Pages

Monday, February 2, 2015

--NITAVUKAJE-- Jinsi ya kufahamu biashara ya kufanya

Wapenzi, nimekutana na makala hii ambapo inajibu dukuduku la wengi la kuwa ni biashara gani wafanye. Naamini ukiisoma japo ni ndefu na nimejitahiji kuipunguza kwa kukuchujia kile cream hutatoka patupu.

Imeandikwa na Makirita Amani
Biashara moja inaweza kuwa nzuri kwa watu wengine ila ikawa mbaya sana kwako. Unaweza kuona watu wanapata faida kwenye biashara fulani ila ukaingia wewe na ukapata hasara kubwa sana.
Hivyo kujua ni biashara gani ufanye ni kitu ambacho unatakiwa kukifikiria kwa kina na sio kuiga au kuamua tu kufanya chochote.
Katika makala hii ya leo tutaangalia vitu viwili, jinsi ya kujua biashara ambayo itakulipa na jinsi ya kupata wazo bora la biashara.
1. Ni biashara gani inaweza kukulipa?
Jibu la swali hili haliwezi kuwa sawa kwa watu wote, linategemea na mtu na ili kuweza kupata jibu la swali lako wewe mwenyewe unatakiwa kujiuliza na kujipa majibu sahihi maswali haya matatu;
a)   Ni kitu gani unapendelea kufanya?
Katika maisha yako kuna vitu fulani ambavyo unavipenda sana au unapendelea kufanya. Inawezekana unapenda mitindo, inawezekana unapenda michezo, inawezekana unapenda magari au kusafiri na kadhalika. Kwa kuangalia mambo haya unayopenda sana kufanya unaweza kufikiria ni jinsi gani unaweza kuyageuza kuwa biashara. Kwa mfano kama unapenda sana kusafiri unaweza kuanzisha biashara ya usafirishaji. Kama unapenda sana mifugo au wanyama unaweza kuanzisha biashara ya ufugaji. Ni vizuri sana kufanya biashara unayoipenda kwa sababu utakuwa na shauku ya kujifunza zaidi na hutokata tamaa mapema hasa mambo yanapokuwa magumu.
b)  Una uzoefu au taaluma gani?
Swali hili ni muhimu na litakuwezesha kujua kitu ambacho unaweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kumbuka ili kufikia mafanikio kwenye jambo lolote ni lazima uweze kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kama kuna kitu ambacho umekisomea na una taaluma nacho ni dhahiri kwamba kuna mambo mengi sana ambayo unayajua kuhusu kitu hicho. Na kama una uzoefu wa kitu au jambo fulani ni rahisi kwako kufikia mafanikio kwenye kulifanya kuliko anayeanzia mwanzo kabisa. Hivyo fikiria ni vitu gani umevipata kupitia taaluma yako na angalia ni jinsi gani unaweza kuvitumia kwenye ujasiriamali na biashara. Pia jiulize ni uzoefu gani ambao tayari unao na jinsi gani unaweza kuutumia kwenye biashara unayoweza kuanzisha. Kwa mfano kama umeajiriwa kwenye kampuni ya wanasheria hii ina maana kwamba tayari wewe una taaluma ya sheria na pia una uzoefu wa kuendesha kesi, kutafuta wateja na hata uendeshaji wa kampuni. Unaweza kutumia taaluma yako hii na uzoefu ulioupata kwenye kampuni uliyofanyia kazi na kwenda kuanzisha kampuni yako mwenyewe ambayo itakupatia mafanikio makubwa sana kama ukiweza kuisimamia na kuiendesha vizuri.
c)   Ni kitu gani ambacho kina uhitaji mkubwa.
Swali la tatu na muhimu kujiuliza ni kitu gani ambacho kina uhitaji mkubwa kwa eneo ambalo unafikiri kufanyia biashara. Angali ni kitu gani ambacho tayari kina soko au unaweza kukitengenezea uhitaji ili uweze kupata wateja pale utakapoanzisha biashara yako. Pia angalia ni jinsi gani unaweza kulifikia soko hilo kulingana na bidhaa au huduma ambayo unatarajia kuitoa.
Kama ukiweza kujiuliza na kujipa majibu sahihi kwenye maswali hayo matatu utapata aina nzuri ya biashara ambayo utaifanya kwa moyo na utaweza kufikia mafanikio makubwa. Njia nzuri ya kufanya hivi ni wewe kuchukua kalamu na karatasi kisha kuorodhesha vitu vyote vinavyohusiana na maswali hayo matatu na kisha kuoanisha na kuona ni kitu gani ambacho kinaweza kuingia kwenye sehemu zaidi ya moja.
Usichukue ushauri wa biashara kwa sababu tu kwamba watu wengi wanafanya au inaonekana kulipa. Ni muhimu biashara utakayokwenda kufanya iwe inatoka ndani yako kweli ndio utaweza kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara hiyo.
2. Njia ya kupata wazo bora la biashara.
Mara nyingi watu wamekuwa wakiniuliza ni biashara gani inalipa ambayo wanaweza kufanya na wakapata mafanikio. Jibu langu ni kwamba kila biashara inalipa, ndio maana kuna biashara mbalimbali zinazofanyika kila kona na watu wanapata faida. Ili biashara iweze kufanikiwa na upate faida ni lazima upende biashara unayofanya na uwe na ubunifu wa kutosha.
Hata baada ya kujua biashara itakayokulipa ni ile unayopenda kufanya bado kuna changamoto ya kuja na wazo zuri la biashara. Nina hakika umewahi kuwa na fedha kidogo na kutamani kuiweka kwenye biashara ila ukashindwa kujua ufanye biashara gani. Changamoto kubwa za biashara zinatokana na kosa moja kubwa ambalo wajasiriamali na wafanyabiashara wengi wanalifanya. Tatizo hili ni kuiga vitu vinavyofanywa na wengine bila ya kujua vinafanyaje kazi kwao.

Hapa nitazungumzia jinsi ya kuja na wazo la biashara ambapo watu watakukimbilia kukupa fedha. Kwa kutumia njia hizi ninazoshauri utaweza kutengeneza biashara yenye thamani na itakayodumu na hutokuwa na haja ya kuiga kila kitu kutoka kwa wengine.
Jua tatizo linalosumbua watu na tafuta njia ya kulitatua.
Biashara zote kubwa duniani zimejengwa kwenye msingi mmoja tu, kutatua matatizo yanayosumbua watu. Watu walikuwa na tatizo la kushindwa kuwasiliana na wenzao wa mbali ndipo biashara za mawasiliano na usafiri zikaanzishwa na kukua kwa kasi.
Kama umewahi kuumwa au kuwa na mgonjwa utakuwa unaelewa vizuri kwamba hata kama mtu ana shida ya fedha kiasi gani linapokuja tatizo la afya atatafuta kila njia ili aweze kulitatua. Hivyo hata watu wawe na shida ya fedha kiasi gani wako tayari kulipia kitu ambacho kitawaondolea tatizo linalowasumbua. Hapa ndipo penye wazo kubwa la biashara.
Kwa kuwa inabidi ufanye biashara ambayo unaipenda na kwa kuwa unahitaji ubunifu ili biashara yako iweze kukua fikiria wazo lako la biashara kutokana na matatizo ya watu. Angalia vitu ambavyo unapenda kufanya kutokana na vipaji vyako. Pia angalia ujuzi ambao unao na elimu uliyopata kwenye kada fulani. Kisha angalia ni matatizo gani watu wanayapata na unaweza kuyatatua. Jinsi ambavyo tatizo ni kubwa ndivyo thamani ya biashara inavyozidi kuwa kubwa. Kwa njia yoyote ile kuna bidhaa au huduma unaweza kuitoa na ikatatua matatizo ya watu.
Wakati mwingine watu hawajui tatizo mpaka waone suluhisho.
Sio kila mara watu watakuwa wanajua matatizo yao, kuna wakati mwingine watu wanakuwa hawajui kama wana tatizo mpaka waone kuna njia rahisi ya kufanya mambo, hii inaitwa ujinga wa soko.
  Hivyo kama wewe unaona kuna njia bora ya kuboresha maisha ya watu tengeneza biashara yako na washawishi watu. Kama wakitumia na kuona ina faida kwao watakuwa wateja wako na watawaambia wengine pia. Hivi ndivyo mitandao ya kijamii kama facebook na twitter ilivyoteka soko. Mwanzo hakuna mtu alidhani kuna uhitaji mkubwa wa mitandao ya aina hii, kabla ya kuanza kwa facebook sikuwahi kuona watu wakilalamika kwamba wanahitaji facebook. Ila baada ya mitandao hii kuwepo na watu wakaanza kuitumia imewawia vigumu kuacha kuitumia. Kila siku tunashuhudia ni jinsi idadi ya watumiaji wa mitandao hii inavyoongezeka.



No comments:

Post a Comment