Pages

Saturday, February 7, 2015

Mara nyingi mchepukaji hachezi mbali.

Mchepukaji awe ni mwanamume au mwanamke kwa asilimia kubwa atachepuka na mtu aliyeko karibu naye, iwe ni mahali anapofanyia kazi ama anapoishi. Abiria chunga mzigo wako..

Soma kisa hiki cha "Happy" kama kilivyo katika gazeti la mwananchi:


Happy: Kahaba ‘aliyeua’ baba mwenye nyumba na kuathiri mtoto
“Hakuna mtu anayependa kuwa kahaba (kujiuza) ila inatokana na sababu maalumu zinazomkabili mhusika,” anasema Happy katika mahojiano na gazeti hili jijini Dar es Salaam.
Happy (siyo jina lake halisi), msichana mweusi, mrefu wa wastani, mwenyeji wa Mkoa wa Arusha aliye na diploma ya uhazili anasema kwamba alizaliwa miaka 22 iliyopita katika familia yenye watoto watatu, yeye pekee akiwa wa kike, huku akiwa pia wa kwanza kwenye familia yao. Anataja kabila lake kuwa ni Mmasai na kwamba anaishi jijini Dar es Salaam, maeneo ya Sinza Kumekucha.

Anabainisha kuwa hana mtoto na wala hana sababu ya kuwa na mtoto kutokana na matatizo yanayomkabili.
Happy ambaye shughuli zake za kujipatia kipato ni ukahaba katika eneo la Buguruni, anaanza kusimulia historia yake ya kusisimua  akisema:
“Nilikuwa mwajiriwa katika benki  moja jijini Dar es Salaam. Katika kuajiriwa kwangu nikawa msaidizi maalumu wa bosi (sekretari) wa benki hiyo, lakini siku nyingine ilitokea mimi na bosi wangu tukaamua kujirusha kama mtu wangu wa karibu.”

“Kaka, unajua kwanza sijawahi kuwa na mume wala mchumba na kwa kweli huyo bosi ndiye alikuwa mtu wa kwanza kufanya naye mapenzi, hivyo nilifurahia penzi lake na alitokea kunipenda kwa dhati na kunijali. Kila kitu nilipata kutoka kwake.”

Anabainisha kuwa aliampenda  bosi wake kwa sababu hakumficha kitu kuhusu maisha yake, kwani alimwambia wazi kuwa pamoja na kumpenda, ana mke na watoto, hivyo jambo lolote linaweza kutokea ikiwa mke wake atajua kinachoendelea.

Anasema kuwa taarifa hiyo alitegemea kuipata kutokana na ukweli kwamba kwa umri aliokuwa nao bosi huyo ni dhahiri kwamba alitakiwa kuwa na familia, hata wajukuu.
“Tulikuwa na uhusiano na huyo bosi kwa miezi zaidi ya minne, lakini siku moja katika tembeatembea yangu mitaani, nilikutana na kijana mmoja mtanashati, akanieleza kwamba ananipenda na kunihitaji,” anasema Happy.

“Kijana huyo hakukata tamaa,   alihangaika kwa mwezi mzima akinifuatilia, mpaka siku nikamkubalia, ndipo akawa mpenzi wangu halali. Nilimwamini sana na mwezi mmoja tu tangu tulipojuana, kijana aliniambia tufanye naye mapenzi.”

Happy anasimulia: “Nilifikiria sana suala hilo na wakati mwingine nilitaka kulia jinsi alivyokuwa ananishika na kuniomba tufanye mapenzi akiwa chumbani kwangu wakati mimi sikuwa radhi. Alijaribu kunishawishi lakini nilimkatalia.”

Anasema kuwa siku moja alimwomba kijana huyo wakapime  afya ili kujua kama wana maambukizi ya magonjwa ya zinaa  au sivyo kabla ya ya kuanza kufanya ngono.
“Kijana yule alikasirika sana wiki nzima na hakufika nyumbani kwangu. Mawasiliano yalikatika kwani hakunipigia simu, kumbe alitaka tufanye tendo la ndoa bila kinga,” anasema.

Anabainisha: “Maisha yaliendelea na mambo mengine yaliendelea bila mawasiliano, lakini wiki ya tatu yule kijana alinipigia simu, akaniomba msamaha akitaka turudiane na alikubali kwenda kupata vipimo vya afya zetu kujua kwanza kabla hatujaanza mambo mengine yoyote.”

Anasema kuwa majibu yalikuwa mazuri na ndipo walianza kuwa wapenzi.
“Alinifurahia hata akawa anatoroka nyumbani kwao, kuja kulala kwangu wakati mwingine mwezi mzima,” anaeleza na kuongeza:
“Mapenzi yangu na kijana yule yalishamiri na wakati huo bado nilikuwa na bosi wangu kule kazini. 

Tuliendelea kwa miezi kadhaa na huyu kijana, huku nami nikiwa na bosi wangu kule kazini.”
Happy anasimulia kwamba siku moja akiwa na rafiki yake waliamua kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kupima afya zao:
“Kwa kweli majibu hayakuwa mazuri kwa upande wangu. Nilistuka sana kwani sikutarajia kupata majibu hayo na kuamua kwenda hospitali nyingine, lakini pia majibu yalikuwa yale yale kwamba nimeathirika na Ukimwi.”

Anasema kuwa hajui kilichotokea, lakini majibu hayo yalimfikia pia bosi wake ambaye alisikitika kwa yaliyonipata na kwa sababu hiyo naye alikwenda kupima ili kujua hali ya afya yake kwa kuwa alikuwa pia na familia.

“Majibu yalivyokuja akakutwa salama, hajaathirika. Hapo  nikajua moja kwa moja kwamba Ukimwi nimeupata kutoka kwa yule kijana wa mitaani na siyo mtu mwingine,” Happy anasimulia akisikitika.
“Niliamua kupeleleza na ukweli niliupata kwamba kumbe yule kijana alikuwa anatembea na mama mmoja ambaye tayari alishaathirika na kufariki dunia muda mrefu.”

Kufukuzwa kazi
Kama Waswahili wasemavyo; baada ya kisa mkasa, Happy alifukuzwa kazi, huku upande wa pili yule kijana naye akifariki dunia
“Kwa kweli hapo ndipo maisha yakaanza kuwa magumu kwani kijana mwenyewe aliniacha peke yangu nikihangaika. Nikawa sina namna ya kumudu maisha. Nikaamua kujiuza ili maisha yaendelee,” anasimulia.

‘Kuua’ baba na mtoto
Happy anayevutia kwa kumtazama anaeleza kuwa mbali ya kujiuza awali, aliona maisha magumu kwani hakuwa amezoea kazi hiyo lakini alilazimika kutokana na kupata ugumu wa kumudu maisha hata kodi ya nyumba.

“Niliamua kutembea na baba mwenye nyumba wangu ambaye alikuwa akinitaka kwa muda mrefu. Kilichosababisha nitembee naye ni kumlaghai ili nisilipe kodi, jambo ambalo nilifanikiwa,” Happy anasimulia.

Hata hivyo anasema: “Baba mwenye nyumba alipata Ukimwi akafariki dunia na baada ya kifo cha mzee nilitembea na mtoto wake ambaye yupo hai mpaka leo na bado ni rafiki yangu.”

Anasema baada ya kuona maisha ni magumu na hana lolote, aliamua kutafuta njia rahisi zaidi ya kujipatia kipato ambazo zingempatia angalau mlo na mavazi baada ya kugundulika kuwa na virusi vya Ukimwi.

Happy anasema kuwa akaanza kutafuta madanguro na sehemu rahisi ambazo anaweza kuuza mwili wake kwa fedha za haraka haraka aweze kuendeleza maisha yake ya kila siku.
“Niliamua kujichanganya na wenzangu kule kwenye mitaa ya Bills, Kwa Macheni na Ohio. Awali, nilishindwa kabisa kufanya kazi hiyo nzito, nilianza kwa kuvaa miwani ili watu wanaonifahamu wasinigundue, lakini ugumu uliongezeka zaidi baada ya kuona wenzangu wakiweka viungo vyao wazi.

Nilianza kwa kuweka mapaja  wazi ili watakaovutiwa wanichukue jambo ambalo nilifanikiwa  na nilikuwa nikiondoka na pesa nyingi. Kwa siku zaidi ya Sh50,000.”

Hata hivyo, anasema kuwa baadhi ya watu huamua kuwakomoa makahaba kwa kuwalazimisha kufanya mapenzi kinyume na maumbile jambo analosema lilinifanya ahame mitaa ya mjini na kwenda Buguruni ambako ameshapazoea.

“Pamoja na kwamba pesa ya hapa siyo nzuri kama mitaa ya mjini, lakini ni wanaume wachache wanaotaka kufanya mapenzi kinyume na maumbile, hapa mnakubaliana tu wenyewe,” anasema.

Maisha ya makahaba
 Akizungumzia maisha ya makahaba Happy anasema wapo wa aina tofauti kutegemea sababu zilizowasukuma kufanya biashara hiyo ya ngono.
“Kwa kweli kaka siyo makahaba wote ni maskini, wengine wanapenda kufanya ukahaba, yaani  hao wamechoka na dunia, lakini wengine walikuwa na wanaume wao wakaachika ndipo wakaamua kuja huku ili wafanye ngono na mwanaume yeyote anayekuja.

“Wengine wana matatizo katika ndoa zao, kupigwa na kadhalika ndipo wanaamua kuja huku kujiuza, au kukaa huku ili kuepuka matatizo katika ndoa zao au uhusiano wao.
“Wengine ndiyo kama hivyo, waume zao hawana nguvu za kutosha  za kiume kufanya nao tendo la ndoa nao wanaamua kuwa makahaba, Hapa kila mtu na lake na mambo yake pia,” Happy anafafanua.

Idadi ya aliofanya nao ngono
Happy anasema kazi anayofanya imeamsaidia na kwamba kwa miaka miwili aliyoifanya, hakuna aliyejua kama ameathirika kwa Ukimwi huku akipata wateja wengi.

“Nilikuwa najitunza na kutunza siri zangu hizi na sikupenda kuzoeana na watu,” anasema.
Kuhusu idadi Happy anasema: “Siwezi kuhesabu ni watu wangapi nimefanya nao ngono, lakini ni zaidi ya 300. Siku nyingine nafanya kazi na watu zaidi ya watatu kwa wakati. Mambo yanaendelea, lakini wengi hawapendi kutumia kondomu.”

Hata hivyo, Happy anayeonekana kuridhika na kazi anayoifanya anasema: “Kwa kweli sifurahii nilivyo, bali ni kutokana na hali ya maisha inayonikabili kaka. Siyo kila mtu anayejiuza anapenda, ana sababu zake binafsi.”

Akimkumbuka aliyekuwa bosi wake Happy anasema akitubu: “Mpaka sasa sijajua anaendeleaje na maisha au vipi, lakini kinachonisikitisha zaidi ni kuhusu familia yake. Nahisi niliikosea sana, naomba Mungu anisamehe kwa hilo.”

Mwanasaikolijia
Mwanasaikolojia Modester Kimonga  amesema tatizo lililomkumba Happy  linawakumba wasichana wengi ikisababishwa na hulka wanayozaliwa nayo.
Anasema wasichana wengi wanaojiuza huwa na matatizo kama hayo na tiba yake ni kupatiwa msaada wa kitaalamu na wala si kuwatupia lawama.


‘’Inasikitisha kwani wengi wana pesa zao na wanatoka katika familia bora, lakini wanazaliwa na tatizo la kuwa na tamaa ya ngono yaani hawaridhiki na mwanamume mmoja,’’ anasema Kimonga.

No comments:

Post a Comment