Pages

Thursday, March 12, 2015

NAPE: MPUUZENI SLAA NI MWONGO...NI KUTOKANA NA MADAI YA KUWEPO NJAMA ZA KUTAKA KUMUUA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaomba Watanzania kumpuuza Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa kwa madai aliyoyatoa ya kuwepo kwa njama za kutaka kuuawa na viongozi wa juu wa CCM kwa vile
madai hayo ni ya uongo.

CCM imetoa rai hiyo kwa Watanzania huku ikisema hatua yake hiyo haijalenga kuingilia utaratibu na sheria kwa vyombo vya serikali kufuatilia madai hayo iliyoyaita ni ya uongo na ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ilisema tuhuma zilizotolewa na Dk Slaa kupitia kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Mabere Marando ni za kipuuzi, lakini pia ni za uongo.

“Machi 8, mwaka huu, Dk Slaa, Katibu Mkuu wa Chadema kupitia kwa Marando alitoa tuhuma kwa Serikali na kuwahusisha baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kuwa wanapanga njama za kumdhuru Katibu Mkuu huyo wa Chadema.“Kimsingi tuhuma hizi ni za kipuuzi, lakini uongo huu usipojibiwa unaweza kugeuzwa kuwa ajenda na chama hiki cha Chadema kwa kukosa ajenda zingine za maana.

“Hakuna asiyejua kuwa Chadema kwa sasa kinapumulia mashine, hivyo maneno na matendo yao kwa sasa lazima yalenge kujaribu kujinasua na balaa la kufa kwa chama hicho.“Ni vizuri Watanzania wakakumbuka historia ya tuhuma lukuki zilizowahi kutolewa na Katibu Mkuu huyu wa Chadema tangu aanze siasa na ambazo zote zilikujathibitika kuwa ni za uongo,” alisema Nape katika taarifa hiyo ya CCM.

Akitolea mfano Nape alisema akiwa Singida katika kampeni za urais za mwaka 2010, Dk Slaa aliwatangazia wananchi mkutano kwamba kulikuwa kumekamatwa lori kubwa la mizigo lililojaza karatasi za kura za urais zilizokuwa tayari amepigiwa kabisa mgombea urais wa CCM, Dk Jakaya Kikwete.

“Katika kuonesha kwamba alikuwa na uhakika wa jambo hilo, alisema hadi namba za lori hilo na tela lake kisha akasema lilikamatwa katika mji wa Tunduma, Mkoa wa Mbeya wakati likiingia kutoka Lusaka Zambia. Lakini Polisi baada ya kulikamata na kulipekua hadharani lilikutwa na shehena ya vipodozi vya akina mama na manukato.” CHANZO: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment