Pages

Monday, April 13, 2015

MAKUBWA MAKUBWA!! Mtoto Aliyefariki na Kuzikwa Agosti Mwaka Jana Arudishwa Akiwa Hai..

Wakazi wa Kibamba Mjimpya, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa wamefurika nyumbani kwa Emmanuel Joseph (32), ambaye ni baba wa mtoto aliyedaiwa kufariki dunia mwezi Agosti, mwaka jana.
Wakazi wa Kibamba Mjimpya, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana walifurika nyumbani kwa Emmanuel Joseph (32), kushuhudia maajabu ya tukio la kufufuka kwa mtoto aliyedaiwa kufariki dunia mwezi Agosti, mwaka jana.

Mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja nusu (jina linahifadhiwa), inadaiwa alizikwa katika makaburi ya Mlongazila.

Anadaiwa kufariki Agosti 7, mwaka jana baada ya kuugua ghafla na kuishiwa damu.

Mtoto huyo anadaiwa kurudishwa akiwa hai na Juma Nakochinya (33) maarufu kwa jina la Bino, mkazi wa eneo la Pandambili mkoani Dodoma ambaye hutibu kwa njia ya maombi.

MAMA MZAZI AFUNGUKA
Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto  huyo, Hellena Mtoro (23) , alisema ilikuwa siku ya Jumamosi majira ya saa 11:00 jioni ambapo mwanawe akiwa na umri wa miezi tisa alizidiwa ghafla na kumkimbiza hospitali ya Mbezi kwa matibabu.

Alisema baada ya kufika hospitalini hapo, vipimo vilionyesha ameishiwa damu hivyo alihamishiwa hospitali ya Tumbi, iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

“Madaktari walijitahidi kadiri ya uwezo wao kutafuta mishipa ya damu maeneo tofauti ya mwili ikiwamo kichwani, cha ajabu mishipa ilikuwa ikionekana lakini ilikuwa inavimba, wakati madaktari wakihangaika, ilipofika saa 6:00 usiku alifariki dunia,” alisema.

Hellena alisema taratibu zote za maziko zilifanyika na walimzika kwenye makaburi ya Mlongazila yaliyopo karibu na eneo analoishi.

Alisema baada ya kuzika siku tatu baadaye walielekea Dodoma kwa ajili ya kumaliza msiba na kurudi Dar es Salaam.

“Ukweli ni kwamba kifo cha mtoto wangu kilikuwa sio cha kawaida, hivyo tulianza maombi na mume wangu, tulikuwa tunasali kwa Nabii Flora Peter, ambaye baada ya kumweleza mazingira ya kifo hiki, alimuweka kwenye maombi na kututaka tumpelekee picha yake,” alisema na kuongeza:

“Baada ya maombi alitueleza kuwa anamuona mtoto wetu yupo hai na anaamini atarudi siku moja. Tuliendelea na maombi na siku moja nilikutana na mama Mariamu ambaye baada ya kumwelezea kifo cha mtoto wangu, aliniambia kuna kijana anaitwa Bino ambaye anaweza kumrudisha kama alikufa kichawi,” alisema.

Alisema mama huyo alimpa namba ya mtu huyo na alipowasiliana naye, Bino alimtaka ashike Sh. 100.

“Nilifanya hivyo na baada ya dakika tano tukiwa bado hewani, alinijulisha kuwa mtoto wangu anamuona yupo hai hivyo akanitaka niende kesho yake Dodoma kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ya kumrudisha,” alisema.

Hellena alisema siku iliyofuata alisafiri kuelekea Dodoma na aliwasili saa 10:00 jioni ambapo alienda moja kwa moja kwa mganga huyo.

“Saa 1:00 jioni Bino alichukua mwiko, ungo na kinu, vifaa anavyovitumia kwenye kazi yake. Ungo aliuweka chini na akaanza kusoma dua kisha nikamuona mtoto amekaa ndani ya ungo ule, nilishtuka sana baada ya kumwona akiwa hana hata nguo, amechafuka na aliyechoka,” alisema.

Alisema baada ya tukio hilo, mtoto alibaki kwa mganga huyo kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.

Alisema alikaa kwa mganga huyo kwa muda wa siku mbili na kurudi Dar es Salaam na kumuacha mtoto huko kama alivyotakiwa.

“Jana (juzi)  aliletwa na Bino ili aje kutusalimia kwa kweli nashukuru Mungu kwa sababu hali ya mwanangu inaendelea vizuri, afya yake ipo vizuri, ” alisema.

Alipoulizwa kama anaamini tukio zima la kurudishwa kwa mtoto wake, Hellena alisema yeye ni Mkristo na kabla ya kwenda huyo alianzia kanisani na maono yalionekana yupo hai.

Aliongeza kuwa, anaamini kilichofanyika ni kutoka kwa Mungu kwa sababu mtu huyo hatumii matunguri zaidi ya kumuomba Mungu kisha kufanya kazi zake.

BABA: HII NI MIUJIZA
Baba wa mtoto huyo, Joseph, alisema kuwa tukio hilo ni la kwanza na la aina yake kwenye ukoo wao na kwamba lilipotokea hakuna aliyeamini hadi walipomuona mtoto.

Alisema baada ya mtoto wake kuletwa, majirani ambao walishiriki kwenye msiba wake, walishtuka na kujaa nyumbani kwake kitendo ambacho kiliwalazimu kwenda polisi kutoa taarifa ya kile kilichotokea.

Alisema baada ya kufika Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa Luis, walihojiwa pamoja na Bino na baadaye kuruhusiwa kurudi nyumbani.

BINO ANENA
Nakochinya maarufu kama Bino alisema kuwa, tukio la kuwarudisha watu wakiwamo watoto kwenye ulimwengu wa kawaida, sio la kwanza.

Alisema kuwa miongoni mwa watoto aliowarudisha na kuwakabidhi kwa wazazi wao idadi yao kwenye mabano ni pamoja na Mtongani Kunduchi (1), Mtwara (2), Mbagala (1), Masasi (1) na Nachingwea (1).

Alisema ana mwaka mmoja toka aanze kazi hiyo na anaifanya kwa kutumia maombi.

Alisema idadi ya aliowasaidia ni zaidi ya watu 150 wakiwamo watoto na vijana na kwamba baadhi yao bado anaendelea kuishi nao kwa matibabu zaidi.

“Mtu anapokuja kwangu kama alivyofanya huyu mama, mizimu ikikubali nitoe huduma mhusika hutakiwa kutaja majina yake na huyo aliyefariki kisha huwa namtaka atoe Sh. 100 ambayo huitumia kumwangalia aliyekufa alipo, anapoonekana aliyefuata huduma yangu hutakiwa kutoa Sh. 30,000 ya mkoba ambayo ni sadaka,” alisema.

Alisema mtoto huyo bado yupo mikononi mwake kwa matibabu zaidi, atakapomaliza atamkabidhi rasmi kwa wazazi wake.

JIRANI
Alfonce Eneliko alisema kuwa, alishiriki kwenye msiba wa mtoto na ameshtuka baada ya kumuona kwenye nyumba hiyo tena.

“Jana (juzi) jioni niliporudi kutoka kwenye shughuli zangu nilisikia mtaani watu wakiongelea kuhusu tukio hili la mtoto, nilipofika hapa kweli nikamuona na aliniambia haya ni maajabu ya Musa, mtoto hajabadilika sura zaidi ya kukua, “ alisema.

Aidha, NIPASHE ilizungumza na msichana mmoja aliyejitambulisha kama Jennifer Mwenda (23), mwenyeji wa Njombe, ambaye alisema aliambatana na Bino kumleta mtoto huyo kwa wazazi wake, kuwa naye alisimuliwa kuwa alifariki dunia akiwa na ujauzito na kurudi kwenye uhai baada ya kuombewa na kijana huyo.

Jennifer alisema nyumbani kwa Bino wanaishi ndani na wale waliopona hutoka na kutembea mitaani hata dukani.

Mjumbe wa nyumba kumi Michael Yuso, alisema kuwa bado hajapokea taarifa rasmi za tukio hilo zaidi ya kumshuhudia mtoto huyo jana.

“Kweli nimemuona na cha ajabu mwaka jana mimi ndiye niliyeshughulikia eneo la kuzikwa na alizikwa kweli, lakini hichi kilichotokea ni kitendawili naendelea kufuatilia zaidi,” alisema.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Agustino Senga, alithibitisha jeshi hilo kupokea taarifa za mtoto huyo na kueleza kuwa, hatua za awali za kiuchunguzi zinaendelea ikiwa ni pamoja na kujiridhisha kama alizikwa kweli, alitibiwa hospitali gani hadi umauti ulipomkuta.

Pia alisema wanafuatilia kujua kama kweli wazazi hao wana cheti cha kifo cha mtoto huyo ndipo hatua nyingine zitakapoendelea.

WENGINE WAVUTIKA
Mmoja wa wanaume waliokuwepo nyumbani hapo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa, anafanya utaratibu wa kwenda kwa mganga huyo kumwangalia mtoto wake ambaye alifariki miezi kadhaa iliyopita kwa kifo cha utata.

“Uchawi upo vifo vingine havitokani na kusudi la Mungu, ndugu zetu wanapotea katika mazingira kama haya lakini kwa sababu hatuna wa kutusaidia basi wanabaki wakiteseka huko walipo, mwanangu alikufa katika mazingira yasiyopishana na huyu, nataka kujiridhisha,” alisema.

No comments:

Post a Comment