Pages

Thursday, July 18, 2013

My article for a newspaper: Kizulia cha jikoni



Malizia muonekano wa jiko lako kwa kuweka kizulia

Jikoni ni sehemu inayopitwa zaidi. Kwa familia zinazopenda mapambo ni kawaida kukuta kizulia kwenye maeneo ya mbele ya stovu na sinki au maeneo mengine ambapo mtu anasimama kwa muda mrefu jikoni.  Vizulia hivi sio tu vinasaidia kuhifadhi sakafu ya maeneo haya isisharibike zaidi ya yale mengine ambayo hayakanyagwi sana bali pia vinasaidia kuburudisha miguu. Na pia unaweza kuweka kizulia jikoni kwa lengo la kupamba. Vyovyote iwavyo, uchaguzi wa kizulia cha jikoni ni tofauti na vile vizulia vingine vya ndani. Unatakiwa kuzingatia uimara, umachachari wa kuzuia madoa na vifaa vilivyotengenezea kizulia husika. Makala hii itakuambia jinsi ya kuchagua na utunzaji wa kizulia cha jikoni kwa lengo la kumalizia muonekano wa jiko lako.

Miaka nenda rudi jikoni kwako pamekuwa ni mahali pa kufanyia kazi ya kuandaa chakula. Badili jiko lako liwe ni sehemu ambayo inavutia zaidi kwa mguso wa rangi za kizulia cha jikoni. Jikoni panapovutia panakuwa ni mahali unapotamani kwenda na si mahali ambapo inakulazimu kwenda. Unakapoweka jiko lako katika mandhari ya kuvutia utashangaa wageni wako wanaoingia kwa kupitia mlango wa nyuma wanakosea njia kwa kuelekea jikoni badala ya kuelekea sebuleni!

Kitu kizuri kuhusu vizulia vya jikoni ni kwamba viko tofauti na ukawaida wa muonekano wa jiko. Watu wengi wanang’ang’ania marumaru nyeupe au za rangi ya krimu jikoni na hii ni sifa ya rangi za jiko toka enzi na enzi. Kwa kuweka kizulia cha rangi tofauti utahuisha muonekano wa jiko lako.
Chagua eneo unalotaka kuweka kizulia , ambalo mara nyingi ni lile linalokanyagwa zaidi au linalokanyagwa kwa muda mrefu kwa mfano chini ya meza, eneo la kuingilia, mbele ya stovu au chini ya sinki au jokofu. Baada ya hapo pima ukubwa wa eneo hilo unalotaka kufunika kwa kizulia. Hii itakusaidia kutupilia mbali kizulia kikubwa sana au kidogo sana wakati wa manunuzi.
Chagua umbo la kizulia kwa kipimo na aina ya fenicha. Kwa mfano, kama unataka kizulia kiwe chini ya meza ya duara basi chagua kizulia cha duara. Amua kama kizulia hiki ni cha mapambo, je ungegependa kiwe cha rangi moja? Unaweza kuchagua rangi ambayo inaoana na ya kabati zako za jikoni au kaunta, au unataka kigeuze shingo kwa kuwa na michoro ya rangi zilizokolea.
Kizulia chenye rangi ya kukolea kitaonyesha madoa machache na uchafu kidogo. Zingatia pia urahisi wa kukisafisha kwani kizulia cha jikoni kiko kwenye hatari ya kupata madoa zaidi ya kizulia kwenye chumba kingine chochote.  Chagua kizulia ambacho hakitelezi kwa maana ya ukikikanyaga kisihame kutoka eneo moja kwenda jingine iwe ni kwenye sakafu ya mbao au marumaru kwani ni hatari kwa mtumiaji kwani kinaweza kumwangusha.
Doa kwenye kizulia cha jikoni linaweza kuwa chochote kutoka kwa mtoto, kikombe kilichoanguka toka juu hadi nyayo zenye tope. Kushughulikia madoa ya kizulia cha jikoni barabara ndio kunakotofautisha mabingwa wa usafi na watu wengine. Unaweza kujiita mtaalam kama utaweza kupambana na madoa ya kizulia chako cha jikoni. Ila kiukweli huhitaji nguvu nyingi kushughulikia madoa hayo.
Kwanza unatakiwa kuwa tu na hisia za kawaida. Kuchukua hatua mapema kuondoa doa lolote mara linapotokea kwenye kizulia cha jikoni kwa wakati huo huo.  Doa liliosahaulika litaumiza kichwa baadaye. Na doa la aina hii linaweza kuharibu kabisa muonekano wa kizulia chako. Kama ukiliacha doa bila kulishughulikia mapema linazama hadi mwanzo wa nyuzi za kizulia na hii itahitaji nguvu kubwa kulishughulikia. Kwahivyo kila wakati kuwa na hisia. Tenda mapema na kwa ufanisi.
Kuna madawa mengi yaliyoaminiwa kwa ajili ya kuondoa madoa ya kwenye zulia. Tembelea maduka yanayohusiana na mambo hayo uwe na dawa yako nyumbani wakati wote.
Kumbuka, jiko lako halitakiwi kuwa ni mahali pa kuandalia chakula tu. Unaweza kubadili jiko lako kuwa kivutio ndani ya nyumba yako kirahisi tu kwa kuleta mguso wa rangi na furaha japo kwa kuweka kizulia cha jikoni.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment