Pages

Friday, March 20, 2015

KINANA AWAAGIZA WALIOWEKEWA X KWENYE NYUMBA ZAO BILA KULIPWA FIDIA WAZIFUTE.....AMESEMA INAWAFANYA WANANCHI KUKAA NA HOFU MUDA WOTE

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amewataka wananchi waliowekewa alama ya `X' katika nyumba zao kwa muda mrefu bila kulipwa fidia kuzifuta hadi serikali itakapowalipa stahiki zao. 

Kinana alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Ngaramtoni Jimbo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Wananchi wanakaa na hofu kwa muda wote wakati serikali haiwalipi haki zao wala kuwapelekea maendeleo na matokeo yake wanaishia kudhulumiwa,” alisema Kinana.
Alisema serikali ikitaka kutengeneza barabara kwanza itafute fedha, kama fedha hakuna basi waondoe alama za `X' walizoweka kwenye nyumba za wananchi.
“Haya mambo ya upembuzi yakinifu, mchakato na tupo mbioni kuleta fedha...ni mazingaombwe ambayo sasa yafikie mwisho. Mimi nasema kawekeni chokaa mpaka mtakapolipwa fedha zenu na wakija waambieni tangu miaka mitatu iliyopita gharama za ujenzi zimeongezeka wawaongeze kidogo,” alisema Kinana.
Alisema haiwezekani mchakato wa kujenga barabara ukae kwa zaidi ya miaka mitatu.
Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema vyama vya upinzani vimeonyesha dalili ya kufa kutokana na kukumbatia vurugu na kuwataka wananchi kuingia mitaani hata kwa mambo yasiyo na maana.
"Mfano nchi mbili za Libya na Misri, wapinzani waliwahadaa vijana waingie mitaani kwa ahadi ya maisha bora, lakini kinachotokea sasa hivi katika nchi hizo ni kinyume chake,” alisema Nape.
Alisema nguvu ya umma hailengi kuipasua nchi, bali ni nguvu ya shetani na kuwataka vijana wasikubali kutumiwa vibaya na viongozi hawa kwa sababu wanawashawishi kufanya vurugu.
“Mkishaanza kupigwa wanawakimbia, hata ukiangalia katika orodha ya waliouawa au kuumizwa majina ya familia zao hayapo,” alisema Nape.
Aliwatahadharisha wananchi wa Arusha kuwa wakati wa vurugu za uchaguzi mkuu mwaka 2007 nchini Kenya, wananchi wengi walipoteza maisha, lakini baadaye viongozi wa vurugu hizo waligawana madaraka wakaishia kufaidi na familia zao.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Arusha, Onesmo Nangole, alisema ziara ya Kinana inarudisha imani ya wanachama kwa chama hicho kupitia ziara hizo.
“Nakupongeza Katibu Mkuu, endelea kuibana serikali kwa sababu viongozi wamejisahau, kero ni nyingi zinahitaji ufumbuzi wa haraka. Vile vile ndani ya Chama kulikuwa na vurugu viongozi wa juu katika mikoa hawakuelewana ndiyo maana katika baadhi ya chaguzi tulianguka, lakini yote yamezikwa kutokana na ziara zako,” alisema Nangole.
Chanzo Nipashe

No comments:

Post a Comment