Pages

Thursday, July 11, 2013

My article for newspaper: bustani hewani




Una ardhi ndogo lakini unahitaji bustani? Fikiria vyungu vya kuning’iniza.

Vyungu vya maua vya kuninginiza ni njia inayopendwa ya kupendezesha makazi yako kwa kuotesha humo mimea utakayoipenda na kuvitundika kwenye maeneo ya ukuta utakayochagua iwe ni ndani au nje ya nyumba. Vyungu vya maua vya kuning’iniza vinasaidia kuongeza rangi kwenye ukuta wa nyumba yako, veranda na bustani. Vyungu hivi vinaweza kutumika kwa ufanisi hasa kwa nyumba yenye eneo dogo la nje na vinaweza kuwekwa kama mapambo kwenye eneo ambalo linahitajika kupambwa. Kama ukichagua maua vizuri bustani zako hizi za hewani zinaweza kudumu kwa miaka kadhaa kwa wewe kuvipaka vyungu rangi tofauti tofauti kuendana na msimu.

Sokoni kuna aina mbalimbali ya vyungu vya maua vya kuning’iniza. Fikiria ni vyungu vya namna gani vitaendana na mapambo yako  ya ndani kama unataka kuvining’iniza ndani ya nyumba na pia mandhari ipi itaendana vyema na bustani yako na maua unayotaka kuotesha humo. Vyungu vya maua vilivyotundikwa ndani kwenye maeneo ya kona ya ukuta vinafanya eneo la sakafu liwe huru na vinapendezesha ukuta wa kona, ule wa sehemu wa kuingilia na hata ule wa sebuleni. Sanaa za kuning’iniza sebuleni kwako zinawasalimia wageni, zinaelekeza njia na pia zinapambana kwa uzuri na rangi za ukuta Kama hutaki kuweka vyungu vya maua vya kuning’iniza ndani ya nyumba basi weka kwenye ukuta wa nje wa nyumba kwa maeneo ya dirishani kwa mfano vinafaa sana kwa kuleta faragha na maua yake yanavutia kuangalia ukiwa ndani.

Vyungu vya maua kwa ajili ya kuning’iniza vinatakiwa vile vyepesi. Hakikisha kuwa vyungu vyako vina matobo kwani udongo unaosimamisha maji muda wote unafanya mizizi ya mimea ioze kwa hivyo mimea kufa. Vyungu vya plastiki ni vyepesi ila tahadhari ni kuwa vinapasuka kirahisi ikiwa eneo vilivyotundikwa vinachomwa na jua kali. Vile vile vyungu vya maua vya kuning’iniza vinahitaji kuwekwa kwa vyuma imara kwani huwa vinakuwa vizito hasa wakati wa kumwagilia. Epuka kusababisha ajali kwenye familia yako pale chungu cha kuning’iniza kitakapomdondokea mwanafamilia.
Vyuma vilivyochimbiwa ukutani kwa ajili ya kushikilia vyungu vya kuninginiza vinatakiwa kuwa imara. 

Chungu chenye udongo na mimea kinaweza kuwa na uzito wa hadi kilo kumi na hiyo ni hata kabla ya kumwagilia. Halafu pia kumbuka kama chungu kimening’inizwa sehemu ambazo hazina paa ni kwamba maji ya mvua yatakuwa yanaingia moja kwa moja hivyo kukifanya kuwa kizito zaidi.
Kabla ya kutundika chungu chako cha maua cha kuning’iniza zingatia pia mahali unapokiweka. Je hali ya hewa ya mahali hapo kwa mfano jua la kuchoma mmea moja kwa moja halitauathiri? Ni upande upi upepo unakoelekea. Hali ya hewa ya joto kali na upepo utauvunja vunja mmea. Upepo mkali unaweza kuukausha mmea na pia kuvunja matawi madogo madogo. Halafu pia kama mmea unaootesha hautaki maji mengi mvua inaweza kuuozesha. Na kitu kingine zaidi cha kuzingatia ni kama katika eneo husika kuna kitu kinachoakisi joto kwa mfano lango la chuma linalopigwa na jua au pia kuna rangi za ukuta za namna hiyo hata kama mmea unastawi kwenye jua kali basi hali hii ya joto kuzalishwa maeneo ya karibu na chungu litauua mmea.

Kwa vyoyote vile, inatakiwa iwe rahisi kwako kumwagilia na kutunza bustani yako ya hewani kwa hivyo hakikisha mahali ulipochagua kuning’iniza chungu chako panafikika. Kwa mfano hutataka kuwa unakanyaga maua mengine ya bustani ya ardhini ili kukifikia chungu, na kama kimening’inizwa juu sana utahitaji jinsi ya kukifikia. Na zaidi ya urahisi wa wewe kukifikia chungu, angalia eneo ulilokining’iniza isiwe inabughudhi watembeaji wengine au inaziba muonekano.

Kama nilivyosema mwanzo kuwa chungu inabidi kiwe na matobo kumbuka kuwa kitadondosha maji baada ya kumwagiliwa, kwa hivyo kunahitajika kuwe na kisahani kinachoambatana na chungu au unakiteremsha chungu chini ukimwagilie halafu ukiruhusu kukauka ndipo ukirudishe juu. Lakini njia rahisi ni hii ya kuwa na chungu chenye kisahani cha kudondoshea maji kwani maji hayo hayo yanahitajika wakati maji kwenye chungu yanapokauka. Vyungu vya maua vya kuning’iniza na visahani vya kudondoshea maji ambavyo ni vya bei rahisi vinapatikana walau kwenye kila kituo cha bustani.

Sasa basi unafikia wakati wa kuotesha mimea kwenye chungu chako. Kuna mimea lukuki ya kuweza kuotesha kwenye vyungu vya kuning’iniza. Unaweza kuotesha mmea mmoja mmoja au mchanganyiko, iwe ni ya kusimama, kuning’inia ama yote kwa pamoja. Jua mimea inayostawi kwenye vyungu. Weka kwenye kundi moja mimea itakayovumilia mahitaji sawa ya maji, mwanga na joto. Maua mbali mabali inaweza  kuwekwa kwenye vyungu vya kuning’inia, ubunifu wako ndio kizuizi pekee. Inafurahisha kuona mmea ukikua kukubaliana na jinsi unavyouongoza. Katikati ya chungu weka mimea inayotoa maua kupata muonekano wa uhakika!

Ulishasikia hadithi ya bustani za kuning’inia za Babiloni? Bustani sio za ardhini tu, kama huna ardhi ya kutosha lakini unapenda bustani weka basi hizi za vyungu vya kuning’iniza uongeze uzuri angani!.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment