Pages

Monday, April 13, 2015

Askofu Gwajima Akana Utajiri Wake....Asema Nyumba, Magari na Chopa ni Baraka za Mungu..

ASKOFU Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, amesema yeye si tajiri kama inavyodhaniwa, bali alichonacho ikiwa ni pamoja na nyumba, magari na helikopta ni baraka tu za Mungu, lakini kama ni utajiri, anatarajia siku moja utamshukia.

Aliyasema hayo jana wakati akihubiri kanisani kwake Kawe,
Dar es Salaam, ambako alisema anawashangaa watu wanaomfuatilia maisha yake huku wakisema yeye ni tajiri mkubwa.

“Wanaodai mimi ni tajiri wana wivu tu na wananionea, mimi si tajiri, bali ni masikini kama walivyo masikini wengine. Natarajia kutajirika hapo baadaye waumini wangu wakiwa matajiri, siwezi kutajirika kama waumini wangu bado ni masikini, nitatajirika pamoja nao,” alisema Gwajima.

Kuhusu mgogoro unaoendelea baina yake na Jeshi la Polisi, Askofu Gwajima alisema yeye anauona kama ni vita vya kiroho na hivyo ataendelea kumwomba Mungu ili amsaidie kupambana na kilichopo mbele yake na anaamini kuwa atashinda vita hiyo kwa uweza wa Mungu anayemtegemea.

“Mungu wangu na awasamehe wote wanaonituhumu kuwa mimi ni tajiri na kuamua kudhoofisha huduma, nasema huduma yangu haitakufa kamwe na wala hatutayumba katika mipango yetu ya kuhubiri injili. Tutapigana kwa uweza wa Mungu na tutashinda kama alivyosema kuwa tutapigana pamoja naye na tutashinda,” alisema Gwajima.

Akizungumzia afya yake, Askofu Gwajima alisema kwa sasa anaendelea vizuri na anaweza kusimama na kutembea, kuhubiri kama ilivyokuwa hapo awali na hatarajii kurejea tena kwenye kiti cha baiskeli ya magurudumu matatu bali atasimama imara daima.

Kuhusu kupeleka nyaraka kadhaa anazotakiwa aziwasilishe polisi siku ya mahojiano Aprili 16, mwaka huu, Askofu Gwajima alisema suala hilo bado wanasheria wake wanalishughulikia na wataendelea kufuata taratibu zote zinazotakiwa na jeshi hilo.

Gwajima anatakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu za hati ya usajili wa kanisa lake, namba ya usajili wa kanisa, hati ya umiliki wa helikopta, hati ya nyumba anazomiliki, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake pamoja na hesabu za fedha za kanisani kwake zinazohusu mapato na matumizi.

Nyaraka zingine ni majina ya Bodi ya Udhamini wa kanisa, mpiga picha za video kanisani kwake siku ya ibada na shughuli zingine za kanisani hapo pamoja na waraka wa Maaskofu uliosomwa makanisani ambao Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo alioupinga na kusababisha yeye kumkashifu kiongozi mwenzake huyo wa dini.

Akionekana kuwa makini sana na lugha anayotumia wakati wa kuhubiri, Gwajima aliwaomba waumini wake waendelee kufuatilia kila sehemu na kuchunguza mambo yote mabaya yanayosemwa juu yake na kanisa lake na kuyaripoti kwake au kwa uongozi wa kanisa ili wayafanyie kazi mara moja kabla hayajaleta madhara.

“Nawaombeni sana mfuatilie kila chanzo cha habari na kuchunguza mambo yote yanayosemwa juu yangu au kuhusu kanisa na kuyaleta mara moja hapa kanisani ili tuyafanyie kazi kabla hayajaleta madhara makubwa,” alisema Gwajima.

Aliongeza kuwa, “tuendelee kuwa na umoja katika kipindi hiki ambapo shetani anataka kupigana nasi ili tuweze kushinda. Tukifarakana hatutaweza bali tukiwa kitu kimoja tutasonga mbele na kuwa huru”.

Utajiri wake

Wakati akikana kuwa tajiri, mwanzoni mwa mwaka jana alifanya mahojiano na gazeti hili na kukiri Mungu anambariki, ndiyo maana mambo yake yanamnyookea.

Aliyasema hayo alipokuwa anazungumzia mpango wake wa kununua helikopta kwa ajili ya huduma za injili ndani na nje ya nchi.

Alikiri kutokana na utajiri anaosema unatokana na baraka za Mungu, anamiliki jumba la ghorofa nne eneo la Mbezi Beach katika Manispaa ya Kinondoni.

Pia amewanunulia wachungaji wake 40 magari ya kutembelea kwa bei tofauti, yakiwemo ya chini ya Sh milioni 10 na mengine ya zaidi ya Sh milioni 20.

“Ni kweli nimewanunulia magari, unajua moja ya misingi yangu ya maisha ni kwamba, mimi siwezi kuishi maisha mazuri, wakati wachungaji wangu wanadhalilika, nimewanunulia magari karibia 40. 

Lakini nina wachungaji wa ngazi mbalimbali, hawa ni wale wa juu, wengine wachungaji wadogo wapo zaidi ya 670, hawa ni watenda kazi muhimu na wanatofautiana kwa ngazi zao, ndio maana kazi ya Mungu inasonga mbele hata nisipokuwepo,” alisema Gwajima.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment