Pages

Thursday, December 5, 2013

My article for newspaper: Sehemu ya kukaa kwenye bustani



Boresha bustani yako kwa kutengeneza eneo la kukaa

Bustani zinamaanisha kutizamwa, lakini utakuta mara nyingi zinakaa zenyewe binafsi na maua na miti yake. Bado, kukaa ni sehemu muhimu ya bustani yoyote. Bustani ni kiwakilishi cha maono ya mwenye nyumba na kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa hakuna kanuni zozote muhimu za juu ya namna ya kutengeneza eneo la kukaa la kwenye bustani.
Eneo hili linaweza kuwa la kudumu na maridadi kwa kiwango cha ubunifu wa mwenye bustani.

Benchi lililowekwa kuelekea muonekano mzuri linaweza lisitumike, lakini eneo lililojengewa vizuri likawekwa sofa au viti pamoja na runinga inaweza ikawa ngumu sana kutovutiwa kukaa mahali kama hapo.  Sehemu maalum ya kukaa iliyotengenezwa kwenye bustani inawavuta wageni kwenye bustani, wanaweza wasikae lakini kishawishi na mapenzi viko pale. Zaidi ya yote ni kama kijisehemu cha kujificha kwa ajili ya kusoma au kiusingizi cha mchana. Sehemu kubwa na yenye rangi inaweza kufanya bustani kuwa ya kukumbukwa, hasa kwa watoto.

Kwa hivyo sehemu hii ya kukaa inaweza kuwa rahisi kama viti viwili chini ya mti au kubwa kama vile eneo la kulia chakula nje ya nyumba. Sehemu hii tulivu inakuvuta wewe na wageni wako na kuwazamisha kwenye uzuri wa bustani.

Wewe mwenye nyumba kuwa mbunifu wa eneo hili la kukaa ndani ya bustani yako mwenyewe, fikiria ni wapi pa kuweka eneo hili na jinsi gani litaonekana. Fikiria ramani ya jinsi unavyowakaribisha wageni wako kwenye bustani: Njooni huku. Karibu kiti. Pumzika hapa. Kwa kufikiria maeneo mbalimbali ya bustani yako, na eneo hilo la kukaa litatumika na watu wangapi utaweza kutengeneza eneo la kukaa ambalo utalitumia kwa muda mrefu na ambalo litatumika kama muendelezo wa nje wa nyumba yako.

Kwenye kona ya ukuta wa uzio wa nyumba yako unaweza kutengeneza sehemu ya kukaa kwenye bustani. Fanya chaguzi ambazo zitaendana na eneo lako. Kwa mfano kwa maeneo makubwa, maanguko ya maji na mimea mingi inaweza kufanya eneo zuri la kukaa. Ukubwa na kiasi cha faragha kinacholetwa na eneo hili ni ishara za jinsi gani eneo litatumika. Unaweza kuliweka dogo kwa faragha au kubwa kwa shughuli za kijamii. Kuendana na ukubwa wa bustani unaweza kuwa na eneo kubwa na dogo pamoja kutokana na matumizi yako

Sasa kwenye eneo hili unatakiwa kuweka mipaka. Unaweza kufanya hivyo kwa mimea au kwa kujenga ukuta mfupi uliokaa kisanaa zaidi kwa kutumia mawe ya urembo. Kwenye paa unaweza kuweka mwavuli au hata kufunga makuti yanayowekwa kimkakati.
Sasa umeshaweka mipaka yako na paa kwa hivyo ni wakati wa kuchagua sakafu, wakati huu chagua zaidi ya muonekano tuu. Jiwe linalotumika hapa liwe na mvuto wa kiasili lakini pia lifae kwa matumizi, kuipa sakafu eneo flati na imara la kuweza kuburudika.

Wakati utakapokuwa unachagua aina ya sakafu unayotaka eneo hili iwe ni mawe ya asili, marumaru, vitofali vya kutengeneza, zege ama kokoto zingatia aina ya fenicha utakazosimamisha kwenye hiyo sakafu. Sakafu yoyote utayochagua itatokana na bajeti yako. Kwa mfano fenicha za chuma zenye miguu myembamba zinahitaji sakafu iliyojishindilia. Zingatia pia utelezi, mawe mengine kwa mfano, yanaota wale fangasi wakati wa masika na huwa wanateleza sana. Fanya uamuzi wako wa mwisho kwa kuzingatia sio tu mfumo wa maisha yako na bajeti bali pia matumizi ya vifaa katika sehemu yako hii. Sasa anza pilika za kuweka sakafu.

Mara unapomaliza kuweka paa, mipaka na sakafu ya eneo lako la kukaa kwenye bustani, unaanza kugundua kuwa inakubidi umalizie eneo hili ambapo ni pamoja na kupaka rangi, kuweka taa za urembo na mapambo mengine ya ukutani na kuweka fenicha tayari kwa kukaa. Usisahau kuweka njia ya mawe ya kukanyagia ya kukufikisha kwenye eneo lako la kukaa. Weka taa na mapambo ya rangi mbali mbali yatakayobadilisha eneo hili kutoka eneo rahisi la kukaa na kuwa eneo la kukaa lenye mvuto la nje ya nyumba yako.

Operesheni tengeneza eneo la kukaa kwenye bustani imekamilika.

Moja kati ya sifa ninazosikia wenye nyumba waliobadili sehemu ya bustani zao kutengeneza eneo la kukaa kwenye bustani wakitukuza ni jinsi wanavyojisikia kama vile nyumba yao imeongezeka ukubwa na kuwa wanatumia eneo la bustani zaidi ya ilivoyowahi kuwa.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment