Pages

Monday, February 9, 2015

Umewahi kusikia mwigizaji Aunt Ezekiel akihusishwa na uhusiano na Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu?


Basi mwigizaji huyo amefunguka na kuwajia juu wale wote wanaomchafua na kudai kuwa hakuna kama baba wa mtoto wake Mose Iyobo.
Aunt Ezekiel alisema maneno hayo ya kumhusisha na kiongozi huyo, hayafahamu yalipotokea na kwamba hata yeye anayasoma kwenye magazeti. Hivyo anataka watu wafahamu yeye na Iyobo ni wa kufa na kuzikana. “Achana na habari za kusikia kumhusu kiongozi huyo jamani baba wa mtoto wangu ajaye ni Iyobo,” alianza kwa kulalama.

Mwigizaji huyo mahiri alienda mbali zaidi na kuwapiga mkwara watu wote wanaotumia jina lake kuchafuana kisiasa na kuongeza kuwa kama wamejipanga hayo basi ni bora wakafanya mambo yao bila kumwingiza yeye.

“Naona kama kuna kitu nyuma ya pazia, kwa kuwa nimesikia hadi bungeni imezungumziwa. Ni kitu cha ajabu na aibu mtu amechaguliwa na wananchi kujadili masuala yao, anajadili mambo ya Aunt!

Akizungumza na Mwananchi, huku akionyesha kukerwa na uzushi huo alisema kuwa, watu wanatumia kukutana kwake na kiongozi huyo nje ya nchi kama fimbo ya kumchapia katika wakati huu wa mambo ya siasa ambao kila mtu anajisafisha kupitia jina la mwingine.

Aunt Ezekiel alieleza kuwa akiwa Marekani kwenye shughuli zake binafsi, alikwa kwenye tafrija na ndipo alipokutana na waziri huyo kama ambavyo angeweza kukutana na mtu mwingine yeyote, lakini anachoshangaa kilichotokea kuanzia hapo hadi mada ikabadilishwa na kuelezwa kuwa walikuwa na uhusiano.

“Ninachofahamu siyo kila unayekutana naye nje ya nchi ni mpenzi wako au unatembea naye. Hili suala linanikera sana kwa sababu linatengeneza kitu ambacho hakipo na wala hakifikiriwi kutokea,” alisisitiza Aunt Ezekiel, huku uso ukionyesha wazi kuchukizwa na kitendo hicho.

“Wazungu wana msemo wao usemao, ‘kama hujafanya utafiti huna haki ya kusema’, kwa jinsi alivyojiamini bungeni ina maana alikuwa na uhakika? Mimi namshauri aje na ushahidi ... Bila kufahamu kuna matatizo gani anayasababisha kwa wahusika.”
Kwa mujibu wa Aunt, baba halali wa huyu mtoto ni Mose Iyobo na kwamba anampenda kwa dhati na kumjali na kwamba hajawahi kupenda kama anavyompenda mwanaume huyo hivyo anahitaji kuheshimiwa mambo yake.


“Nina uhusiano wangu pia Waziri ana mke na familia yake suala hili linamwathiri kama ambavyo linaniathiri mimi, sitaki kujadiliwa kwa mambo ya kinafiki. Mimi ni msanii lakini hiyo siyo bendera ya kuwa kila ninayekutana naye tuna uhusiano, huko ni kunivunjiana heshima na kunidhalilisha,” alisema Aunt Ezekiel.

No comments:

Post a Comment