Pages

Tuesday, December 31, 2013

je unabaki nyumbani usiku huu?

kwa mawazo yangu nadhani ni vyema kubaki nyumbani usiku huu ukawa na familia yako usiku wa mwaka mpya. na sababu zangu hizi hapa:
1. huna haja ya kwenda kuliwa na mbu au kupigwa na baridi kama uko maeneo yenye kati ya vitu hivyo viwili
2. hutalazimika kulipia kinywaji kwa gharama kubwa huko kwenye mabaa kwa ajili ya usiku huu
3. unaweza kuvaa mavazi utakayojisikia burudani ukiwa nyumbani badala ya kujilazimika kuvaa kiusiku usiku kimtoko
4. kama una watoto hutakuwa na wasiwasi wa mtu wa kuwaacha nao
5. hutakuwa na risk zitokanazo na heka heka za kuupokea mwaka mpya
6. unaweka kulala kwa raha zako

kwa sababu hizi kwangu ni vizuri zaidi kuupokea mwaka mpya ukiwa nyumbani.

Happy New Year!

kama wewe ni uzao wa dot com hujatumia hii

ni nyumba chache za waTZ walioko TZ unaweza kukuta zina chumba cha kufulia. nafikiria kuandika makala ili kuzitia moyo familia changa zijenge makazi yenye chumba cha kufulia. usikose kutembelea hapa mara kwa mara ili ujue zaidi juu ya muonekano wa chumba hicho.

siku miss opportunity yoyote..

nikiwa likizo yangu ya krismasi nilihakikisha natumia kila fursa iliyojitokeza na sikutaka kumiss mwaliko wowote. hapa ni picha za mishe mishe za hapa na pale
asubuhi mimi na rafiki zangu wakweli tukienda kupiga misele ya hapa na pale. wengi wameniambia nimenenepa

 watu wangu wadogo wanaanza safari
 mchana tukaulamba kuelekea harusini

 bibi na wajukuu
 harusi ilifungwa na askofu mstaafu. mtu wangu mdogo alipata bahati ya kushikana mikono na askofu
makala yangu ya maanadalizi ya eneo la bustani inakofungwa harusi hapa inahusu. nyasi zilitakiwa kukatwa wiki mbili kabla ya harusi
maharusi walipendeza sana na kitu kilichonishangaza ni namna wanavyofanana sura

Friday, December 27, 2013

chimbo la watoto ukitembelea maeneo ya Moshi

muda wote niliokuja hapa Moshi kwa ajili ya sikukuu sikuwahi kulijua hili chimbo. leo nimeligundua na ni sehemu nzuri yenye michezo mingi ya watoto. nimebaki kufilisika kwa mizunguko ya treni!!


cute boys

abiria wakiwa ndani ya treni

Wednesday, December 25, 2013

Jinsi nilivyosheherekea Christmas yangu leo

helo wadau wangu, namshukuru Mungu siku ya leo ya Christmas mimi na familia yangu tumeweza kwenda kanisani na pia binafsi nimeweza kutembelea mahali nilipozaliwa. wewe je ulishereheka vipi?
 watu wangu wadogo wakiwa wameshaulamba kwa ajili ya kwenda kanisani

 familia
 this is where your auntie was born. nyumba hii ina miaka zaidi ya 40
nikaenda upande wa pili kutembelea shule aliyoanzisha mama yangu 
baada ya mama kwenda mbinguni 2010 dada yangu mkubwa ameendeleza sana shule. yale kule juu ni madarasa. kutokana na landscape ya eneo hili utafurahia ubunifu wa bustani zake.
 utapenda bustani, huwezi amini wanafunzi wanapita pita humu
 maua ya aina mbalimbali
 hall na vyumba vya hostel ya wasichana
front view

Saturday, December 21, 2013

Maboresho ya Nyumbani: Jinsi ya kuzuia wadudu wasiingie ndani

hata u fumigate kila siku (of course huwezi fanya hivyo) bado kuna wadudu watakaozama ndani. ni kwa kuwa kwenye milango ya nje kuna nafasi eneo la chini kwa vile haiwezekani sakafu kukaba kabisa mlango bila kuacha kinafasi. kinafasi hiki kinafanya wadudu wadogo wadogo kama vile vijongoo vyembamba kuzama ndani. sasa leo nimejitolea kukupa suluhisho ambalo ni kufunga rubber za milangoni. tizama picha hapa chini..utakapofanya na kufanikiwa kumbuka kurudi kunishukuru!
rubber yenyewe inaonekana hivi na inauzwa kwa mita



ikiwa tayari imeshafunga mlangoni. fundi anaifunga kwa ndani na inakaba kabisa sakafu
. wadudu ndani bai bai

Friday, December 20, 2013

My article for newspaper: Meza ya chakula msimu wa sikukuu


Wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka uko karibu sana na kama wengi wetu walivyozoea ni wakati wa familia kukaa pamoja kwa ukaribu zaidi kwa kipindi walau kisichozidi wiki mbili. Kwa mfano baba mama na watoto hukutana pamoja na familia za watoto wao wakubwa ambapo huwa ni pamoja na wajukuu na kama Mungu amewaweka wazazi hawa huenda na vitukuu wakawepo. Pia ndugu jamaa na marafiki hutembelea na kusheherekea sikukuu pamoja. Sasa basi kwa vile wanafamilia ndani ya nyumba wanakuwa wengi inabidi kuwa na maandalizi ya mahali pa kulia chakula. Na mahali hapo ni kwenye chumba cha chakula. Kwa maana hiyo wakati huu chumba cha kulia chakula inabidi kiwe tayari kwa ajili ya familia na wageni watakaotembelea kukaa pamoja. 

Chumba cha chakula ni mahali ambapo patatumika kwa mlo wakati huo wote wa sikukuu.
Kwa kawaida mara nyingi milo ya kila siku familia huwa sio rasmi, isipokuwa wakati wa milo ya sikukuu maalum. Hata hivyo milo na wageni inaweza kukurusha roho wewe mwenye nyumba. Kwa maana hiyo maandalizi ni hayakwepeki kipindi hiki.

Kwa kuwa chumba cha kulia chakula kilicho rasmi kinaweza kisiwe burudani kwa milo ya kawaida, watu wengi wanapamba chumba hiki kwa kuwa na muonekano rasmi pale tu wanapokuwa na eneo la pili la kulia chakula. Lakini kama una chumba kimoja cha kulia chakula ambacho unategemea kwa ajili ya milo yote miwili yaani ile rasmi na isiyo rasmi bado unaweza kufurahia dunia zote hizi mbili.

Kwanza kabisa tuangalie muonekano halisi wa chumba cha kulala. Meza na viti vya kulia chakula ndio utambulisho rasmi wa chumba cha chakula. Meza hii yaweza kuwa ya umbo la duara, yai au pembe nne. Meza za umbo la yai na duara huwa sio rasmi sana kama zile za pembe nne. Najua msomaji ya kuwa unaona shughuli zote rasmi huwa meza zinazowekwa ni za pembe nne. Meza za duara na yai zinampa kila mtu uhuru sawa, na zinawezesha mazungumzo kirahisi kwa kila mmoja mezani wakati zile za pembe nne  ni rasmi zaidi na huwa zinawaweka wakaaji katika ngazi tofauti tofauti, kama vile eneo la mwenyeji au mgeni  rasmi na kadhalika. Andaa meza ya chakula ya ukubwa ambao utatosha wageni wako.

Kitamaduni, viti vya mikono vinatumika kwenye miisho ya meza za pembe nne. Viti visivyokuwa na mikono vinaruhusu upenyaji wa kirahisi. Andaa meza yako vyema kwa kuwa na kitambaa cha meza na kama kitambaa hicho kikiwa na rangi za msimu itakuwa bora zaidi. Tukumbuke kuwa rangi za msimu huu wa sikukuu ni nyekundu, nyeupe na kijani. Vesi ndogo ya maua hata kama ni kutoka kwenye bustani yako itaongeza mvuto. Kila wakati wa mlo hakikisha kuwa mezani kuna napkin hasa zile za kipambaa – zinatumika muda wote wa tukio kwa kufuta alama za vyakula, glasi baridi, matone na mengine mengi. Hizi za kitambaa ni nzuri zaidi kuliko zile za karatasi na hata ni rafiki zaidi kwa mazingira.

Andaa kuta na sakafu za chumba hiki kwa ajili ya ujio wa familia kubwa. Paka kuta zake rangi za kuvutia zitakazoongeza hamu ya kula chakula na kutengeneza sehemu ya kukaa na kuongea. Zulia sakafuni ni upendeleo wa mtu binafsi, wengine huona kuweka zulia chuni ya meza ya chakula ni changamoto hasa kama kuna watu wadogo ambao wanaweza kuwa wanadondosha vyakula wakati wa mlo. Hata hivyo kuna aina nyingi za mazulia ambazo ni rahisi kusafishika kwa dawa zilizopo na hivyo kufanya kazi ya usafishaji iwe rahisi na zulia kuonekana jipya kila wakati.

Chanzo cha mwanga kwenye chumba cha kulia chakula huwa ni ile taa maalum ya kwenye chumba cha chakula. Hata hivyo taa hii sio lazima iwe chanzo kikuu kama sio ya kuweza kurekebisha kiasi cha mwanga kwani wakati umekaa na wageni wako waweza kuhitaji kupunguza ukali wa mwanga. Kwa hiyo kama kuna taa nyingine za mwanga hafifu basi zitumie wakati huo ili kupunguza msongo wa mwanga mkali kwenye macho na pia kujenga mandhari yenye mvuto.

Fremu za picha za ukutani  sio muhimu chumba cha kulia chakula. Zile rangi maridadi za kuta zinatengeneza mvuto wa kutosha kwenye nyumba hasa kwa kuwa kitovu kitakuwa ni wageni walioko mezani.

Mwisho kabisa weka mazingira ya burudani wakati wa milo. Watu wanataka burudani kwa hivyo hawatapendelea kukaa muda wote kwenye viti vya meza ya chakala hasa pale kwenye tumazungumzo twa hapa na pale. Wanafamilia wengine wanaweza kukaa kwenye sofa ila hii haimaanishi kutofuata utaratibu wa wakati wa mlo pamoja. Mfanye kila mmoja wa wanafamilia wako afurahie kulia sikukuu ya kipindi hiki nyumbani kwako kwa kuweka mazingira ya starehe wakati wa mlo kwa jinsi itakupendeza wewe mwenyeji wao.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Thursday, December 19, 2013

throwback thursday...various

pre wedding (send off ) of your antie..Jan 2007 huko kijiji Moshi
mtu wangu mdogo rafiki yangu ya ukweli siku ya ubatizo wake ...

curl vivi

Monday, December 16, 2013

...vitu vizuri...

dinnerware za msimu ya sikukuu..ni mwendo wa red & white hadi kwenye glass


Thursday, December 12, 2013

My article for newspaper: Uzio Sahihi



Jinsi ya kuchagua uzio sahihi wa nyumba yako kwa bajeti yako

Uzio ni moja ya sura au tuseme kipengele cha makazi ambacho kinaweza kuwa kwa ajili ya kazi na pia kwa ajili ya urembo kwa jinsi ambavyo unataka kiwe. Kutegemea na bajeti yako, ubunifu, hitaji la ulinzi na pia ladha yako binafsi kuna aina nyingi za uzio kwa ajili yako kuchagua. Hapa ni baadhi ya dondoo zangu ninazoamini zitakuwezesha kupata uzio utakaokufaa.
Kwa ujumla walau kila nyumba inawezekana kuzungushiwa uzio, iwe ni kwa ajili ya ulinzi, usalama, faragha au muonekano. Uzio ulio imara unaongeza pia thamani ya mali yako hiyo.
Ili mpango wako wa kuweka uzio ufanikiwe na bila kujutia hela yako jiulize mambo yafuatayo kabla ya kuweka uzio wako:

Jambo la kwanza kabisa jiulize ni nini nia yako ya kuweka huo uzio. Je unataka kujiweka mbali na macho ya majirani wapelelezi? Kuzuia mbwa wako wasitoroke unapowafungulia? Au ni kwa ajili tu ya kuongeza urembo wa makazi yako? Kwa hivyo kabla hujaamua kuchagua mtindo au vifaa vya kutengenezea uzio wako hakikisha umejua kuwa lengo lako la kuweka uzio ni nini. Hapana shaka kuwa wewe msomaji wangu umeshawahi na bado unaona uzio zilizowekwa zikaacha maeneo ya wazi ambayo baadaye wenyeji wameamua kuyaziba ama kwa makuti au kwa bati.

Jambo la pili la kufikiria ni utunzaji wa uzio wako. Aina ya uzio utakayochagua itasema ni gharama kiasi gani ya utunzaji wake uko tayari kuitumia. Kwa mfano uzio wa mbao unatakiwa kupakwa rangi mara kwa mara na pia mbao zinaoza baada ya wakati kwa hivyo zinahitaji maboresho ya muda mfupi mfupi. Wakati huo huo uzio za wavu (chain-link) hauna gharama kubwa kwenye utunzaji kwani nguzo zake ni za zege na zile chuma hazipati kutu lakini huenda usikupe faragha sahihi. Orodheha gharama ya vifaa mbali mbali na linganisha bajeti yako na hitaji lako ili kupata uzio sahihi.

Jambo la tatu la kuzingatia kabla ya kuweka uzion ni muundo au mtindo wa uzio wenyewe. Kwa kuwa imeonekana watu wengi wanaendeleza sehemu za nje ya nyumba zao kwa shunguli nyingi za maisha ya kila siku kwa (mfano makala iliyopita tulizungumzia watu kuwa na eneo la kukaa kwenye bustani), muonekano wa uzio umekuwa ni jambo la kuzingatia kuliko ilivyowahi kuwa. Lango kuu na taa nazo zinaboresha muonekano huu. Na kwa kupunguza gharama labla au hata kupata hewa safi unaweza ukaweka uzio wa aina fulani eneo la mbele  na aina nyingine eneo la nyuma. Kwa mfano, nimeona baadhi ya watu walioweka uzio wa gharama kubwa eneo la mbele ya nyumba na upande wa uani wakaweka uzio wa chain-link  ikishirikiana na miti ya uzio aina ya michongoma. Hii itategemea ni kwa jinsi gani uzio wako wa eneo hilo utakavyoweza kukubaliana na lengo na bajeti yako.

 Jambo la nne ni kuhusu faragha na ulinzi. Jua ni nini uzio wako utaruhusu uweze kuacha nje ya nyumba na ni  nini lazima kiingizwe ndani. Uzio unaoacha nafasi nafasi au matundu matundu hauna faragha na wala hauwezi kukulinda vya kutosha, ila unakupa starehe ya kuangalia kinachoendelea nje ya makazi yako unapokuwa umejipumzisha bustanini.

Baada ya kuweka akili sawa kwa hayo mambo manne ya kuzingatia, anza kufanya utafiti wako wa aina za uzio zilizopo. Kwa mazingira yetu ya Kitanzania zipo uzio za aina mbali mbali kama vile tofali, mbao, miti, makuti, chuma, aluminiam, wavu, bati, PVC na kadhalika. Karibia kila aina ya uzio ina faida na hasara zake linapokuja swala la bei, utunzaji, umaridadi na lengo lake. Fikia ni uzio upi ungependa kuweka na tembelea masoko si chini ya matatu ili ulinganishe gharama kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Sasa umeshafanya utafiti wako wote na uko tayari kuanza kujengea uzio wako. Jambo la mwisho lakini sio dogo ni juu ya ujirani mwema. Kabla hujaweka uzio wako cheki na majirani kuhakikisha kuwa uzio unaoamua kuweka hautaleta usumbufu kwao. Kwa mfano, uzio wa miti itayooteshwa karibia kabisa na nyumba ya jirani huenda ikaleta mgogoro. Na pia kuna uzio ule ambao vibati vinawekwa juu tuseme uzio ni wa ukuta na una marembo yake, wenye nyumba wengine wanapendelea kuweka vibati vya plastiki kwa juu ili ukuta usiloe ukaoza. Maji ya mvua kwenye hivi vibati kama yameelekezwa kumwagika kwa jirani inaweza ikaleta kero. Jua mipaka yako kwa kukumbuka kuwa uzio usiloleta kero kwa jirani unafanya ujirani mwema, kuwa jirani mzuri kwa kuweka uzio ambao hautamkera jirani yako.

Zaidi ya yote fahamu sheria za mipango miji juu ya kujenga uzio. Kwa mfano uzio wa tofali wa urefu fulani hauruhusiwi kwenye makazi.

Sio siri kuwa kuchagua uzio kwa ajili ya nyumba yako inaweza kuwa uzoefu mgumu. Kuwa na dongoo hizi kichwani, pamoja na bajeti yako na kipaumbele cha staili itakuhakikisha kuchagua uzio sahihi kwa ajili ya nyumba na familia yako.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Wednesday, December 11, 2013

picha za kumbukumbu ya kusherehekea maisha ya Mandela hapo jana

 watu waliokuwa wamefurika FNB Stadium Soweto kwa sherehe rasmi za kumbukumbu ya maisha ya Madiba hapo jana

 Rais wa Marekani Barack Obama akisalimiana na Rais wa Cuba Raul Castro
 bahari ya miavuli ya wahudhuriaji kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha


 Obama akitoa speech

wanandoa waliochukua taulo na kwenda kufuta picha ya Madiba iliyowekwa katikati ya uwanja kabla huduma ya kumbukumbu haijaanza

picha kwa hisani ya Tsvangirayi Mukwazhi

Tuesday, December 10, 2013

lime green ni mojawapo ya rangi nzuri za nyumba

watu wengi hawajui ama wanaona aibu kutumia rangi zile ambazo zinang'aa sana ama ziko bold kwenye makazi yao. na pia baadhi ya wenye nyumba sio wabunifu kiasi kwamba akishaoana fulani kapaka rangi nyeupe basi kila mmoja anaiga na hivyo kufanya mtaa mzima kuwa wa nyumba nyeupe. maadam hapa kwetu tuna uhuru wa kuchagua ni rangi gani upake nyumba yako basi ipendezeshe dunia. hapa mimi nimeamua kukumbatia lime green. rangi hii ikitumika na combination kama nyeupe itafanya nyumba yako isimame kileleni--kwa muonekano mzuri! karibu kwenye ulimwengu wa lime green!


Saturday, December 7, 2013

picha mbili tatu za msiba wa Mandela

 waombolezaji wakiwa nyumbani alikofia Mandela. kuna dada hapo kati huyo anayekutazama, anafanana na mimi..na vinywele vyake hivyo hivyo kama vyangu
Mandela enzi za uhai wake akiwa na mke wa ujana wake

Thursday, December 5, 2013

xmas ya mwaka huu imechangamka mapema...

kwa mtizamo wangu sikukuu imeshaanza kupamba moto. watu wangu wadogo nao haoooo wameshaondoka zao kula sikukuu. nyumba imepooza mno kukosa fujo zao za hapa na pale..


My article for newspaper: Sehemu ya kukaa kwenye bustani



Boresha bustani yako kwa kutengeneza eneo la kukaa

Bustani zinamaanisha kutizamwa, lakini utakuta mara nyingi zinakaa zenyewe binafsi na maua na miti yake. Bado, kukaa ni sehemu muhimu ya bustani yoyote. Bustani ni kiwakilishi cha maono ya mwenye nyumba na kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa hakuna kanuni zozote muhimu za juu ya namna ya kutengeneza eneo la kukaa la kwenye bustani.
Eneo hili linaweza kuwa la kudumu na maridadi kwa kiwango cha ubunifu wa mwenye bustani.

Benchi lililowekwa kuelekea muonekano mzuri linaweza lisitumike, lakini eneo lililojengewa vizuri likawekwa sofa au viti pamoja na runinga inaweza ikawa ngumu sana kutovutiwa kukaa mahali kama hapo.  Sehemu maalum ya kukaa iliyotengenezwa kwenye bustani inawavuta wageni kwenye bustani, wanaweza wasikae lakini kishawishi na mapenzi viko pale. Zaidi ya yote ni kama kijisehemu cha kujificha kwa ajili ya kusoma au kiusingizi cha mchana. Sehemu kubwa na yenye rangi inaweza kufanya bustani kuwa ya kukumbukwa, hasa kwa watoto.

Kwa hivyo sehemu hii ya kukaa inaweza kuwa rahisi kama viti viwili chini ya mti au kubwa kama vile eneo la kulia chakula nje ya nyumba. Sehemu hii tulivu inakuvuta wewe na wageni wako na kuwazamisha kwenye uzuri wa bustani.

Wewe mwenye nyumba kuwa mbunifu wa eneo hili la kukaa ndani ya bustani yako mwenyewe, fikiria ni wapi pa kuweka eneo hili na jinsi gani litaonekana. Fikiria ramani ya jinsi unavyowakaribisha wageni wako kwenye bustani: Njooni huku. Karibu kiti. Pumzika hapa. Kwa kufikiria maeneo mbalimbali ya bustani yako, na eneo hilo la kukaa litatumika na watu wangapi utaweza kutengeneza eneo la kukaa ambalo utalitumia kwa muda mrefu na ambalo litatumika kama muendelezo wa nje wa nyumba yako.

Kwenye kona ya ukuta wa uzio wa nyumba yako unaweza kutengeneza sehemu ya kukaa kwenye bustani. Fanya chaguzi ambazo zitaendana na eneo lako. Kwa mfano kwa maeneo makubwa, maanguko ya maji na mimea mingi inaweza kufanya eneo zuri la kukaa. Ukubwa na kiasi cha faragha kinacholetwa na eneo hili ni ishara za jinsi gani eneo litatumika. Unaweza kuliweka dogo kwa faragha au kubwa kwa shughuli za kijamii. Kuendana na ukubwa wa bustani unaweza kuwa na eneo kubwa na dogo pamoja kutokana na matumizi yako

Sasa kwenye eneo hili unatakiwa kuweka mipaka. Unaweza kufanya hivyo kwa mimea au kwa kujenga ukuta mfupi uliokaa kisanaa zaidi kwa kutumia mawe ya urembo. Kwenye paa unaweza kuweka mwavuli au hata kufunga makuti yanayowekwa kimkakati.
Sasa umeshaweka mipaka yako na paa kwa hivyo ni wakati wa kuchagua sakafu, wakati huu chagua zaidi ya muonekano tuu. Jiwe linalotumika hapa liwe na mvuto wa kiasili lakini pia lifae kwa matumizi, kuipa sakafu eneo flati na imara la kuweza kuburudika.

Wakati utakapokuwa unachagua aina ya sakafu unayotaka eneo hili iwe ni mawe ya asili, marumaru, vitofali vya kutengeneza, zege ama kokoto zingatia aina ya fenicha utakazosimamisha kwenye hiyo sakafu. Sakafu yoyote utayochagua itatokana na bajeti yako. Kwa mfano fenicha za chuma zenye miguu myembamba zinahitaji sakafu iliyojishindilia. Zingatia pia utelezi, mawe mengine kwa mfano, yanaota wale fangasi wakati wa masika na huwa wanateleza sana. Fanya uamuzi wako wa mwisho kwa kuzingatia sio tu mfumo wa maisha yako na bajeti bali pia matumizi ya vifaa katika sehemu yako hii. Sasa anza pilika za kuweka sakafu.

Mara unapomaliza kuweka paa, mipaka na sakafu ya eneo lako la kukaa kwenye bustani, unaanza kugundua kuwa inakubidi umalizie eneo hili ambapo ni pamoja na kupaka rangi, kuweka taa za urembo na mapambo mengine ya ukutani na kuweka fenicha tayari kwa kukaa. Usisahau kuweka njia ya mawe ya kukanyagia ya kukufikisha kwenye eneo lako la kukaa. Weka taa na mapambo ya rangi mbali mbali yatakayobadilisha eneo hili kutoka eneo rahisi la kukaa na kuwa eneo la kukaa lenye mvuto la nje ya nyumba yako.

Operesheni tengeneza eneo la kukaa kwenye bustani imekamilika.

Moja kati ya sifa ninazosikia wenye nyumba waliobadili sehemu ya bustani zao kutengeneza eneo la kukaa kwenye bustani wakitukuza ni jinsi wanavyojisikia kama vile nyumba yao imeongezeka ukubwa na kuwa wanatumia eneo la bustani zaidi ya ilivoyowahi kuwa.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk