Pages

Thursday, November 28, 2013

My article for newspaper: Safisha mifereji

Masika yanaanza, safisha mifereji kabla haijasafisha mifuko yako



Kusafisha mifereji ya maji iliyojengewa kwenye nyumba (gutter) ni moja kati ya kazi muhimu za kufanya kipindi hiki ambacho masika yanaanza. Japo mara  nyingi huwa jambo hili inachukuliwa kijuu juu tu, kwa bahati mbaya wengi wetu tunasubiri hadi madhara yatokee ndio tunafikiria kusafisha mifereji ya nyumba zetu. Kuchelewa kuondoa majani ya miti yanayodondoka na kuingia ndani ya mifereji ya nyumba pamoja na vumbi kunasababisha matatizo makubwa mara mvua zinapoanza. Na hivyo kufanya kazi ya kusafisha iwe ngumu na kubwa zaidi. Majani yaliyoozea ndani ya mifereji pamoja na tope linalosababishwa na vumbi hukutana na maji ya mvua na kufanya tope kubwa zaidi linaloziba mfumo mzima wa usafirishaji maji ndani ya makazi yetu. 

Kama utasafisha mifereji ya maji kwenye makazi yako mara kadhaa kwa mwaka, hasa wakati wa miti kudondosha majani, usafishaji utakuwa rahisi. Mara moja pekee au kuacha kabisa, inaweza kuja kuwa kazi kubwa ambayo itakugharimu hela nyingi kwa shida zitakazotokana na kutosafisha huko.

Tatizo la mifereji iliyoziba ni kuwa maji ambayo yanasimama yanaharibu ukuta wa nyumba. Mifereji ya maji iliyojengewa kwenye nyumba yako imebuniwa kusukuma maji yaende chini kutoka kwenye paa yaende mbali na nyumba na msingi wake kwa ajili ya ukaukaji wa haraka wa maji maeneo yasiyohitajika kusimamisha maji au kuwa chepechepe. Maji yanayobaki yamesimama kwenye mifereji iliyoziba yanatafuta njia na kuweza kupenya kwa kupitia eneo lile ambalo ni dhaifu zaidi wakati yakijitahidi kuondoka, na hii inamaanisha kuwa yanaweza kukimbilia moja kwa moja kwenye ukuta na dari la nyumba yako.

Tatizo la kwanza kabisa la mifereji iliyoziba kwa majani na tope ni kuongezeka uzito. Hayo majani yaliyooza yakiloa, yananyonya maji ya mvua kama sponji na yanakuwa mazito haswaa. Mzigo huu unaweka msongo kwenye mifereji na vishikizo vyake na hii inaweza kuangusha mifereji toka kwenye nyumba. Mifereji iliyoanguka ni gharama kuweza kuirudishia tena, zaidi ya hayo taa au vioo vya dirisha vinavweza kuvunjika wakati mfereji ukiporomoka chini.

Maji yanayofurika kwenye mifereji yanaharibu rangi ya nyumba na pia michirizi ya maji inafanya alama kwenye kuta. Maeneo yenye mbao mirefeji ilikopita nako kunaozeshwa na maji yaliyoziba na kuanza kuvuja.
Msingi wa nyumba na sakafu zenye nyufa ni dalili nyingine pia za mifereji iliyoziba. Kama kwa kipindi kirefu maji hayataondoka kwenye msingi wa nyumba kuelekea sehemu yalikoelekezwa yanaweka kuangusha nyumba.

Sasa ni nini unachohitaji ili kufanya kazi hii ya kusafisha mifereji? Unahitaji vitu vichache kuendana na njia utakayochagua. Ila dhana kuu ni rahisi, ni kuchukua ngazi na kuvuta takataka toka kwenye mifereji. Unahitaji ngazi, ndoo ya kuwekea uchafu, mpira wa bustani na kama utapenda pia glavu.

Ondoa taka kutoka kwenye urefu wote wa mfereji na weka kwenye ndoo kwa ajili ya kwenda kutupa na baada ya hapo fungulia maji kwa kutumia mpira wa bustani ili kuondoa uchafu mdogo mdogo uliobaki. Hakikisha maji yanapita bila kikwazo na huu pia ni wakati mzuri wa kuona kama mifereji yako ina popote panapovuja kwenye kona au maungio. Kama kuna mahali panapovuja unaweza ukanunua silikoni ya kuzibia na kwa urahisi tu ukapaziba. Kumbuka kuwa maji yanatembea kufuata sehemu rahisi kupitia kwa hivyo ukiwa na mfereji unaovuja ni sawa tu na kuwa na mfereji ulioziba.

Kama unapenda sana unadhifu unaweza ukapaka nje ya mifereji yako rangi kufanya nyumba yako ionekane mwaa.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment