Pages

Monday, March 2, 2015

Mtoto wa miaka 10 aliyeozwa kwa siri, muoaji adanganya majirani ni ndugu huku wakiishi wawili tu kwenye nyumba, wazazi wa binti kufikishwa mahakamani

WAZAZI wa mtoto mwenye umri wa miaka 10 aliyeozwa kwa siri wilayani Bahi, katika Mkoa wa Dodoma, wanafikishwa mahakamani leo kujibu mashitaka yanayowakabili.

Mtoto huyo aliokolewa kutoka kwenye ndoa aliyokuwa amelipiwa mahari ya mbuzi 12 na Sh 100,000.

Kijana, Joshua Mnamba (25) aliyekuwa amemuoa, inadaiwa alifikishwa mahakamani Februari 24, mwaka huu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alithibitisha wazazi wa mtoto huyo ambao walikuwa wakishikiliwa na polisi, Stephano Mkuta (baba) na Juliana Gideon (mama), wanafikishwa mahakamani leo kujibu mashitaka ya kuozesha mtoto.

Inadaiwa mtoto huyo aliozwa kwa shinikizo la mama na bibi yake kabla ya kuokolewa kutoka kwenye ndoa hiyo na kuishi nyumbani kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Bety Mkwasa.

Taarifa kutoka kwa majirani zinadai, kijana aliyemuoa mtoto huyo, awali, alikuwa akidai binti huyo ni ndugu yake.

Hata hivyo, ilidaiwa majirani wa kijana huyo, katika kijiji cha Ibihwa, walitilia shaka kutokana na vilio vya mtoto huyo nyakati za usiku ambaye amedumu kwa mwanaume huyo kwa wiki mbili kabla ya kuokolewa.

Polisi wilayani Bahi imekiri kupokea taarifa za tukio hilo kwa mara ya kwanza Februari 9, mwaka huu na kuanza upelelezi na hatimaye kuwatia mbaroni watuhumiwa wote.

Majirani na nyumba alimokuwa akiishi mtuhumiwa (mume) waliliambia gazeti hili kwamba, walikuwa wakihoji binti huyo ni nani lakini wakijibiwa kwamba ni ndugu yake.

“Cha kushangaza walikuwa wakiishi peke yao kama mume na mke,” alisema mmoja wa majirani.

Akizungumza na Habari Leo akiwa nyumbani kwa Mkwasa ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, mtoto huyo alisema hajui kusoma wala kuandika kwani wazazi wake hawakumpeleka shule na alikuwa akikaa nyumbani kulea wadogo zake.

“Sijapelekwa shuleni…nina wadogo zangu sita, mimi ndio mkubwa na wazazi wangu na bibi ndio walikuwa wakitaka niolewe lakini nilikuwa nikikataa… mimi ni mdogo,” alisema.

Alisema alikuwa akiishi na wazazi wake eneo la Bahi Sokoni na baada ya kuolewa, alipelekwa Ibihwa kwa mumewe.

“Baba, mama na bibi walisema nenda ukaolewe, niliondoka lakini nguo niliziacha kwa mama nikakuta Mnamba anaishi peke yake tukawa tunaishi wote na tunalala pamoja” alisema na kusisitiza, “Nilikuwa sipendi kuolewa lakini walinilazimisha.”

Mtoto huyo alisema kwenye fedha za mahari ambazo zilitolewa, bibi yake alipewa Sh 10,000. Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mkwasa alisema tatizo la ndoa za utotoni katika wilaya hiyo ni kubwa.

No comments:

Post a Comment