Pages

Friday, February 6, 2015

Wananchi wamuua aliyetoroka baada ya kumuua polisi aliyekuwa anaokoa mtoto asiuawe


MTUHUMIWA Tissi Mallya ambaye alitoroka baada ya kumuua polisi, G.7168 Koplo Joseph Swai, ameauwa usiku wa kuamkia jana na wananchi alipokuwa amejificha akiwa na panga lenye damu lililotumika kwenye mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David 
Misime alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Mauaji hayo yalitokea juzi asubuhi katika eneo la Chang’ombe Juu.
Kamanda Misime alisema baada ya Malya kutekeleza mauaji hayo alikimbia lakini ilipofika saa 5.00 usiku wananchi walimuona maeneo ya Mtimkavu Mailimbili akiwa bado na panga alilotumia kumuua Koplo Joseph.

“Wananchi walichukua sheria mkononi na kumshambulia hadi polisi walipofika eneo la tukio wakamchukua na kumkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma lakini aligundulika tayari amekwisha kufariki dunia,” alisema.
Kamanda Misime alisema katika kumbukumbu zilizopo, mwaka 2006 Mallya aliwahi kufungwa miaka mitatu kwa kujeruhi, pia mwaka 2009 alifungwa miezi sita kwa kutishia kuua.

Nawapongeza wananchi walioonyesha kuchukizwa na kitendo alichotendewa askari wetu lakini waache kujichukulia sheria mkononi,” alisema.
Pia alitoa wito kwa wananchi kuchukua hatua kurekebisha maadili kuanzia ngazi ya familia kwa sababu imebainika mtuhumiwa alikuwa mvuta bangi kiasi kwamba alikuwa anafanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii.

Diwani wa Kata ya Mnadani, Steven Masangia, alisema alimfahamu polisi aliyeuawa kama kijana mchapakazi ambaye alijitolea kutoa elimu hata kwenye mitaa juu ya ulinzi shirikishi.
“Alipokuwaa Mnadani alipambana kuhakikisha uhalifu unakomeshwa na hata vijana wanaovuta bangi aliwasambaratisha, na alikuwa akifundisha polisi jamii kwenye mitaa ya kata,” alisema na kuongeza:

“Alikuwa na cheo kidogo lakini kazi alizokuwa akifanya zilikuwa ni kubwa ikilinganishwa na cheo na umri wake” alisema .

Katika mkasa huo uliotokea juzi asubuhi, askari huyo aliitikia wito wa kuwapo kwa dalili za tendo la jinai nyumbani kwa mkazi mmoja wa Chang’ombe Juu.

Alipofika nyumbani kwa mkazi huyo ndipo mkasa huo ulipomtokea alipotaka kumuokoa mtoto mchanga ambaye alikuwa auawe na baba yake kwa panga.

No comments:

Post a Comment