa mrundikano kwenye kaunta kutafanya jiko liwe na mpangilio na mvuto.

Safisha makabati na weka vyakula kwenye makontena yenye mifuniko. Kuacha vyakula vya maboksi vilivyofunguliwa tayari kwenye makabati kunaleta mende, panya na wadudu wengine jikoni. Kwa hivyo vyakula vyako kama unga na mchele weka kwenye kontena zenye mifuniko isiyoingiza hewa, namna hii itakuwa rahisi kuchukua vyakula kirahisi wakati wa kupika na pia kuvihifadhi visishambuliwe na wadudu na kuokoa hela yako kwa vyakula kubaki na ubora wa awali kwa muda mrefu!

Wekeza kwenye zana sahihi za kuweka mpangilio mzuri jikoni kwenye makabati ya vikombe, vikaangio na sufuria.

Tembelea kwenye jokofu. Umeshaangalia kwenye jokofu na ukakutana na mboga mboga na matunda? Osha vyakula vinavyotakikana kuwekwa kwenye jokofu na viweke kwanza ndani ya kontena au mifuko inayoonyesha vilivyomo ndani, baada ya hapo ndio uweke ndani ya jokofu. Kuwa na vyakula ndani ya jokofu vilivyohifadhiwa kwenye kontena kunarahisisha kupata unachotafuta wakati wa kupika au wa kuandaa orodha ya sokoni. Watu wengi hawachukui muda kupanga ndani ya majokofu yao, lakini nguvu zinazotumika hapo zinalipa kwa ajili ni njia rahisi ya kuokoa muda, pesa na nafasi. Panga vyakula kwenye shelfu za jokofu kwa mtiririko wa kueleweka kwa mfano shelfu la mbogamboga, la matunda, la vitafunwa na kadhalika. Fanya milango ya jokofu iwe ni kwa ajili ya vitu vya kipekee kama dawa. Mpangilio huu utasaidia kutokuwa na jokufu lenye mrundikano na hivyo kuokoa muda wa kupata kile unachotafuta.

Watu wengi hawapendi kusafisha jiko baada ya chakula cha usiku, lakini kwa bahati mbaya ni lazima jiko lisafishwe ili lisiwe makazi ya mende, panya na wadudu wengine watakaokuja kujifaidia makombo ya vyakula wakati wa giza. Ili kupunguza kazi ya kusafisha baada ya chakula ni vyema kusafisha kidogo kidogo kadri unavyopika na sio kuacha kila kitu hadi mwishoni. Kwa mpishi anayependa kuweka jiko safi ataendelea kufuta kaunta wakati huo huo anapika. Hakikisha jikoni kunakuwa na sabuni maalum za kusafisha jiko.

Pamoja na ajira, kuweka nyumba safi na kulea familia, inaweza kuwa ngumu kwa mama yeyote kuwa na mpangilio mzuri jikoni, lakini sio kwamba haiwezekani. Cha muhimu ni kuwa hakikisha jiko lako linakuwa kwenye mpangilio ambao chochote unachohitaji hapo unakipata mara moja na hata kwa mwanafamilia mwingine inakuwa hivyo hiyvo. Ijulikane kwa wanafamilia wote kwa mfano visu vinakaa hapa, sahani zinakaa pale na kadhalika. Mara unapoweka jiko lako kwenye mfumo wa mpangilio fulani basi ng’ang’ania mfumo huo. Kwa bahati nzuri kama una mwenza anayekujali basi mama wa familia unaweza kuwa kama mashine iliyotiwa mafuta vizuri na kuweza kumudu majukumu yako mengine na wakati huo huo kuwa na mpangilio utakaoleta mvuto na kurahisisha maisha jikoni.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment