Pages

Monday, February 9, 2015

Hivi ni nani mwenye dhamana ya kumzika mkewe, ni mume au ndugu?


Jeshi la polisi mkoa wa Kinondoni lalazimika kuimarisha usalama katika hospitali ya Mwananyamala, baada ya familia mbili kugombea maiti ya Saada Humudi, ili ikaizike.
Mvutano huo ulihusisha upande wa mume wa marehemu na ukeni ambao wapo waliotaka mwili huo ukazikwe Kigoma na wengine Dar es Salaam.

NIPASHE ilishuhudia juzi familia hizo zikiwa kwenye mvutano hospitalini hapo na kufikia hatua ya kurushiana maneno ambayo yalisababisha  jeshi la Polisi likiwa na silaha mbalimbali kufika eneo hilo kuimarisha ulinzi na usalama ili amani isitoweke.

Mvutano huo ambao ulianza asubuhi  ulisababisha Jeshi la polisi, ndugu wa marehemu waliokuwa wakivutana na uongozi wa hospitali hiyo kukaa pamoja ili kutafuta muafaka wa tukio hilo.

Licha ya pande hizo kukutanishwa na kikao kufanyika zaidi ya saa mbili lakini hakuna muafaka uliopatikana zaidi ya shauri hilo kuamriwa kupelekwa mahakamani.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Sophinias Ngonyani, akizungumza na NIPASHE mara baada ya kikao hicho, alisema kuwa Saada alipokelewa hospitalini hapo Januari 30, mwaka huu na alikumbwa na umauti Jumatano ya wiki hii.

Alisema baada ya dada huyo kukumbwa na umauti, ndugu hao walianza kukinzana sehemu ya kuuhifadhi mwili huo ambapo familia moja ilitaka uzikwe Kigoma huku wengine wakitaka uzikwe Dar es Salaam.

Alisema hospitali kazi yake ni kukabidhi mwili kwa ndugu na pindi hali kama hiyo inapotokea huwashauri wahusika wakubaliane na wanapofikia muafaka ndipo mwili hukabidhiwa.

“Kwa hawa imeshindikana hivyo tunaandika barua ambayo wataenda nayo mahakamani ili kutafuta suluhisho ya tatizo lililojitokeza,” alisema.

Alibainisha kuwa polisi walilazimika kufika hospitalini hapo kuimarisha ulinzi na usalama ili watumiaji wa hospitali hiyo wakiwemo wagonjwa wasipate bughuza.
     

No comments:

Post a Comment