Pages

Monday, February 9, 2015

Mabinti walioletwa nchini kutoka Nepal na India kwa ajili ya kuja kufanya biashara ya ukahaba warudishwa makwao

WASICHANA 22 walioingizwa nchini na mmiliki wa Continental Night Club na Hunters Club, Omprakash Singh kwa ajili ya kufanya biashara ya ukahaba wanarudishwa leo Nepal na India walikotoka.

Akizungumza jana na Mtanzania kwa njia ya simu, Kamishna wa Uhamiaji Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka, Abdallah Abdullah, alisema wasichana hao wanatarajia kuondoka leo baada ya kumaliza matibabu waliyokuwa wakipata.

“Wasichana waliokuwa wanaugua TB na UTI wote wamepona, tiketi zilichelewa kidogo lakini zimepatikana wanasafiri kesho (leo),”alisema.
Alisema Singh ameshalipa faini ya Sh milioni 15 alizoamuliwa kulipa na mahakama, pamoja na kulipa mishahara ya wasichana hao Dola za Marekani 30,625.

Tangu wasichana hao walipobainika walikokuwa wamefichwa, Idara ya Uhamiaji imekuwa ikiwasimamia kwa kuwapa matibabu na kufanikisha safari ya kurudi nchini mwao.

Hata hivyo idara hiyo ilifanya mawasiliano na mashirika ya kimataifa kuona jinsi watakavyowasaidia wasichana hao mara watakapofika huko.

Hivi karibuni Singh alitiwa hatiani na Serikali kutaifisha magari yake matatu baada ya kupatikana na hatia ya kuwaingiza nchini wasichana hao kutoka India na Nepal kwa ajili ya kuwafanyisha kazi ngumu ikiwamo biashara ya ngono.

Singh alitiwa hatiani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka baada ya kukiri kosa lililokuwa linamkabili la kuwaingiza nchini wasichana hao, ambapo aliwatumikisha kazi ngumu na alikuwa akiwauza kwa ngono na kujipatia fedha.

Mahakama ilimpa adhabu ya kulipa faini kila kosa Sh milioni tano hivyo kwa makosa matatu alitakiwa kulipa Sh milioni 15 na magari yake matatu yalitaifishwa na Serikali.

Pia mahakama ilimtaka kuwalipa wasichana hao 22 mishahara yao na endapo mshtakiwa angeshindwa kulipa faini angekwenda jela miaka 10.

Mshtakiwa alikuwa akiishi Mwananyamala, alikuwa Mkurugenzi wa Dhamaka Entertainment Center Limited, kampuni ambayo aliisajili Tanzania.

Inadaiwa alikuwa Tanzania mwaka 2010 kwa nia ya kuanzisha dancing club. Mwaka 2011 alifungua Night Club Kinondoni, TX Market inayoitwa Hunters Club.

Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila alidai baada ya miezi michache alifungua club nyingine maeneo ya clock tower, barabara ya Nkrumah inayoitwa Continental Night Club na zote mbili ziko chini ya Kampuni ya Dhamaka na ziliajiri madansa kutoka India na Nepal.

Mwangamila alidai madansa hao walisafirishwa na mshtakiwa kutoka kwao kuingia nchini, aliwakatia viza, kibali cha kufanya kazi nchini, mahali pa kulala, chakula na mahitaji mengine.

Ilidaiwa kuwa kati ya Mei na Desemba mwaka jana mshtakiwa alipokea madansa 21 kutoka Nepal na dansa mmoja kutoka India, walipofika mshtakiwa alichukua hati zao za kusafiria, simu zao na kuwalazimisha kujiingiza kufanya ngono kisha yeye akusanye fedha huku akiwafanya hao wasichana ni sehemu ya biashara yake.

Idara ya Uhamiaji ilipata taarifa za mshtakiwa, Desemba 19 mwaka jana walikwenda alikokuwa akiishi nyumba namba 531, Block 9 inayomilikiwa na Thuraya Mohammed Abdullah na kuwakuta wasichana hao 22.

Maofisa wa uhamiaji walifanya upekuzi katika chumba cha mshtakiwa na kukuta hati za kusafiria 22 na simu 27 ambazo ni za wasichana hao.
‘’Uchunguzi ulibaini kwamba mshtakiwa alikubaliana na wasichana hao kuwalipa kila mwezi ujira kati ya Dola za Marekani 500 mpaka 1000 lakini aliwalazimisha kusaini mkataba wa ujira unaoonesha kwamba atawalipa kila mwezi Dola za Marekani 200 mpaka 500,”anadai Mwangamila.

Alidai uchunguzi ulibaini kwamba wakati tofauti mshtakiwa alikuwa akiwatoa wsichana hao kutoka nyumba waliyokuwa wakiishi Mwananyamala na kuwapeleka Hunters na Continental na mahali kwingine kwa nia ya kuwafanyisha kazi kwa nguvu na ngono.

Mshtakiwa katika safari hizo alikuwa akitumia gari lenye namba za usajili T540 CBN aina ya RAV4, namba T111CCS Toyota Vox Noah na Toyota Hiace namba T111CRZ.

No comments:

Post a Comment